Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji, ambayo yanatupa maarifa sahihi na hatua za kuchukua ili kuweza kujenga utajiri mkubwa kupitia uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo kwa muda mrefu.

Tunaendelea kujifunza kuhusu uwekezaji wa mifuko ya pamoja, uwekezaji rahisi kufanya kwa kila mtu bila kujali uelewa wake kwenye uwekezaji au mtaji alionao.

Pia tunaendelea kujifunza kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja ambayo inasimamiwa na dhamana ya uwekezaji Tanzania ambayo ni UTT AMIS. Leo tunakwenda kuangalia mfuko wa UKWASI. Karibuni tujifunze na kuendelea kupata uelewa mpana ili kuwekeza vyema.

THAMANI YA UTAJIRI (NETWORTH) NA UKWASI (LIQUIDITY).

Kwenye kupima utajiri wa mtu, kinachoangaliwa huwa ni thamani ya utajiri wake wote. Thamani ya utajiri huwa inakokotolewa kwa kuchukua thamani ya mali zote ambazo mtu anamiliki (kwa bei ya soko) na kutoa madeni yote ambayo mtu anayo.

Hiyo ni hesabu ambayo kila mtu anatakiwa kuweza kuikokotoa ili kujua anasimama wapi kwenye utajiri wake. Pale mtu anapokuwa na madeni mengi kuliko thamani ya mali alizonazo, anakuwa amefilisika. Yaani kama kila kitu chake kikiuzwa bado hawezi kumaliza madeni aliyonayo, anakuwa kwenye hali ya kufilisika.

Kwa upande wa pili, UKWASI ni kiasi cha fedha ambacho mtu anakuwa nacho au anaweza kukipata kwa haraka pale anapokuwa anakihitaji. Ukwasi unapima ni kiasi gani cha fedha ambazo mtu anakuwa nacho kwenye wakati husika.

Mtu anaweza kuwa na thamani kubwa ya utajiri, lakini asiwe na ukwasi, na hili ndiyo lipo kwa watu wengi na limekuwa linawafanya wanyanyasike sana, licha ya kuonekana wana utajiri mkubwa.

Chukua mfano wa mtu ambaye ana nyumba, ambayo thamani yake sokoni ni milioni 100, lakini mtu huyo akipata shida inayomtaka awe na milioni 10 ya haraka, anakuwa hana. Na hata akisema auze nyumba hiyo kupata fedha, mteja hawezi kupatikana haraka kama inavyokuwa inahitajika. Hapo mtu atalazimika kuingia kwenye mikopo ili kutimiza hitaji lake.

Kwa hiyo unaweza kuona hapo, mtu ana utajiri (thamani ya milioni 100) lakini hana ukwasi (amekosa fedha kiasi cha milioni 10). Hivi ndivyo hali za wengi zilivyo kifedha na zimekuwa zinawaweka kwenye wakati mgumu sana pale wanapokuwa na uhitaji wa fedha.

Kwa kuona changamoto hiyo ya watu kuwa na thamani kubwa ya utajiri ila wanakosa ukwasi, UTT AMIS waliona fursa ya kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa UKWASI, kwenye lengo la kuwawezesha watu kupata fedha pale wanapokuwa wanazihitaji kwa haraka. Kama ambavyo utajifunza, mfuko huu ndiyo wenye siku chache za kupata fedha pale unapouza vipande, ambapo ni siku 3, ili kuhakikisha mtu anakuwa na ukwasi kweli.

MFUKO WA UKWASI WA UTT.

Mfuko wa Ukwasi ni mfuko wa tano kuanzishwa na taasisi ya UTT AMIS. Mfuko wa Ukwasi ulianzishwa mwezi Aprili 2013. Ni mfuko wa uwekezaji wa pamoja ambao hutoa fursa kwa taasisi na watu binafsi kuwekeza kipato chao cha ziada kwa kipindi kifupi cha kati au muda mrefu kwa faida na ukwasi madhubuti.

MALENGO YA MFUKO

Mfuko wa Ukwasi ni mfuko unaofaa kwa wawekezaji wa muda mfupi, wa kati na mrefu wenye malengo ya kukuza mtaji, kupitia uwekezaji mseto kwenye maeneo yenye mapato ya kudumu (fixed income).

UKWASI/KUUZA VIPANDE

Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya 3 za kazi baada ya kupokelewa. Fedha zitatumwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya mwekezaji.

NANI ANARUHUSIWA KUWEKEZA.

Wawekezaji wote ikiwa ni pamoja na watu binafsi, taasisi, makampuni, na vikundi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

SERA YA UWEKEZAJI

Kiwango chote (100%) kinawekezwa kwenye maeneo yenye dhamana zinazotoa vipato vya kudumu (fixed income securities).

