Rafiki yangu mpendwa,
Licha ya wingi wa upatikanaji wa taarifa na maarifa kwenye zama hizi, bado watu wengi wamekuwa wanashindwa kupata mafanikio makubwa ambayo wangependa kuyapata.
Wingi na urahisi wa kupatikana kwa taarifa na maarifa kwenye zama hizi, ni zaidi ya kipindi chote cha uwepo wa binadamu hapa duniani. Miaka 50 tu iliyopita raisi wa taifa lenye nguvu kubwa duniani hakuwa na maarifa na taarifa nyingi kama alizonazo mtu wa kawaida kwa sasa.

Kwenye hayo maarifa na taarifa nyingi zinazopatikana kirahisi, mafunzo na ushauri umekuwa ni mwingi pia. Mambo mengi yamekuwa yanafundishwa na kushauriwa kuhusu mafanikio kwenye kila eneo la maisha. Lakini bado wengi wamekuwa hawanufaiki na ushauri wanaokuwa wanaupata.
Eneo ambalo ushauri umekuwa hauwanufaishi wengi, na hata wakati mwingine kuwa kikwazo kwao ni kwenye biashara. Kwa ushauri mwingi wa kibiashara ambao umekuwa unatolewa, tena mara nyingi bure kabisa, kila anayefanya biashara angepaswa kuwa na mafanikio makubwa.
Lakini hivyo sivyo ilivyo kwenye uhalisia, biashara zenye mafanikio ni chache sana. Wengi wanashindwa kupata ushauri bora na unaowawezesha kujenga biashara zenye mafanikio makubwa.
Wewe rafiki yangu unakwenda kuvunja hilo leo, baada ya kujifunza hapa utakwenda kujenga biashara yenye mafanikio makubwa kupitia kupata na kutumia vizuri ushauri unaopewa.
Kitu cha kwanza muhimu sana na ambacho wengi huwa wanakikosea wakati wa kuomba au kuchukua ushauri ni wanakuwa hawajui nini hasa wanachotaka. Hivyo wanapoomba ushauri, wanawataka watu wengine wawaambie ni nini wafanye. Hapo ndipo maswali kama biashara gani nifanye yanapokuwa mengi.
Niwe tu mkweli kwako rafiki yangu, kama unauliza ni biashara gani ufanye, tayari umeshashindwa kabla hata hujaanza. Unapaswa kuwa tayari unajua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako na ili kukipata unapaswa kufanya kazi au biashara gani. Utaweza kujua hilo kwa kusikiliza sauti iliyo ndani yako, ambayo huwa haichoki kukuambia vile unavyopaswa kuwa.
Hivyo basi, ili kunufaika na ushauri wowote unaopewa, kwanza jua nini hasa unachotaka na nini cha kufanya ili kupata unachotaka.
Baada ya kujua unachotaka, hatua nyingine muhimu ni kuomba ushauri mahususi badala ya ushauri wa jumla. Ushauri mwingi ambao watu wanaomba au kupokea huwa ni wa jumla, ambao hauelezi kwa uhakika nini hasa mtu anapaswa kufanya ili kupata anachotaka. Ushauri wa jumla unaonekana kumlenga kila mtu, ila hauwi na msaada kwa yeyote. Ushauri wa jumla ni kama kuambiwa biashara fulani inalipa sana. Hakuna chochote cha maana unachokuwa umeambiwa kwenye maelezo kama hayo.
Ushauri mahususi ni ule unaolenga kitu fulani na kutoa hatua za mtu kuchukua ili kupata matokeo bora na ya tofauti. Ushauri huo unakuwa unaendana na mtu kwenye kile anachofanya na hali anayokuwa anapitia. Ushauri mahususi ni unamlenga mtu mmoja na hauwezi kuwa na manufaa kwa wengine wengi, kwa sababu wanayofanya na kupitia ni tofauti kabisa.
Ili uweze kupata ushauri mahususi ni lazima ujue kile unachotaka, kisha umweleze anayekushauri ni wapi hasa umekwama. Baada ya kukuuliza maswali na kukusikiliza kwa kina, ndipo sasa ataona maeneo gani unayokwama na kukushauri hatua za kukuwezesha kutoka kwenye hayo maeneo uliyokwama. Ni kwa njia hiyo ndiyo ushauri unakuwa na manufaa makubwa kwako.
Haya ni mambo mawili ya msingi kati ya matano ya kuzingatia ili uweze kupata ushauri mzuri na wenye manufaa kwako. Mambo mengine matatu nimeyaelezea kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Sikiliza kipindi hicho kujifunza ili uweze kunufaika na ushauri sahihi na upige hatua kubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.