3337; Tingwa na mambo ya kufanya.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna viashiria ambavyo mtu akiwa navyo, anakuwa anadhihirisha kwamba hajatingwa na mambo ya kufanya.
Maana yake anakuwa na muda mwingi na mambo machache ya kufanya.
Muda wa ziada anaokuwa nao, ambao anakuwa hana cha kufanya nao ndiyo anakuwa anautumia kwa mambo ambayo hayana tija kabisa kwake.

Kuwahitaji sana watu na kuwalalamikia kwamba hawapatikani, huku mambo unayowalalamikia nayo yakiwa hayahusu malengo makuu unayofanyia kazi ni kiashiria cha kuwa na muda wa ziada.
Ukiwa umetingwa hasa na yale makubwa unayofanyia kazi, unashukuru pale wengine nao wanakuwa wametingwa, hivyo huwalalamikii kwa kuwakosa.

Kufuatilia yanayoendelea kwenye maisha ya watu wengine, ambayo hata hayahusu yale makubwa unayofanya ni dalili nyingine ya kuwa na muda mwingi kuliko ya kufanya.
Ukiwa umetingwa hasa na makubwa unayofanya, hupati muda wa kuhangaika na maisha binafsi ya watu wengine.

Kuhofia mambo yajayo, ambayo bado hata hujayafikia ni dalili nyingine kubwa ya kuwa na muda mwingi kuliko mambo ya kufanya.
Hapo ndipo muda huo unapotelea kwenye kuhofia mambo ambayo bado hata hujayafikia.
Unapokuwa umetingwa hasa na yale unayofanya sasa, hupati kabisa muda wa kuhofia yale yajayo.
Unajikuta tu umeyafikia na kuyapita bila hata kujua kama yangekuwa magumu au kutokuwezekana.

Kila unapojikuta unahangaika na mambo ambayo hayachangii kwenye malengo makubwa unayofanyia kazi, jua hujatingwa vya kutosha na yaliyo muhimu.
Ongeza majukumu zaidi kwenye hayo unayofanya ili muda wako wote umezwe na majukumu yaliyo muhimu zaidi kwako na siyo vinginevyo.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunaletwa pamoja siyo kwa kuridhishana tu kama kundi, bali kwa yale makubwa tunayofanya.
Ambaye hana makubwa anayopambana nayo, hatumwoni akiwa amejitoa vya kutosha na anakuwa usumbufu kwa kila mtu.
Tunawaepuka wale ambao hawana makubwa wanayopambana nayo kwa sababu wana nguvu kubwa ya kuturudisha nyuma kwenye yale tunayopambania.

Tiketi yako ya kuwa kwenye jamii hii ni yale makubwa sana unayoyapambania, ambayo watu wa kawaida wakiyasikia, wanasema dhahiri kwamba hayawezekani.
Hapo sasa ndipo unatingwa hasa kuhakikisha unawaonyesha yale wanaona hayawezekani, yanawezekana.
Hujali kingine chochote ambacho hakiendani na hayo makubwa sana unayoyapambania.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe