Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya sababu ambazo zimekuwa zinapelekea watu wengi kushindwa kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao, ni kukosa maana. Wengi wamekuwa wanaishi maisha yao hapa duniani kama minyoo, kwa maana kwamba wanazaliwa, wanaishi maisha ya kawaida na wanakufa bila kuacha alama yoyote ile.
Hivyo ndivyo kundi kubwa la watu wanavyoyaendesha maisha yao hata sasa. Utawaona wakihangaika sana na maisha, wanapitia magumu na changamoto mbalimbali. Lakini ukiwauliza yote hayo wanayafanya kwa sababu gani, wanakuwa hawana majibu. Wengi wanakuwa wanayasukuma tu maisha, wakisubiri kufa na kuzikwa.

Huwa kuna swali la utani kwamba mtu anakula ili aishi au anaishi ili ale? Kwa walio wengi, ni dhahiri wanaishi ili wale, kwa sababu shughuli zao zote ni kuhakikisha wanapata chakula. Na wakishapata chakula, basi hakuna tena kingine ambacho kinawasumbua.
Hii ni hasara kubwa sana ambayo jamii ya binadamu inapitia, kwani watu wengi sana wanaopita hapa duniani, wanashindwa kuacha alama ambazo zipo ndani ya uwezo wao kuacha. Na hayo yote yanaanzia kwenye kushindwa kujua maana ya maisha.
Swali la maana ya maisha ni nini limekuwa linaonekana ni la kifalsafa au kidini. Na licha ya kuulizwa na kujadiliwa kwa muda mrefu, halijawahi kupata majibu yaliyonyooka. Na hiyo ni kwa sababu, hakuna maana moja ya maisha kwa watu wote.
Viktor Franklin, ambaye alikuwa daktari wa magonjwa ya akili, alikuwa ni mmoja wa wafungwa wa kivita waliopitia kwenye makambi ya mateso (concentration camps) ya Wajerumani wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.
Kwenye kitabu chake alichoandika, kilichoitwa MAN’S SEARCH FOR MEANING, Franklin ameshirikisha mateso makubwa sana ambayo waliyapitia kwenye makambi hayo na jinsi ambavyo kuweza kubaki hai ilikuwa ni swala la bahati kuliko kingine chochote.
Kupitia mateso hayo na kwa uzoefu wake kwenye saikolojia na magonjwa ya akili, aliona jinsi ambavyo baadhi ya watu waliweza kuwa imara licha ya hayo waliyopitia huku wengine wakiwa dhaifu na kufa, siyo kwa sababu tu ya mateso, bali kwa kukosa matumaini.
Kupitia uzoefu wake wa makambi ya mateso na saikolojia ya binadamu, Franklin ameainisha kuna njia tatu za mtu kuweza kujua maana ya maisha yake. Njia ya kwanza ni kupitia kazi au biashara ambayo mtu anafanya. Njia ya pili ni kupitia mapenzi ambayo mtu anakuwa nayo kwa mtu/watu wengine. Na njia ya tatu ni kupitia mateso ambayo mtu anayapitia.
Hii njia ya tatu ndiyo tutaiangalia hapa na jinsi ambavyo kila mmoja wetu anaweza kuitumia na kuyafanya maisha yake kuwa na maana ili aweze kufanya makubwa.
Iko hivi, hakuna maisha ya mtu yeyote ambayo yamenyooka kadiri ya anavyotaka. Kila mtu kuna magumu, matatizo na changamoto ambazo anakutana nazo kwenye safari ya maisha. Ni jinsi mtu anavyopokea na kutumia hayo anayokutana nayo ndiyo itaamua atakuwa mtu wa aina gani.
Wale ambao wanachukulia mateso wanayopitia kama sehemu ya kutumia uwezo wao wa ndani kuleta matokeo ya tofauti, huwa wanayavuka magumu hayo na kuwa na maisha ya mafanikio. Lakini wale ambao wanayaona magumu wanayokutana nayo kama ndiyo mwisho wa maisha yao, huwa wanaishia kushindwa vibaya.
Franklin anatoa mfano kwenye makambi, kipindi cha kati ya Krismasi na mwaka mpya ndiyo wafungwa wengi sana walikuwa wanakufa. Na haikuwa sababu ya mateso kuwa makali, bali wengi walikuwa na matumaini kwamba Krismasi watakuwa nyumbani. Sasa pale Krismasi ilipofika na kuwa bado kwenye makambi, walikata tamaa na kuona maisha hayana tena maana. Hapo miili yao ilikuwa dhaifu na kuwa rahisi kwao kufa.
Pale unapopitia mateso ya aina yoyote ile ndiyo wakati mzuri wa kuyatumia hayo kuyafanya maisha yako kuwa ya maana. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwaangalia watu ambao wanategemea sana uwepo wako au wanaonufaika sana na kile unachofanya. Hilo ndiyo litakalokusukuma uendelee kupambana licha ya magumu hayo.
Lakini jambo la msingi sana, kama tulivyoona kwenye mfano hapo ni kutokupoteza matumaini, hata mambo yawe magumu kiasi gani. Unapaswa kuendelea kuwa na matumaini makubwa kwamba mambo yatakaa sawa. Ni wewe kuendelea na mapambano ukitegemea mazuri na yatakuja.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha mambo mengi zaidi kutoka kwenye kitabu hicho cha MAN’S SEARCH FOR MEANING, kutoka kwenye mifano ya maisha ya Frankln kwenye makambi ya mateso. Karibu ujifunze kwa kusikiliza kipindi hiki, ili uweze kuishi maisha yenye maana kwako na kujenga mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.