Kila mtu aliye hai, tayari anazo sababu nyingi sana za kumsukuma yeye kufanikiwa. Kwa bahati mbaya sana, wengi hawafanikiwi kwa sababu hizo sababu ambazo ndiyo zingewapa mafanikio, wanakubali ziwe kikwazo cha mafanikio yao.

Mwalimu mmoja amewahi kusema inapokuja kwenye kile ambacho mtu anakitaka hasa, hakuna mtu mvivu wala mzembe. Alitoa mfano kwamba ukimchukua mtu ambaye unadhani ni mvivu na mzembe kabisa, kisha ukampeleka kwenye kina kirefu cha maji na kumzamisha kwa nguvu, atatumia kila nguvu kutoka kwenye maji hayo. Hiyo ni kwa sababu anakuwa amekosa kitu anachokitaka zaidi, ambacho ni pumzi.

Mwalimu huyo akahitimisha akisema pale mtu anapoyataka mafanikio kama anavyotaka kupumua, hakuna kinachoweza kumzuia kufanikiwa. Atakutana na vikwazo na changamoto, lakini vyote atavuka na kupata kile anachotaka.

Na hapo ndipo ninapotaka kukuonyesha wewe rafiki yangu kwamba tayari unazo sababu za kupata mafanikio makubwa. Sababu hizo ni vile vikwazo ambavyo unakutana navyo sasa kwenye maisha yako. Yaani ugumu wowote unaokutana nao na kudhani unakuzuia kufanikiwa, huo ndiyo unapaswa kuwa sababu ya wewe kufanikiwa.

Je ni fedha huna? Vizuri, kukosa kwako fedha ndiyo inapaswa kuwa sababu ya wewe kuzitafuta zaidi.

Upo kwenye ajira ambayo haikulipi vizuri? Safi, tumia hiyo kama sababu ya kuwa bora zaidi na kutumia njia mbadala kuongeza kipato chako.

Biashara yako haina wateja? Sawa, tumia hiyo kama sababu ya kukusukuma kuwafikia wateja wengi zaidi kwenye biashara yako.

Kwa walio wengi, pale wanapokutana na ugumu au changamoto, wanaona ndiyo mwisho wa safari. Kwako wewe hupaswi kuwa hivyo, tumia ugumu na changamoto kama kichocheo.

SOMA; Hiki unachokutana nacho mara kwa mara siyo mwisho wa malengo yako.

Mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius alikuwa na kauli maarufu aliyokuwa anasema kikwazo unachokutana nacho kwenye njia yako, kinapaswa kuwa ndiyo njia ya wewe kufika kule unakotaka kufika. Akimaanisha kwamba hupaswi kukubali kukwamishwa na chochote kwenye safari ambayo umeamua. Kila kikwazo unachokutana nacho, kifanye kuwa sababu ya wewe kufanikiwa.

Kama ambavyo moto mkali unaowaka, huwa unatumia kila kinachoingia kwake kama nishati. Hata ukimwaga maji kwenye moto mkali, hauyazimi, bali unayachochea zaidi. Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa pia, taka sana kile unachotaka kiasi kwamba pale unapokutana na changamoto, inakuwa kichocheo kwako kupata unachotaka.

Kamwe usikiri unyonge, usikubali kukwamishwa na chochote pale unapokuwa umeamua kweli kile unachotaka kupata. Hakikisha unapata kile unachotaka au unakufa ukiwa unakipambania. Chochote tofauti na hapo usikipe nafasi kabisa.

Uzuri ni kwamba, pale unapokataa chochote usichotaka, basi unaishia kupata kile unachotaka. Hiyo ina maana watu wengi kwenye maisha wamepata vile wasivyotaka kwa sababu wamevikubali hivyo. Wewe ukikataa kata kata chochote usichotaka, utaishia kupata kile unachotaka hasa.

Tayari unajua unachotaka, vizuri, sasa wajibu wako ni kupambana mpaka upate hicho unachotaka bila kukubali kuishia njiani. Usiruhusu kikwazo chochote kikuzuie. Ndiyo utakutana na vikwazo vingi, lakini vyote vigeuze kuwa kichocheo kwako kupata hicho unachotaka.

Ukishaamua ni wapi unataka kufika, usibadili yale maamuzi. Badili njia unazotumia kufika, lakini usibadili safari. Maana unapobadili safari unakuwa umekiri kushindwa na ukishakiri kushindwa kwenye kitu kimoja itakuwa mwendelezo kwako kushindwa kwenye vitu vingine vingi.

Kataa kushindwa, kataa kuzuiwa na chochote, tumia kila kikwazo kama sababu ya kufanikiwa. Na hata pale unapopata matokeo ambayo hukuyategemea, yatumie kama funzo kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.

Nakuamini sana rafiki yangu, najua unaweza kuyapata mafanikio makubwa kwa sababu kuna vikwazo mbalimbali vinavyokukabili. Vitumie hivyo vizuri ili uweze kufanya makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.