SIFA ZA MFUKO:

1. Ni rahisi kwa mwekezaji kupata fedha zake za mauzo ya vipande, (ndani ya siku 3 za kazi baada ya maombi ya kuuza vipande kupokelewa katika ofisi za UTT-AMIS makao makuu)

2. Mfuko wa Ukwasi hautozi ada ya kujitoa wala kujiunga.

3. Umiliki wa mtu mmoja au umiliki wa pamoja unaruhusiwa katika mfuko huu.

4. Kiwago cha chini cha uwekezaji ni TZS.100,000 na kwa uwekezaji wa nyongeza ni TZS. 10,000.

5. Mfuko unaruhusu uhamishaji wa vipande kutoka mwekezaji mmoja kwenda kwa mwekezaji mwingine.

6. Mwekezaji akifariki, mrithi, mwakilishi au mwombaji wa pili ataruhusiwa kuendeleza uwekezaji huo.

7. Vipande vinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo katika tasisi za fedha.

8. Hakuna ukomo wa kiwango cha juu cha uwekezaji.

SOMA; Uwekezaji Kwenye Mifuko Ya Pamoja (Mutual Funds).

JINSI YA KUPANGILIA UTAJIRI NA UKWASI WAKO.

Kwa watu wengi kukosa elimu sahihi ya uwekezaji, wamekuwa wanafanya uwekezaji ambao unawapa thamani kubwa ya utajiri, lakini inawanyima ukwasi. Hili lipo dhahiri kwa watu wengi wanaomiliki ardhi na nyumba, thamani ya uwekezaji wao huwa ni kubwa, lakini fedha wanakuwa hawana.

Huwa ni jambo la kawaida sana kukuta mtu anamiliki nyumba zenye thamani kubwa ya fedha, lakini akipata shida inayomtaka hata kuwa na fedha ambayo ni asilimia 10 tu ya utajiri wake mzima anakuwa hana. Na hata akitaka kuuza mali hizo, huwa inachukua muda kupata mteja na hata akipata kwa haraka, atauza kwa hasara.

Ili kuepuka hayo, sisi wawekezaji wa NGUVU YA BUKU tunapaswa kupangilia vizuri utajiri na ukwasi wetu. Kanuni ambayo sisi tunaifanyia kazi ni angalau nusu ya thamani ya utajiri wako iwe kwenye ukwasi, yaani kwenye uwekezaji ambao ni rahisi kuugeuza kuwa fedha. Na huo ni uwekezaji kwenye masoko ya mitaji, hisa, vipande, hatifungani na mingine ambayo tumekuwa tunajifunza.

Unaweza kuwekeza vyovyote utakavyo na kwenye maeneo yote unayotaka, lakini hakikisha nusu inakuwa kwenye masoko hayo yenye kukupa ukwasi kwa urahisi. Ukifuata kanuni hii, hutakuja kunyanyasika kifedha wakati una utajiri. Hata pale unapokabiliana na changamoto mbalimbali, utaweza kuzitatua bila kuingia hasara kwa sababu ya ukwasi unaokuwa nao.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo ili kushirikisha yale uliyojifunza na kuelewa kwa kujibu maswali haya;

1. Eleza tofauti ya thamani ya utajiri na ukwasi. Kwa nini kuna watu wanaweza kuwa na utajiri lakini bado wakakosa fedha?

2. Eleza tofauti kubwa tatu za mfuko wa UKWASI wa UTT na mifuko mingine. Sifa ambazo zipo kwenye mfuko huo tu na hazipo kwenye mifuko mingine.

3. Eleza jinsi unavyokwenda kupangilia uwekezaji wako ili kuwa na thamani ya utajiri na ukwasi pia, kuepuka kunyanyasika kifedha.

4. Kokotoa thamani ya utajiri wako (jumla ya vyote unavyomiliki kutoa madeni uliyonayo), kisha chukua ukwasi ulionao na gawanya kwa thamani hiyo ya utajiri na zidisha kwa 100. Toa jibu lako kwa asilimia na eleza unaenda kufanya nini ili iwe angalau 50%. Jinsi ya kufanya zoezi hili, kwa mfano una nyumba yenye thamani ya milioni 30, madeni milioni 10, benki na cash milioni 1, UTT milioni 4, ukokotoaji wako unaenda hivi; thamani ya utajiri; 30 + 1 + 4  – 10 = 25. Thamani ya utajiri wako ni milioni 25. Ukwasi wako ni 1 + 4 = 5, milioni tano. Asilimia ya ukwasi kwa utajiri ni 5/25 x 100 = 20%. Hivyo ni asilimia 20 ya utajiri wako ndiyo ipo kwenye ukwasi.

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya kuwa umejifunza na kwenda kuchukua hatua ili kujenga utajiri mkubwa kupitia uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.