Huenda ukisikia neno utapiamlo linawekwa pamoja na mafanikio unashangaa. Hiyo ni kwa sababu unaweza kujiona huna utapiamlo, bali una afya njema. Ni kweli kimwili unaweza usiwe na utapiamlo, japo hilo unaweza usiwe na uhakika nalo sana. Lakini kuna utapiamlo mwingine ambao umekuwa kikwazo cha mafanikio yako.

Utapiamlo huo umekuwa unakukwamisha wewe kuziona fursa kubwa na nzuri kwako kuweza kufanya makubwa zaidi. Utapiamlo huo umepelekea ufanye mambo kwa mazoea na kwa muda mrefu bila ya kupata manufaa yoyote makubwa.

Utapiamlo ninaouzungumzia hapa rafiki yangu ni wa akili. Ndiyo, utapiamlo wa akili. Huenda unashangaa kwa sababu hujawahi kusikia kwamba kuna utapiamlo wa akili.

Kabla hatujazungumzia utapiamlo wa akili, turudi kwenye utapiamlo wa mwili ambao utakuwa rahisi kwako kuelewa. Utapiamlo ni pale mwili unapokosa virutubisho fulani au inapokuwa na virutubisho fulani kwa kuzidi. Hivyo mtu mwenye uzito mdogo sana ana utapiamlo, wakati pia mwenye uzito mkubwa sana ana utapiamlo pia.

Inapokuja kwenye akili, utapiamlo ni pale akili inapokosa maarifa sahihi au inakuwa na maarifa yasiyo sahihi kwa wingi. Na utapiamlo huo wa akili huwa unasababishwa na mtu kutokujifunza maarifa sahihi au kuingiza yasiyo sahihi kwa wingi.

Mtu ambaye hasomi vitabu na kujifunza mambo yenye tija ana utapiamlo wa akili. Akili yake inakuwa na ukomo ni nini anaweza kuona au kufanya. Hilo linamkwamisha asiweze kufanya makubwa.

Mtu ambaye anafuatilia zaidi habari na mambo mengine yasiyokuwa na manufaa kwake pia anakuwa na utapiamlo wa akili. Anakuwa na maarifa mengi hasi ambayo yanampa mtazamo hasi na kumkwamisha kufanya makubwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimeelezea kwa kina huu utapiamlo wa akili na jinsi unavyoweza kuuepuka ili uweze kufanya makubwa na kupata mafanikio unayoyataka. Karibu ujifunze kwenye kipindi hiki na ukachukue hatua ili kuwa bora.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.