Wauzaji bora kuwahi kutoke, usakaji ndiyo pumzi ya biashara hivyo unapaswa kufanyika mara zote. Kila biashara inapaswa kuwa inatengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote.
Tumeshaona njia kubwa mbili za kusaka wateja wapya wa biashara kupitia kuomba rufaa ambayo ndiyo njia yenye nguvu na ushawishi na pia tumeona njia ya kuwatembelea wateja na kukutana nao ambayo pia ina ushawishi.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza usakaji kupitia kupiga simu, njia ambayo haina ushawishi kama hizo mbili, lakini inaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Hiyo ni kwa sababu upigaji wa simu ukiweza kupangiliwa vizuri unaweza kuwafikia watu wengi kuliko hizo njia nyingine. Kwenye muda ambao mtu anatembelea na kukutana na wateja, anakuwa na ukomo ni watu wangapi anaoweza kuwafikia. Kwa muda huo huo akiutumia kupiga simu, anaweza kuwafikia wengi zaidi.
Kwa mfano kwenye masaa manne ya kutembelea wateja, mtu anaweza kukutana na watu 10, na hapo itategemea umbali na muda wa mazungumzo. Lakini kwa masaa hayo hayo manne, mtu anaweza kupiga simu kwa watu 100. Hivyo ndivyo usakaji kwa simu unaweza kuwa na ufanisi kwenye kufikia wengi na hivyo kufidia ushawishi wake unaokuwa chini.

Aina ya simu za kupiga kwa wateja.
Simu za kuwasiliana na wateja zimegawanyika kwenye makundi matatu.
Kundi la kwanza ni simu za baridi. Hizi ni simu ambazo unapiga kwa wateja ambao wewe huwajui na wala wao hawakujui. Simu hizi huwa zinapokelewa kwa uchache na mapingamizi ni makubwa kwa sababu ya kukosekana kwa imani. Kwa simu hizi, inatakiwa kurudiwa mara nyingi nyingi mpaka wateja kuzoea na kujenga imani.
Kundi la pili ni simu za vuguvugu. Hizi ni simu ambazo zinapigwa kwa wateja ambao tayari wanakujua lakini hawajanunua kwako au walinunua muda mrefu uliopita na kwa sasa hawanunui tena kwako. Simu hizi huwa zinapokelewa kwa wingi, lakini huwa zinakuwa na mapingamizi mengi. Wateja wanakuwa na imani kidogo na hivyo kutokuwa tayari kuchukua hatua. Simu za aina hii zinapaswa kufanywa kwa kurudia rudia ili kujenga imani kwa wateja na kuwafanya wawe tayari kununua.
Kundi la tatu ni la simu za moto. Hizi ni simu za wateja ambao tayari wanakujua na wana imani na wewe. Hawa wanaweza kuwa tayari wananunua au wamepewa rufaa na ambaye ananunua. Simu hizi zinapokelewa kwa wingi na hazina mapingamizi sana, hivyo kukamilisha mauzo ni rahisi kwa simu za aina hii.
Kwenye usakaji wa wateja kwa kutumia simu, lengo lako ni kuwapitisha wateja kwenye hayo makundi, kutoka kuwa wa baridi, kwenda vuguvugu na kuishia kuwa wa moto. Hilo litawezekana pale zoezi la kupiga simu linapofanyika kwa msimamo na kwa ufuatiliaji usiokuwa na ukomo.
SOMA; Mkakati Mkuu Wa Usakaji Endelevu Kwenye Chuo Cha Mauzo.
Orodha ya simu za kupiga.
Usakaji kwa kupiga simu huwa unaanza na orodha ya simu za kupigwa. Hii ni orodha ya wateja walengwa ambao wanapigiwa simu na kuelezwa kuhusu biashara kisha kupimwa kama wanakidhi vigezo vya wateja tarajiwa ili waendelee kufuatiliwa.
Wajibu wa kwanza wa msakaji ni kujenga orodha kubwa ya mawasiliano ya watu ambao watapigiwa simu na kuchujwa ili kupatikana kwa wateja tarajiwa. Zipo njia mbalimbali za kujenga orodha ya wateja walengwa, baadhi ya njia hizo ni kama ifuatavyo;
1. Kuomba rufaa kwa wingi kisha kupata mawasiliano ambayo yatapigiwa simu.
2. Kutembelea wateja na kupata mawasiliano yao.
3. Kuchukua mawasiliano kwenye taarifa mbalimbali zinazopatikana, mfano mabango ya biashara na matangazo mengine.
4. Kuchukua mawasiliano kwenye orodha mbalimbali, mfano wafanyabiashara wa eneo husika, wakazi wa eneo husika n.k.
5. Kuchukua mawasiliano kwenye makundi mbalimbali ambayo watu wanakuwepo, yawe ya makundi ya kukutana au ya mtandaoni.
6. Kujibu matangazo mbalimbali yanayotolewa kama vile ni mteja ili kupata mawasiliano na kuyafuatilia.
7. Kutembelea tovuti na mitandao mingine kupata mawasiliano.
8. Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii na kupata mawasiliano.
9. Kununua orodha ya mawasiliano kwa watu ambao wanauza, kulingana na vigezo vya wateja unaowalenga.
10. Kulipia matangazo ambayo watu wanachukua hatua ya kupiga simu au kutuma ujumbe kisha mawasiliano yao yanatumika kufanya usakaji kwa simu.
Njia ambazo muuzaji au biashara itatumia inategemea na aina ya biashara ambayo inafanya, wateja inaowalenga na bidhaa au huduma zinazouzwa.
Hatua muhimu kwenye kutengeneza orodha ni kuhakikisha orodha inakuwa bora ili wateja tarajiwa wanaopatikana wawe na sifa ambazo biashara inazilenga.
Siyo lazima orodha nzima wapatikane wateja wenye sifa, ukiweza kupata angalau mteja mmoja mwenye sifa kwenye watu 10, orodha ni nzuri. Hapo wengine wakiendelea kufuatiliwa wataendelea kuwa na sifa kadiri muda unavyokwenda.
Zoezi la kujenga orodha ya wateja walengwa linapaswa kuwa endelevu ili kisima kisikauke. Ukikusanya wateja na kuanza kuwafuatilia huku ukiwa huendelei tena kuongeza wengine, utafika mahali na kuwa huna tena wateja wanaofaa kufuatilia.
Lakini kwa kuendelea kuongeza watu kwenye orodha, kila mara unakuwa na wengi zaidi wa kufuatilia.
Namba nzuri ya wastani wa orodha unayopaswa kuwa nayo ni mara 10 ya wateja tarajiwa unaotaka au mara 100 ya wateja kamili unaowataka. Hiyo inamaanisha orodha hiyo inapaswa kuwa kubwa sana ili uweze kupata wateja tarajiwa wenye sifa na wanaokidhi vigezo vya biashara.
Baada ya kuwa na orodha, kinachofuata ni kupangilia upigaji wa simu, kitu ambacho tutajifunza kwenye somo linalofuata.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.