3342; Usiipoteze bahati.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Japokuwa bahati siyo mkakati sahihi wa mafanikio, huwa tunakutana nayo kwenye hii safari.
Inakuwa ni bahati pale unapokutana na fursa ambayo hukuwa unaitegemea na hivyo hukuwa na maandalizi sahihi nayo.
Kwa kukosa misingi sahihi, huwa ni rahisi kw kitu kuanguka.
Hivyo kitu ambacho mtu anapaswa kufanya mara moja ni kujenga misingi sahihi kwenye kila eneo lake.
Pale mtu anapopata fursa kwenye kitu ambacho hakuwa amekijengea misingi sahihi, kitu cha kwanza anachopaswa kufanya ni kujenga misingi sahihi ili asipoteze fursa hiyo.
Lakini hivyo sivyo wengi wanavyofanya.
Wengi wanapokutana na fursa ambayo hawakuwa na maandalizi nayo, wanajisahau haraka na kuanza kujiona kama ni kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wao.
Badala ya kujenga misingi sahihi itakayofanya kitu kuwa imara zaidi, wanakimbilia kutumia na kufurahia kitu.
Matokeo yake ni kuishia kupoteza ile fursa waliyopata kwa sababu hawakuwa na misingi sahihi.
Mtu mwenye hekima amewahi kusema, ukijikuta umejenga ghorofa angani, kinachopaswa kufuata ni kujenga msingi ili ghorofa hilo liwe imara na usipoteze kazi yako.
Lakini wengi wamekuwa hawafanyi hivyo, wakijikuta wamejenga ghorofa angani, wanaanza kuonyesha ni jinsi gani wana miujiza na uwezo mkubwa wa kuweka ghorofa angani.
Matokeo yake yanakuwa ni anguko la ghorofa hilo na wanapoteza kila kitu.
Chukua mfano wa mtu anayepata fedha nyingi na kwa haraka, ambazo hajazifanyia kazi na kuumia.
Hatua ambayo mtu angepaswa kuchukua ni kutuliza kwanza fedha hizo na kujenga kwanza misingi sahihi ya kuziendeleza fedha hizo kabla hajaanza matumizi. Kufanya hivyo kungesaidia fedha hizo kuwa na manufaa kwa mtu.
Lakini hivyo sivyo inavyokuwa kwenye uhalisia, wengi wanapopata fedha nyingi na kwa haraka, huwa wanaongeza zaidi matumizi na haiwachukui muda wanakuwa wamepoteza fedha zote kwa haraka kama zilivyokuja.
Hakikisha una misingi sahihi kwenye kila kitu unachojihusisha nacho.
Pale unapojikuta umepata fursa ambayo hukuwa na misingi yake sahihi, usijisahau na kudhani umekuwa na uwezo wa kimiujiza.
Badala yake anza kujenga misingi haraka sana ili kuimarisha kile ulichopata.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mara zote tunahangaikia misingi sahihi, ili kuhakikisha ipo imara na inaweza kukabiliana na chochote kinachoweza kuja.
Tunajua changamoto kubwa zaidi ipo kwenye kutunza kile ambacho tumeshapata kuliko hata kukipata.
Kwenye jamii hii tunawajibishana ili kuhakikisha tunajenga na kukaa misingi sahihi ambayo itadumisha kile tulichojenga.
Unapochagua kuwa kwenye jamii hii, maana yake unakuwa umechagua kuwa mtu wa kusimamia misingi muda wote.
Wajibu wako mara zote ni kupima uimara wa misingi yako katika kuvuka changamoto na magumu ambayo yanaweza kutokea.
Pale madhaifu yanapoonekana, hatua zinachukuliwa mara moja.
Hangaika na misingi sahihi na mengine yote yatakaa sawa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe