Uko hapa kwa ajili ya kujifunza na kuchukua hatua ili uweze kupata mafanikio makubwa. Huenda umeshajaribu njia mbalimbali, lakini zote unaishia pale ulipoanzia, ukiwa hujafanikiwa.
Licha ya kufanya kila ulichoelekezwa kufanya ndiyo ufanikiwe, bado mafanikio yanakuwa magumu kwako. Mpaka unaanza kuamini huenda kuna namna wale waliofanikiwa wanatumia nguvu zisizo za kawaida kupata mafanikio yao.
Nataka nikutoe wasiwasi, kama unasoma hapa kwanza jipongeze, maana umefika mahali sahihi ambapo mafanikio kwako itakuwa kitu cha lazima. Unachopaswa kufanya ni wewe kujifunza, kisha kuchukua hatua kwa msimamo bila kuacha, huku ukiboresha na utayapata mafanikio.

Maarifa kuhusu mafanikio ni mengi, na wakati mwingine yanachanganya. Maana kuna wakati utaambiwa fanya hivi, na kwingine unaambiwa usifanye hivyo bali vile. Haya huwa yanachanganya watu wanaojaribu vitu vingi kwa wakati mmoja.
Kitu kimoja nilichojifunza kuhusu mafanikio ni njia za kufanikiwa ni nyingi. Lakini ili mtu ufanikiwe, lazima uchague njia moja na ukae kwenye hiyo kwa muda mrefu bila kuacha. Tabia ya watu kujaribu njia kwa muda mfupi na wakiona haifanyi kazi wanakimbilia njia nyingine ndiyo imekuwa inawakwamisha sana.
Hapa nakwenda kukushirikisha njia moja ya uhakika ambayo ukiifuata hiyo tu na kuachana na nyingine zote, kwa muda mrefu bila kuacha, mafanikio yanakuwa ni ya uhakika kwako.
Njia hii ina hatua kuu nne;
Hatua ya kwanza ni LENGO.
Kwenye lengo ndiko unaeleza nini hasa unachotaka kupata au kufikia. Unaweza kushangaa jinsi hatua hii ilivyo rahisi, lakini watu 9 kati ya 10 unaopishana nao kila siku, hawajui kwa hakika nini wanataka. Utawaona wakiwa na haraka kama vile kuna mahali wanawahi, wakati hakuna lolote. Sana sana wanasukumwa na mahitaji wanayokuwa nayo, ambayo wakishayatimiza wanaridhika na kurudi kwenye maisha ya kawaida.
Bila ya malengo, tena ambayo ni makubwa sana ambayo mtu umeyaweka, huwezi kufanikiwa. Utaishia kuhangaika na kila linalokuja mbele yako ila hutadumu kwa muda mrefu, kwa sababu utakapokutana na magumu, utaacha.
Hatua ya pili ni MPANGO.
Mipango ni namna unavyokwenda kutekeleza malengo uliyoyaweka, hatua kwa hatua. Hatua hii pia ni rahisi kusema, lakini ngumu sana kutekeleza. Nikupe mfano mdogo, kama unafanya biashara, je umewahi kukaa chini na kuandika mpango kamili wa biashara yako? Jibu unalo. Sasa hebu jaribu kwenda kuomba mkopo wa biashara benki na cha kwanza watakuuliza mpango wako. Swali jingine, je unaweza kujenga nyumba bila ya kuwa na ramani? Yaani uanze tu kupanga matofali na nyumba ijitokeze?
Unaona jinsi ambavyo mpango ni muhimu kwenye mafanikio yoyote yale. Kwa sababu huo ndiyo unaongoza nini kifanywe na nini kisifanywe ili kufikia malengo yaliyopo. Mpango ndiyo unakudhibiti usipotee kwa mambo yasiyokuwa na tija. Ukishaweka mpango, unapaswa kuufuata kama ulivyouweka ili uweze kufanya kazi.
SOMA; Ndoto, Malengo na Mipango.
Hatua ya tatu ni IMANI.
Hatua mbili za kwanza tulizoona, ni rahisi sana kuzisemea na hata kuzipangilia, lakini hatua mbili za mwisho, zimekuwa ngumu kuzipangilia na hata kuzifanyia kazi. Tukianza na hatua ya imani, imekuwa ni ngumu mno kwa walio wengi na ndiyo chanzo cha wengi kushindwa. Watu wanaweza kuweka malengo na mipango, lakini inapokuja kwenye utekelezaji ni labda hawaanzi kabisa au hata wakianza wanaishia njiani. Hiyo ni kwa sababu wanakuwa hawana imani thabiti juu ya malengo na mipango wanayokuwa wameweka.
Ili uweze kujenga mafanikio makubwa unayoyataka, unapaswa kuamini bila ya shaka yoyote kwamba unakwenda kupata mafanikio hayo. Unapaswa kuyaamini malengo uliyojiwekea ndiyo sahihi kwako na utayafikia, inyeshe mvua au liwake jua. Mpango unaoweka pia unapaswa kuuamini ndiyo uweze kuutekeleza. Ukiwa na mawazo ya aina mbili kwenye kitu chochote, hutaweza kujitoa kukifanyia kazi kweli. Amini bila ya shaka yoyote na utapata msukumo mkubwa wa kuchukua hatua.
Hatua ya nne ni HATUA.
Hatua ya mwisho ni kuchukua hatua kwenye mipango uliyoweka ili kuyafikia malengo. Hapa ndipo mawazo na mipango vinapogeuka kuwa uhalisia. Hapa ndipo vitu visivyokuwepo vinavyozaliwa. Na ndipo pagumu zaidi kwa sababu hapahitaji maelezo zaidi ya utekelezaji.
Uchukuaji wa hatua unapaswa kuwa wa msimamo na kwa muda mrefu bila kuacha. Unapaswa kufanyika kwa kuboresha zaidi kadiri mtu unavyokwenda na matokeo unayoyapata. Hupaswi kufanya leo kama ulivyofanya jana. Badala yake unapaswa kuwa bora kadiri unavyokwenda. Hivyo ndivyo utakavyoweza kutekeleza mpango ulioweka na kufikia malengo uliyonayo.
Fuata hatua hizi nne za uhakika kwenye safari yako ya mafanikio na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. Muhimu ni usikubali chochote kile kikukwamishe kwenye safari yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.