Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji kwenye programu ya NGUVU YA BUKU. Tunaendelea kujifunza kwa kina kuhusu uwekezaji wa mifuko ya pamoja (Mutual Funds) ambapo tunaiangalia mifuko iliyo chini ya UTT AMIS.

Kwenye somo lililopita tulijifunza kuhusu mfuko wa Umoja ambao ndiyo mfuko wa kwanza wa UTT. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza kuhusu mfuko wa Wekeza Maisha. Karibu tujifunze ili tuendelee kuwa bora kwenye uwekezaji na kuwekeza kwa msimamo ili kujenga utajiri mkubwa.

Mfuko wa Wekeza Maisha ni mfuko wa pili kuanzishwa na UTT AMIS na ulizinduliwa mnamo tarehe 16 Mei 2007. Mfuko ulitimiza miaka 10 na kuiva mwaka 2017. Mfuko wa Wekeza Maisha unatoa faida za aina 2 ambazo ni, faida ya kukuza mtaji, pamoja na bima ya maisha kwa wawekezaji. Mfuko unawekeza katika hisa zilizoorodheshwa na maeneo yenye vipato vya kudumu.

Kwa kifupi, mfuko wa Wekeza Maisha unaleta vitu viwili kwa pamoja; UWEKEZAJI na BIMA YA MAISHA. Kwenye uwekezaji thamani inakua na kwenye bima, unapata fidia pale majanga ya kimaisha yanapokukuta.

MALENGO YA MFUKO

Ni mfuko wa wazi wenye lengo la kukuza mtaji  na kutoa faida za; bima ya maisha, bima ya ajali, bima ya ulemavu wa kudumu na gharama za mazishi. Zaidi ya 99% za fedha za wawekezaji wa mfuko wa Wekeza Maisha huwekezwa kwenye masoko mbalimbali ya fedha na 1% ni kwa ajili ya malipo ya bima.

Michango inayokusanywa, sehemu kubwa inawekezwa na ndogo ndiyo inabaki kwa ajili ya kulipa fidia kwa wanaopata majanga.

NANI ANARUHUSIWA KUWEKEZA NA UMRI WA KUINGIA.

Mfuko uko wazi kwa Mtanzania mkazi na asiye mkazi mwenye umri wa miaka 18 hadi 55.

UKWASI/KUUZA VIPANDE

Mwekezaji ataruhusiwa kutoa sehemu ya uwekezaji wake baada ya kudumu kwa miaka 5 katika uwekezaji na ataruhusiwa kutoa kiasi chote baada ya kudumu kwa miaka 10 katika uwekezaji.

Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya 10 za kazi baada ya kupokelewa. Fedha zitatumwa moja kwa moja katika akaunti ya benki ya mwekezaji.

SERA YA MFUKO

Mfuko unaruhusiwa kuwekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa, ikizingatiwa kuwa kiasi cha pesa kitakachowekezwa kwenye sehemu hiyo kisizidi 40% ya uwekezaji wote wa mfuko na 60% iliyobaki huwekezwa kwenye dhamana mbalimbali za serikali zenye ukomo tofauti, hatifungani za kampuni binafsi, na kwenye akaunti za amana.

SIFA ZA MFUKO

1. Watu binafsi wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 55 ndio wanaoruhusiwa kujiunga.

2. Mfuko unaruhusu umiliki wa mtu binafsi tu.

3. Mfuko unatoa fursa za aina mbili za mpango wa kuchangia/kuwekeza:

(a) Kuchangia kwa awamu na

(b) Kuchangia kwa mkupuo

4. Vipande vinauzwa kwa thamani halisi ya wakati huo [hakuna gharama za kujiunga].

5. Mfuko unampa fursa mwekezaji kuwekeza kwa mpangilio maalum. Mwekezaji anaweza kuchagua kuchangia kila mwezi, mara mbili kwa mwaka au mara moja kwa mwaka.

Kiwango cha kuwekeza:

(a) Kiwango cha chini kwa uwekezaji kwa miaka kumi ni TZS. 1,000,000 ambacho kinaweza kuwekezwa kwa awamu au kwa mkupuo.

