Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kitabu cha HOW I RAISED MYSELF FROM FAILURE TO SUCCESS IN SELLING, mwandishi anashirikisha hadithi yake kwenye mauzo. Alikuwa muuzaji wa bima ya maisha kwenye moja ya makampuni ya bima, lakini hakuwa anafanya vizuri. Mauzo yake yalikuwa madogo sana kiasi cha kushindwa kupata kipato cha kuendesha maisha yake.
Hali hiyo ilimfanya afikie maamuzi ya kuachana na kazi hiyo ya mauzo na akapanga kwenda kufanya vibarua ambavyo vitampatia kipato cha kuendesha maisha yake. Alikuwa ameacha vitu vyake ofisini na hivyo akaamua kwenda kuchukua vitu vyake na kuacha kazi rasmi.

Alipofika ofisini, alikuta kikao cha wauzaji kinaendelea na bosi wao. Hakutaka kuleta usumbufu, hivyo akaamua asubiri wamalize kikao ndiyo aingie na kuchukua vitu vyake. Pale alipokuwa anasubiria alikuwa anasikia kila kinachoendelea kwenye kikao hicho.
Aliwasikia wauzaji wakitaja namba zao za mauzo na akawa haamini kama ni kweli. Kwani kila muuzaji alikuwa anaripoti mauzo mazuri aliyofanya. Mwisho a mkutano bosi wao akawa anaongea, kuwapa neno la hamasa. Bosi huyo alisema kauli ambayo ilimgusa sana mwandishi. Alisema; ‘Nionyeshe muuzaji yeyote, ambaye ataeleza hadithi yake ya mauzo kwa watu wanne mpaka watano kila siku na nitakuonyesha muuzaji mwenye mafanikio makubwa.’
Kauli hiyo ilimfanya mwandishi Frank Bettger kutafakari kwa kina, kwamba kumbe mauzo yanaweza kuwa rahisi hivyo? Kumbe hahitaji kufanya makubwa sana, kazi yake ni kueleza hadithi yake kwa watu wanne mpaka watano kwa siku. Alijiambia mdomo ninao wa kueleza hadithi hiyo na miguu miwili ninayo ya kuwatembelea watu. Hapo alikata shauri kwamba ataendelea na kazi hiyo ya mauzo na atafanyia kazi kanuni hiyo tu.
Frank alifanyia kazi mpango huo na ndani ya miezi 10 akawa amefanya mauzo makubwa kuliko kipindi cha miaka mitatu ambayo alikuwa amefanya kazi hiyo ya mauzo. Nini kilibadilika kwake? Ni kuwa na mfumo rahisi wa mauzo kwake, wa kuwafikia watu na kuwaeleza watu hadithi yake ya mauzo.
Rafiki, hiki ndiyo ninakushauri na wewe ufanye. Kama unataka kukuza mauzo unayoyafanya, usihangaike sana na mambo mengi, wewe chukua hatua ya kuandaa hadithi yako nzuri ya mauzo (uwasilishaji mzuri wa kile unachouza) kisha kuhakikisha unatoa hadithi hiyo kwa watu wengi zaidi kila siku. Kwa zama za sasa zenye kila aina ya usumbufu na ushindani mkali, watu wanne mpaka watano hawatatosha. Kiwango cha chini kabisa ni angalau watu 10. Lakini kama unataka mauzo makubwa, unapaswa kueleza hadithi yako kwa namba kubwa zaidi ya watu kila siku, kuanzia 100 na kuendelea.
Uzuri ni kwamba kwenye zama hizi kuna teknolojia nyingi zinazoweza kurahisisha wewe kufikisha hadithi yako ya mauzo kwa watu wengi. Unaweza kuandika maudhui mazuri yanayoelimisha na kusambaza kwa wengi. Unaweza pia kutoa maudhui kwa njia nyingine kama picha, sauti na video.
Na pia unahitaji kufanya zoezi la kuwafikia watu moja kwa moja, kupitia kuwatembelea na kukutana nao, na hapa ndipo kanuni ya watu 4 mpaka 5 kwa siku inapofanya kazi. Kwa muuzaji yeyote yule, akiweza kuwafikia watu wanne mpaka watano kila siku na kuwaeleza hadithi yake ya mauzo, ataweza kufanya mauzo makubwa sana.
Njia nyingine ya kuwafikia wateja na kuwapa hadithi ni kuwapigia simu na kuongea nao. Kwa njia hii unaweza kuwafikia wengi zaidi na kuwashawishi kununua. Mawasiliano ya jumbe na mitandao ya kijamii pia ni njia ya kuwafikia wengi.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua zaidi dhana hii ya kueleza hadithi yako ya mauzo kwa watu wengi zaidi ili kukuza mauzo. Karibu uangalie kipindi hapo chini na ufanyie kazi yale unayojifunza ili kuwa na ushawishi na kufanya mauzo makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.