Ubunifu ni hitaji muhimu kwa mtu yeyote anayetaka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yake. Hiyo ni kwa sababu kufanya yale ambayo kila mtu anafanya, huwa unaishia kupata matokeo ambayo wanapata, ambayo pia ni ya kawaida sana.
Ili uweze kupata matokeo ambayo wengine hawayapati, ambayo ndiyo yatakupa mafanikio, lazima ufanye yale ambayo wengine hawafanyi. Na ili uweze kufanya ambayo wengine hawafanyi, lazima uwe na njia ya tofauti ya kuiona dunia. Hapo ndipo ubunifu unapokuwa muhimu.

Watu wengi huwa wanadhani ubunifu ni kwa ajili ya watu wachache waliopewa uwezo huo. Lakini ukweli ni kwamba ubunifu upo ndani ya kila mtu, wengi siyo wabunifu kwa sababu wanashindwa kutumia uwezo huo ambao tayari upo ndani yao.
Leo nakwenda kukushirikisha zoezi ambalo ukilifanya kila siku utaweza kufikia uwezo mkubwa wa ubunifu ulio ndani yako na kufanya makubwa.
Mwalimu mmoja wa sanaa ya uchoraji aliligawa darasa lake kwenye makundi mawili na kutoa mtihani wa kuchora. Masharti kwenye makundi hayo mawili yalikuwa tofauti. Kundi la kwanza waliambia watapewa maksi kwenye ubora wa mchoro, yaani yule atakayechora kwa ubora zaidi ndiyo atapata maksi nyingi zaidi. Kundi la pili waliambiwa watapewa maksi kwa wingi wa michoro, yaani yule atakayekuwa amefanya michoro mingi zaidi ndiye atapata maksi nyingi zaidi.
Zoezi lilifanyika na baadaye michoro ya wanafunzi kukusanywa. Katika kuipitia ndipo jambo la kushangaza lilionekana. Wale walioambiwa watapimwa kwa ubora, walikuwa na michoro michache na mingi haikuwa bora. Wakati wale walioambiwa watapimwa kwa wingi, walikuwa na michoro mingi na baadhi kati ya hiyo ilikuwa na ubora wa hali ya juu. Hivyo kwenye makundi hayo mawili, wale waliofanya kwa wingi ndiyo walionyesha ubunifu zaidi.
Je wewe unajifunza nini kwenye hilo na inakusaidiaje kuwa mbunifu zaidi? Jibu ni moja, unachojifunza ni ubunifu unatokana na kufanya kwa wingi. Hiyo ina maana kwamba hata kama uwezo wako ni wa kawaida, kama utafanya kitu kwa wingi, utaweza kuzalisha matokeo ya kibunifu.
Hivyo ndivyo kila mtu anaweza kufikia na kutumia uwezo mkubwa wa ubunifu ulio ndani yake. Kwa kufanya kile anachofanya kwa wingi, anajiweka kwenye nafasi ya kuzalisha vitu vya tofauti.
SOMA; KIL A MTU NI MBUNIFU, JE UNAUTUMIA UBUNIFU WAKO KUFIKIA MALENGO YAKO?
Katika kufanyia kazi hili, kuna mambo matatu muhimu ya kuzingatia.
Jambo la kwanza ni lazima mtu akubali kwamba katika mengi anayofanya, mengi hayatakuwa na ubora ambao mtu anategemea upatikane. Na hilo halina ubaya wowote, kwa sababu yale machache yatakayokuwa bora, yatafidia mengi ambayo hayakuwa bora. Wengi hukwama kufanya kwa wingi kwa sababu wanataka ukamilifu, wanataka wafanye kila kitu kwa ubora kabisa la sivyo hawafanyi kabisa.
Jambo la pili ni usirudie kile kile mara zote. Kwa kuwa tumejifunza kufanya kwa wingi kunafungua ubunifu, haimaanishi urudie kufanya kitu kile kile kwa namna ile ile. Kufanya hivyo ndiyo unaitwa ujinga. Ndiyo unapaswa kufanya kwa wingi, lakini kila mara unapofanya unapaswa kuboresha zaidi, kufanya kwa namna ya tofauti. Ni kupitia kufanya kwa kuboresha, hata kama ni kidogo ndiyo unaweza kuzalisha matokeo ya tofauti.
Jambo la tatu ni pangilia ufanyaji wako ili ufanye kila mara badala ya kufanya na kuacha. Wengi huwa na nia nzuri ya kufanya jambo kila siku au kila mara, lakini kufanya kwa msimamo bila kuacha ndipo wanakwama. Wengi hufanya pale wanapojisikia na wasipojisikia hawafanyi. Ubunifu hauwezi kuchochewa kwa kusubiri mpaka ujisikie. Hivyo unatakiwa kupangilia ufanyaji wako kiasi kwamba unalazimika kufanya. Tenga kabisa muda wa kufanya na kuwa na namna ya kuwajibishwa pale unapoacha kufanya. Hilo litakusukuma ufanye na kuzalisha matokeo ya tofauti.
Tayari unao ubunifu ndani yako, kama hujaweza kuutumia ni kwa sababu hujafanya kwa wingi vya kutosha. Anza sasa kufanya kwa wingi kama ulivyojifunza hapa na utaweza kufikia na kutumia uwezo mkubwa wa ubunifu ulio ndani yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.