Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.
Kwenye eneo la usakaji, ambapo ndiyo tunatengeneza wateja wapya kwenye biashara, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE.
Tumeshajifunza njia mbalimbali za kuwasaka wateja wa biashara, kuanzia kuomba rufaa, kuwatembelea wateja na hata kuwapigia simu. Lakini kwenye kila njia, siyo wote utakaowapata watakubali kuwa wateja mara moja. Wengi itawachukua muda mpaka waweze kuwa wateja wa biashara yako.

Kinachohitajika kufanyika ili kuhakikisha wateja unaowafikia wanakubali kununua kwenye biashara yako ni kuwa na ufuatiliaji wa kina na wa karibu kwa wote ambao wameshafikiwa. Bila ya kuwa na ufuatiliaji mzuri, biashara haiwezi kuwa na wateja wa kutosha kufanya mauzo makubwa.
Simu ni moja ya zana muhimu sana kwenye mfumo wetu wa mauzo. Simu ndiyo kifaa tunachokitegemea sana kwenye mikakati yetu yote ya mauzo. Na eneo kubwa tunalofanyia kazi kwenye simu ni kuzungumza na wateja.
Kufuatilia wateja wa biashara kwa mazungumzo ya simu ni moja ya majukumu ambayo kila muuzaji anapaswa kufanyia kazi. Hiyo ni kwa sababu kwa sehemu kubwa, wateja wanahitaji kusikia kwako mara kwa mara kabla hawajaamini na kununua. Na kupitia simu ni rahisi kuwafanya wateja wengi zaidi wasikie kutoka kwako.
Ili ufuatiliaji wako wa wateja kwa kutumia simu uwe na tija, unapaswa kuzingatia haya yafuatayo;
1. Ufuatiliaji unapaswa kuwa wa msimamo bila kuacha.
Wauzaji wengi huwa wanafuatilia wateja mara chache na wakiona hawana mwelekeo wa kununua wanaachana nao. Kumbe wateja nao wanakuwa wanaangalia muuzaji atakuwa na ufuatiliaji kiasi gani.
Ukishawaweka wateja kwenye ufuatiliaji wako, hupaswi kuacha kuwafuatilia. Hivyo weka ratiba nzuri ya kuhakikisha unawafikia wateja wote ulionao kwenye orodha yako angalau mara moja kila wiki.
Kwa sasa kelele zinazowasonga wateja ni nyingi sana, kama huna ufuatiliaji wa karibu na wa msimamo, unasahaulika haraka na kukosa mauzo. Na hii ni kwa wateja wote, ambao bado hawajanunua na hata kwa wale ambao tayari wameshanunua. Ukikaa mbali na wateja wako, yaani usipowafikia, unawapoteza.
2. Ufuatiliaji haupaswi kuwa wa kumchosha mteja.
Kama kila unapompigia mteja simu unamtaka anunue, utawachosha wateja na watakuwa wanakwepa simu zako, kwa kutokupokea au kukata. Hivyo unapaswa kupangilia ufuatiliaji wako ili usiwe wa kumchosha mteja na mambo yale yale kila siku.
Kuna vitu vya tofauti unavyoweza kufanya kwenye ufuatiliaji na vikawafanya wateja kuwa tayari kukupa ushirikiano. Inaanza na kuwapa wateja zawadi mbalimbali, kwa nyakati unazowafikia, tenga ambazo unakuwa umewaandalia zawadi ambazo zinawanufaisha. Pia kuwapa salamu mbalimbali za kujua maendeleo yao au pongezi kwa hatua mbalimbali wanazopiga ni kitu ambacho hakiwachoshi wateja.
Kuwa mbunifu kwenye kuwafuatilia wateja wako, kiasi cha wateja kuwa na shauku kila wanapoiona simu yako, kwa sababu wanajua kuna kitu kizuri watakipata.
SOMA; Usakaji Wa Wateja Kwa Kupiga Simu.