(b) Kiwango cha chini cha uwekezaji wa awamu ni TZS.8,340 kila mwezi.

(c) Hakuna kiwango cha juu cha uwekezaji, lakini mafao ya bima ya maisha hayatazidi TZS. 25,000,000.

Gharama za kujitoa kwenye mfuko;

a) 2% ya bei ya kipande baada ya miaka 5.

b) Hakuna gharama za kutoka baada ya miaka 10.

Mafao ya bima yanayopatikana ni: –

i. Bima ya maisha,

ii. Bima ya ulemavu wa kudumu,

iii. Bima ya ajali.

Mafao ya bima ya maisha – Kifo au ulemavu wa kudumu.

1. Mpango wa kuwekeza kwa awamu: Kinga ya Bima ya maisha ina thamani sawa na kiasi kisicholipwa na mwekezaji kwa muda uliosalia katika mpango wake wa uwekezaji. (Muhimu: Kiwango cha juu kitakacholipwa ni TZS. 25,000,000).

2. Mpango wa kuwekeza kwa mkupuo: Kinga ya Bima ya Maisha ina thamani sawa na kiwango alichochagua mwekezaji. (Muhimu: Kiwango cha juu kitakacholipwa ni TZS. 25,000,000).

3. Mafao ya bima ya ajali: Mwekezaji atalipwa 20% ya kiwango kilichokusudiwa katika mpango wa uwekezaji, hata hivyo kiwango cha juu kitakacholipwa ni TZS. 5,000,000.

4. Mafao ya Gharama za Mazishi: Kila mwekezaji atalipwa TZS.500,000 kwa ajili ya mazishi endapo atafariki bila kujali kiwango alichowekeza. Mafao haya yatalipwa kwa ajili ya wawekezaji watakaoingia wakati wa mauzo ya mwanzo tu.

5. Kama mwekezaji atakaa kipindi chote cha uwekezaji wake, atapata faida ya mkono wa pongezi ikiwa amechangia michango yote kwa wakati na mwekezaji hakuuza vipande vyake katika kipindi chote cha uwekezaji.

Faida ya mkono wa pongezi ni:

(a) Kwa mpango wa kuchangia kwa awamu – 5% ya kiwango kilichokusudiwa katika mpango wa uwekezaji.

(b) Kwa mpango wa kuchangia kwa mkupuo – 7% ya kiwango kilichokusudiwa katika mpango wa uwekezaji.

FAIDA ZA MFUKO WA WEKEZA MAISHA.

1. Mwekezaji kupata manufaa ya aina mbili, uwekezaji na bima.

2. Mfuko umekuwa na ukuaji mzuri wa thamani kwa kipindi chake chote, wakati mwingine ukiwa ndiyo unaongoza kwa ukuaji ukilinganisha na mifuko mingine.

HASARA ZA MFUKO WA WEKEZA MAISHA.

1. Ukomo kwenye kutoa fedha nje ya kipindi cha uwekezaji, hii inamzuia mwekezaji asiwe huru kuuza uwekezaji wake muda wowote. Japo hilo linawezekana kama mtu akitaka, lakini gharama zake zinakuwa kubwa.

2. Vipande katika mfuko huu haviruhusiwi kuhamishwa kutoka kwa mwekezaji mmoja kwenda kwa mwingine, au kutumika kama dhamana ya mkopo.

MJADALA WA SOMO;

Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kupitia kujibu maswali yafuatayo;

1. Mfuko wa wekeza maisha unaleta pamoja vitu viwili, vitaje na eleza jinsi mwekezaji ananufaika navyo.

2. Mpango wa bima ya maisha kwenye mfuko wa Wekeza maisha unafanyaje kazi? Fidia zinatolewa kwenye maeneo gani na kwa kiasi gani?

3. Unaelewa nini kuhusu bima ya maisha? Je wewe una bima ya maisha? Kama ndiyo ni kwenye bima gani? Kama siyo una mpango gani kwenye hilo?

Shirikisha majibu ya amswali hayo kama sehemu ya kujifunza masomo haya ya uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.