Mafanikio ni safari ambayo kila mtu kwenye maisha huwa anajikuta kwa lazima. Nasema kwa lazima kwa sababu unazaliwa, unalelewa na wazazi au walezi wako. Kisha baada ya kufika umri fulani unaambiwa sasa unatakiwa ukajitegemee. Hapo ndipo kipenga cha safari kinapokuwa kimepulizwa, lakini kwa bahati mbaya sana unakuwa umeingia kwenye safari ambayo huna maandalizi.

Unakuwa umeambiwa tu kwamba unatakiwa ujitegemee na kuyajenga maisha yako, lakini hakuna anayekupa ramani nzima ya safari. Ni kama tu unaingia kwenye basi ambalo lina watu, lakini hakuna anayejua basi hilo linaelekea wapi. Ila cha kushangaza sasa, kwenye kila kituo kuna watu wanashuka na wengine wanapanda.

Unaweza kuona kama wewe ndiyo hujui unakoenda, wakati wengine wote wanajua. Lakini siyo kweli, wengi walio kwenye hilo basi wapo kama wewe tu, wamejikuta kwenye safari ambayo hawakuwa na maandalizi nayo.

Unaweza kulaumu kwa kuwekwa kwenye safari bila maandalizi, lakini ukweli ni unatakiwa kushukuru hata kwa kuwekwa kwenye hiyo safari. Maana wapo wengi ambao hawapati hata nafasi kama uliyopata wewe.

Na jambo jingine, hakuna anayejua nini hasa unataka kwenye maisha yako na nini hasa unaweza kufanya. Hivyo wanaishia tu kubashiri labda unataka au unaweza vitu fulani.

Hiyo ndiyo maana, pamoja na yote, ni wewe ndiye unayetakiwa kuamua nini hasa unataka kwenye maisha yako na nini unachoweza kufanya.

Ukijikuta kwenye hatua yoyote ya maisha yako unawauliza wengine nini unataka au nini unaweza kufanya, jua kabisa umeshashindwa kabla hata ya kuanza. Hakuna yeyote anayeweza kukuambia hayo mawili kwa uhakika isipokuwa wewe mwenyewe.

Iwe ni wazazi, walimu, washauri, watabiri na wengine waliojivika mamlaka mbalimbali, mamlaka zao zinaishia kwenye yale wanayofanya. Mamlaka zao hazina nguvu kwako. Mamlaka yenye nguvu kwako ni wewe mwenyewe. Na kama utashindwa kutumia mamlaka hiyo, hakuna kingine kitakachoweza kukusaidia.

SOMA; Hii ndiyo zawadi kuu unayopaswa kujipa wewe mwenyewe kwa ajili ya mwaka 2022.

Wakati naanza huduma hii ya mafunzo, ushauri na ukocha, nilikuwa nakutana na watu wengi wanaoomba ushauri wafanye nini na maisha yao. Nilikuwa napenda kuwashauri watu hao na kuwaeleza nini hasa wanaweza kufanya, baada ya kuwa nimewauliza maswali mbalimbali. Lakini baada ya muda, nakuta bado hawafanyi yale tuliyoshauriana wafanye.

Na hapo ndipo nilipojifunza kwamba kama mtu hajui nini hasa anachotaka, na hilo likatoka ndani yake mwenyewe, hakuna namna anaweza kufanikiwa kwa kitu cha kuambiwa kutoka nje yake.

Ni lazima mtu akitake kitu hasa, kutoka ndani yake ndiyo aweze kukipigania mpaka kukipata bila ya kukatishwa tamaa na mambo mbalimbali anayokutana nayo. Ambaye anafanya kwa kushauriwa au kuiga wengine, hawezi kustahimili magumu anayokutana nayo kwenye safari yake.

Kitu kingine nilichojifunza na kikanishangaza ni kwamba hakuna ambaye hajui nini hasa anachotaka. Kila mtu anajua kabisa nini anataka. Kila mtu ndani yake kuna sauti inayomwambia nini anataka. Wengi wanaoomba ushauri kwa nje, wakisema hawajui nini wafanye, ni kwa sababu hawajiamini wao wenyewe vya kutosha. Wanadharau sauti yao ya ndani na kutaka kusikiliza sauti ya nje. Na hilo ndiyo linafanya safari ya mtu kuwa ngumu zaidi.

Mtu akishadharau sauti yake ya ndani na kusikiliza sauti za nje, safari yake inakuwa ngumu sana. Hiyo ni kwa sababu kila anapokutana na magumu au kushindwa, sauti ya ndani inamsuta sana. Inamwonyesha kwamba ameidharau na kuhangaika na mengine, ambayo yanamkwamisha. Matokeo yake ni mtu kujikuta anahangaika na mambo mengi, lakini hafanikiwi kwa sababu anayohangaika nayo siyo sahihi kwako.

Unaweza kuomba ushauri kwenye mambo mengi na ukakusaidia sana kwenye safari yako ya mafanikio. Lakini unapojikuta unaomba ushauri wa nini utake kwenye maisha yako na nini unaweza kufanya, jua tayari umeshindwa kabla hata hujaanza. Hivyo vitu vipo ndani yako, huwezi kuvipata kwa nje.

Swali ni unawezaje kuvipata vitu hivyo ndani yako? Jibu ni rahisi, kwa kujisikiliza wewe mwenyewe. Ndani yako tayari kuna sauti inayokuambia mambo hayo, ni wewe kuwa mtulivu na kusikiliza. Acha kuhangaika na usumbufu unaokupoteza. Jisikilize wewe mwenyewe na chukua hatua sahihi ili kufanikiwa.

Jua kwa hakika kile unachotaka kwenye maisha yako, jua yale unayoweza kufanya kisha yafanye kwa uhakika ili kupata unachotaka. Omba ushauri kwenye mikakati na mbinu za kufanya kwa ubora zaidi kile ambacho umeshachagua kufanya na ushauri huo utakuwa na manufaa makubwa kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.