3. Pata sababu ya kumtafuta tena mteja kwenye kila ufuatiliaji.
Kwa kila mazungumzo ya simu unayofanya na mteja, hakikisha unapata sababu ya kumtafuta tena wakati mwingine. Hivyo endesha mazungumzo yako kwa namna ambayo unapata miadi au ahadi ya mazungumzo mengine yajayo ambayo kuna kitu mteja atafanya au wewe utafanya.
Pale mnapokuwa na miadi ya mazungumzo yanayofuata inakuweka kwenye nafasi nzuri ya mteja kupokea simu yako kuliko mkiwa hamna miadi. Hivyo kila unapoongea na mteja, jiulize nini unakwenda kufanya ili kutengeneza mazingira mazuri kwa mazungumzo yajayo.
Maswali unayouliza, taarifa unazowapa na ahadi mbalimbali unazotoa zinapaswa kulenga kuwepo kwa mazungumzo mengine baada ya hapo. Kwa mfano kama umempa mteja zawadi, tayari una fursa ya kumfuatilia kujua kama zawadi imemfaa. Au kama mteja ataahidi kufanya manunuzi wakati fulani ujao, tayari una ahadi ya kufuatilia. Tengeneza hali kama hizo nyingi ili uwe na ufuatiliaji wa uhakika kwa wateja wako.
4. Toa thamani zaidi kwenye kila ufuatiliaji.
Kwa kila mazungumzo ambayo unafanya na wateja wako, hakikisha unawaacha wakiwa bora zaidi ya walivyokuwa kabla ya kuzungumza na wewe. Hivyo toa thamani zaidi kwa wateja wako kwa kila mazungumzo unayofanya nao. Utaweza kufanikisha hilo kama utakuwa unawajua wateja wako kwa kina na kila mara kutafuta fursa za kuwanufaisha zaidi.
Pale unapokutana na taarifa ambazo zina manufaa kwao, unaweza kuwashirikisha unapozungumza nao ili wanufaike nazo. Au pale kunapokuwa na habari njema kuhusu biashara yako, labda mabadiliko ya bei au upatikanaji wa mali, unawaonyesha kwamba umewapa wao kipaumbele kwenye taarifa ili wanufaike zaidi.
Kwa kuijua biashara yako vizuri na kuwajua wateja wako kwa kina utaona fursa nyingi za kuwapa thamani kubwa zaidi kwenye kila ufuatiliaji ambao unaufanya.
5. Kusanya taarifa zaidi kwenye kila ufuatiliaji.
Kila unapowasiliana na wateja, usifanye tu ili kusema umekamilisha hilo zoezi, badala yake fanya kimkakati. Hakikisha kwa kila nafasi unayopata ya kuzungumza na wateja kwa simu, kuna taarifa zaidi unazokuwa umejua kuwahusu wao, ambazo zinakupa fursa ya kuendelea kuwafuatilia zaidi.
Utaweza kupata taarifa hizo kwa kuuliza maswali na kusikiliza kwa kina. Watu wanapoulizwa maswali huwa wanajibu na wanaposikilizwa huwa wanajieleza. Fanya hayo mawili kila unapozungumza na wateja wako na fursa za kupata taarifa nyingi kuhusu wao zitafunguka.
Hapo pia utapata sababu nyingine ya kuwafuatilia zaidi. Kwa mfano kama kupitia mazungumzo unayofanya na mteja umejua timu anayoshabikia, pale timu hiyo inapopata ushindi, unakuwa na sababu ya kuwapigia simu na kuwapongeza kwa ushindi huo. Au kama utakuwa umejua tarehe yao ya kuzaliwa, unakuwa na sababu ya kuwapigia kwenye tarehe zao na kuwatakia heri ya kumbukizi ya kuzaliwa.
Tumia vizuri simu kwenye kuwafuatilia wateja kwa kuongea nao ili kuzoeleka, kuaminika na kuwashawishi wawe tayari kununua kwako. Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kutengeneza wateja wengi zaidi na kukuza zaidi mauzo kwenye biashara yako.
Kamwe usikate tamaa na kuacha kuwafuatilia wateja, hata kama umekutana na ugumu kiasi gani. Wewe ichukulie hiyo kuwa ni kazi yako kama muuzaji na ifanye kwa msimamo bila kuacha, utapata matokeo mazuri.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.