Rafiki yangu mpendwa,

Maisha huwa yanakuwa na changamoto na vikwazo vya kila aina. Na hilo limekuwa ni kwa mwendelezo kwa kipindi chote cha maisha ya mtu. Wengi hudhani changamoto na matatizo ni kabla hawajafanikiwa na wakishafanikiwa basi vitaondoka. Wanachokuja kushangaa na hata baada ya kufanikiwa, changamoto na matatizo vimekuwa havikosekani.

Kila mtu kwenye maisha huwa anapitia matatizo na changamoto mbalimbali. Lakini matokeo ya mwisho kwenye maisha baina ya watu hao huwa yanatofautiana. Wapo ambao wanajenga mafanikio makubwa licha ya magumu wanayopitia. Na wapo ambao wanakatishwa tamaa na magumu wanayopitia kitu kinachowazuia kufanikiwa.

Sehemu kubwa ya watu wamekuwa wanakwamishwa na magumu na changamoto wanazokuwa wanapitia. Hiyo inatokana na wao kujiona hawana uwezo wa kuyakabili hayo. Maisha yao yanakosa maana na wanaona hawana haja ya kusumbuka wakati matatizo hayataisha. Hawa wanakuwa wamekubali kushindwa kwenye maisha. Wengi huishia hata kuwa na maisha mafupi kwa sababu hata miili yao inakosa uimara wa kupambana na magonjwa mbalimbali.

Sehemu ndogo ya watu huwa wanatumia matatizo na changamoto wanazokutana nazo kupambana ili kufanikiwa. Magumu wanayokutana nayo wanayatumia kama sababu kwa nini hawakubali kubaki pale walipo. Wanapambana kwa kila namna bila kukata tamaa, mpaka wanapata mafanikio ambayo ni makubwa.

Ili na wewe uweze kuyatumia mateso unayopitia kujenga mafanikio makubwa, kuna mambo matatu ambayo unapaswa kuyafanya.

Jambo la kwanza ni kujitambua wewe mwenyewe, kupitia kujisikiliza na kufanya yale ambayo ni sahihi kwako. Kitu ambacho kinawakwamisha watu wengi ni kufuata mkumbo na kuiga yale ambayo yanafanywa na watu wengine. Watu wengi wamekuwa hawajiamini kuendea kile ambacho kipo ndani yao hasa. Wanaona kile kinachofanywa na wengine ndiyo sahihi zaidi kuliko wanachotaka kufanya wao. Mwishowe wanashindwa vibaya kwa sababu kile wanachokazana kufanya hakiendani na uimara ulio ndani yao.

Wewe usiwe kama watu hao, jisikilize wewe mwenyewe, maana ndani yako kuna sauti inayokuambia unapaswa kuwa mtu wa aina gani na unapaswa kufanya nini. Tayari unajua nini sahihi kwako kufanya, hata kama hakuna wengine wanaofanya. Wajibu wako ni kufanya hicho, maana ndiyo chenye mafanikio makubwa kwako.

Jambo la pili ni kutumia magumu unayokutana nayo kama sababu ya kuendelea kufanya na siyo kikwazo cha kuacha. Chochote kinachokukwamisha, kigeuze hicho kuwa ndiyo njia ya wewe kupata kile unachotaka. Kamwe usiingiwe na mawazo ya kukata tamaa au kuacha. Mara zote kaa kwenye mapambano bila ya kuacha. Mambo yanavyozidi kuwa magumu na wewe ndiyo unazidi kuwa mgumu na kupambana zaidi.

Hapa pia kuwa na sababu kubwa ya kwa nini upitie mateso hayo na kuendelea nayo bila kukata tamaa. Kuwa na sababu za nje yako ambazo zinakufanya uendelee. Ukiwa unajiangalia tu mwenyewe ni rahisi kukata tamaa na kuacha. Lakini kwa kuwa na sababu kubwa za nje utapata msukumo wa kuendelea.

Jambo la tatu ni kuwa na mfumo utakaokuwajibisha ili usitoroke au kuacha kile unachofanya. Ikiwa ni wewe mwenyewe unayeamua ufanye au usifanye, ni rahisi sana kujidanganya na kuacha kufanya. Lakini kunapokuwa na mfumo wa kukuwajibisha iwapo utaacha, pale unapolazimika kueleza kwa wengine kwa nini hujafanya, unapata msukumo wa kuendelea kufanya licha ya kupitia magumu.

Mfumo wa kuwajibika unaanza na jamii inayokuwa inakuzunguka. Unapaswa kuzungukwa na watu ambao wanakusukuma uwe bora zaidi na ufanye makubwa zaidi. Pia mfumo wa kuwajibika unakutaka uwe na Kocha anayekusimamia kwa karibu kwenye yale unayofanya, ambaye hatakubaliana na wewe kirahisi pale unapotaka kuacha kufanya.

Kwa kuzingatia haya matatu uliyojifunza hapa, utaweza kuendelea na safari yako ya kujenga mafanikio makubwa licha ya mateso utakayokuwa unayapitia.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kutumia mateso ili kufanya makubwa kwenye maisha yako. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na uchukue hatua ili kuweza kufanya makubwa licha ya magumu utakayokuwa unayapitia kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.