Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Ukamilishaji wa mauzo ni pale mteja anapokubali kutoa fedha na kupata bidhaa au huduma unayouza.

Kama mteja hajafanya maamuzi hayo, mauzo hayajakamilika, hata kama ameahidi kwa msisitizo kiasi gani. Ni mpaka mteja aseme nimekubali kununua na kutoa fedha au mpango wa malipo ndiyo mauzo yamekamilika.

Hivyo hatua ya ukamilishaji ni muhimu sana kwenye mchakato wa mauzo, kwani ndiyo inayoleta mafanikio au kushindwa kwenye mauzo.

Kwa sababu ushindi kwenye mauzo unapimwa kwa wale waliokubali pekee na siyo kwa ahadi.

Biashara zinashindwa kwa sababu hazipati mapato ya kutosha kutokana na kutokukamilisha mauzo. Watu huweza kutoa sababu mbalimbali kwa nini biashara zinashindwa, lakini ya kwanza kabisa ni hiyo ya kushindwa kukamilisha mauzo na hata mipango mingine inayokuwepo.

Kwa kulitambua hilo rafiki yangu nikupendaye, nimekuandalia mbinu mbili za uhakika za kukamilisha mauzo. Na leo tunakwenda  kujifunza mbinu namba 17 na 18.

17. Ukamilishaji wa kukubaliana – 3.
Unakutana na mteja anakupa pingamizi pale unapotaka kumkamilisha, labda anakuambia bei ni ghali, hali ngumu, nitakutafuta nikiwa tayari na sababu nyingine nyingi. Wewe hupaswi kumbishia mteja, bali mwambie; 

“Nakubaliana na wewe na kila ambaye amewahi kununua hii bidhaa au huduma huwa anasema hivyo. Nahitaji sahihi yako hapa, nahitaji tukamilishe hili, lipia uchukue bidhaa yako uende ukaifurahie.

Hapa unatumia wengine kukukubaliana naye na kukamilisha mauzo. Kwa pingamizi lolote atakalokupa utamwambia nakubaliana na wewe na wote wanaonunua hii bidhaa au huduma huwa wanasema hivyo. Hapa unakuwa unatumia nguvu ya silaha ya kufuata mkumbo. Mtu akishaona kama wengi wanasema kama yeye na kisha wakakubali kununua na yeye atashawishika kununua.

Mapingamizi mengi ambayo watu wanayatoa ni malalamiko tu na siyo mapingamizi ya kweli, hupaswi kuyapa uzito zaidi ya kukubaliana nao kisha kuendelea na ukamilishaji wa mauzo.

18. Ukamilishaji wa haitakuwa mara ya mwisho.

Unakutana na mteja anasema kwamba ni fedha nyingi kweli na kutumia kama sababu ya kutokukamilisha mauzo wewe mwambie,

“Nakubaliana na wewe, na hii haitakuwa mara ya kwanza wala ya mwisho kwako kutumia fedha nyingi kuliko ulivyokuwa unategemea. Nahitaji uweke sahihi hapa, nahitaji tukamilishe hili, lipia uchukue bidhaa yako uende ukaifurahie.”

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea, kila mtu huwa ananunua vitu kwa bei kubwa kuliko alivyotegemea.

Kitu kimoja zaidi, tabasamu wakati unamwambia mteja hilo kisha kamilisha mauzo.

Hizi mbinu zinafanya kazi kama ukizifanyia kazi. Usiogope kuzitumia kama unataka kupata matokeo mazuri.
Mara zote unapaswa kukamilisha mauzo na tumia mbinu hizi pale unapokutana na changamoto ya kutokukamilisha mauzo.

Hatua ya kuchukua leo; kuwa na njaa ya kuuza, usikubali sababu za mteja anazokuambia, wewe mshawishi anunue kwa kutumia mbinu ambazo umeshajifunza hapa kwenye CHUO CHA MAUZO.

Mwisho, ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Ushindi wa biashara ni kuuza, hivyo hakikisha unauza na siyo kuja na visingizingizio.
Watu hawahitaji maelezo yako mazuri. Watu wanahitaji matokeo mazuri.
Uza na maelezo hayahitajiki iwe umepata au hujapata ushindi.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz