3326; Kabla ya kusema haiwezekani.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Kila kitu huwa hakiwezekani mpaka pale kinapokuw kimefanywa.
Mambo yote mapya na makubwa ambayo yamefanywa na binadamu, kwa kipindi kirefu yalionekana hayawezekani.

Ni mpaka pale walipokuja watu ambao walijua haiwezekani, lakini bado wakaamua kufanya ndiyo walioleta mabadiliko makubwa.
Watu hao walioleta mabadiliko, hawakutaka tu kukubaliana na hali vile ilivyo, bali walitaka kuleta kitu cha tofauti.
Na hilo limekuwa linafanikiwa mara zote na kuwa ndiyo chanzo cha ugunduzi mpya kwenye mambo mbalimbali.

Hivyo ndivyo wewe unavyopaswa kuwa kwenye safari yako ya mafanikio.
Kila unachopaswa kufanya ili upate matokeo unayoyataka, kinakuwa hakiwezekani.
Na wengi wanaokuwa wanakuzunguka wanakiri hilo wazi kwamba haiwezekani.
Utakuwa na ushahidi wa kila aina kwamba haiwezekani.

Lakini bado inakubidi ufanye ili kuleta matokeo ya tofauti na unayopata sasa. Bado ni lazima ufanye ili upige hatua ambazo hujawahi kupiga.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa kwenye maisha yetu.
Kwa kufanya yale ambayo hayawezekani.

Ili kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako, hupaswi kukubali haraka yale unayokutana nayo au matokeo unayoyapata.
Tayari unajua unachotaka, pambania hicho mpaka kukipata.
Usiangalie kitu kingine chochote.
Kwa kila matokeo unayoyapata, angalia namna ya kuboresha zaidi ili kupata yale unayotaka wewe.

Na muhimu zaidi, kabla ya kukubaliana na jambo kwamba haliwezekani, angalau lifanye.
Lifanye kwa msingi wa awali, kwamba kama isingekuwa haijulikani kwamba haiwezekani, lingeweza kufanyikaje?
Kufikiri kwa namna hiyo kunakuwa na nguvu ya kuleta matokeo ya tofauti na yale ambayo yamezoeleka kupatikana.

Kutokuwezekana au kushindikana kwa kitu mara nyingi huwwa siyo kwa milele.
Inaweza kuwa hivyo kwa kipindi fulani tu au katika hali fulani tu.
Kadiri mambo yanavyoenda yakibadilika, ndivyo pia uwezekano unavyokuwa mkubwa.
Hivyo hata kama kitu kilikuwa hakiwezekani jana, leo ni siku nyingine ya tofauti, kinaweza kuwezekana.

Ni kupitia kufanya ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na yale yasiyowezekana huwa inapatikana.
Ukiacha kufanya kwa sababu unaona haiwezekani, unakuwa umekubaliana na hali hiyo kwamba haiwezekani. Na pia unakuwa umeamua isiwezekane kamwe.
Ukifanya licha ya kujua haiwezekani, unajiweka kwenye nafasi ya kuleta matokeo ya tofauti kabisa na ilivyozoeleka.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti kabisa tunayoijenga, ni marufuku kusema kitu hakiwezekani kabla hujakifanya.
Kila unachopaswa kufanya ili kuleta matokeo unayoyataka, unapaswa kukifanya kama vile una uhakika kitafanya kazi.
Hata pale watu wanapotoa maoni mbalimbali juu ya kitu hicho, wewe unapaswa kuwa umetingwa sana na kufanya kiasi cha kutokupata nafasi ya kufuatilia kwa nini haiwezekani.

Ndani ya KISIMA CHA MAARIFA kila kitu kitu kinawezekana. Ndiyo, hakuna kinachoshindikana pale nia ya dhati ya kukipata inapokuwepo.
Kutokuwezekana ni msamiati wa kuwafariji wale ambao hawapo tayari kujitoa hasa ili kupata wanachotaka.
Ndani ya hii jamii ya tofauti hatufarijiani, kwa sababu faraja inalea yale yaliyopo.
Huku tunaambiana ukweli hata kama unauma, ili tuweze kuutumia kuleta matokeo ya tofauti ambayo ndiyo tunayoyataka.

Kuwezekana au kutokuwezekana kwa kitu halipaswi kuwa linakusumbua wewe.
Wewe sumbuka na nini cha tofauti unachofanya na kaa kwenye ufanyaji wake.
Wajibu wako mkuu kwenye maisha ni kupata kile unachotaka au kufa ukiwa unakipambania.
Hupaswi kukubali hali nyingine tofauti na hizo.
Hilo ndiyo litakusukuma wewe kuweza kufanya makubwa na yatofauti.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe