3343; Rasilimali haba zaidi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Zipo rasilimali muhimu tunazozihitaji sana kwenye safari yetu ya mafanikio.
Zipo rasilimali ambazo zinapatikana kwa utele na hazina shida.
Halafu kuna rasilimali ambazo huwa zinapatikana kwa uhaba.

Huwa imezoeleka rasilimali kama fedha na muda kuwa na uhaba. Hiyo ni kwa sababu huwa zinahitajika zaidi na zaidi kadiri ukuaji unavyoendelea kuwepo.

Ipo rasilimali yenye uhaba mkubwa zaidi, ambayo kwa haraka huwa haionekani hivyo.
Rasilimali hiyo ni watu.
Kabla hujaanza kuhitaji watu, utaona wapo wengi na rahisi kupatikana.
Ni mpaka pale unapokuwa unawahitaji watu na kuanza kuwatafuta ndiyo unakutana na huo ukweli kwamba kuna uhaba mkubwa wa watu.

Watu wanaweza kuonekana wakiwa wengi na wakitaka nafasi mbalimbali. Lakini wengi huishia kuwa ni watu wasiofaa kwenye hizo nafasi wanazokuwa wanataka.

Tuchukue mfano wa kuajiri.
Kabla hujaanza kuajiri, utaona wenye uhitaji wa kazi ni wengi na hivyo kuona zoezi litakuwa rahisi.
Ni pale unapoanza kuajiri ndiyo unagundua wengi hawana ule msukumo ambao unataka wawe nao.
Utakutana na wengi, ambao watakupa maneno mazuri na utakuwa na  matumaini makubwa.
Lakini inapokuja kwenye utendaji, ndipo unapogundua kwamba kusema na kufanya ni vitu wiwili tofauti.

Njia ya kukabiliana na uhaba wa rasilimali hii ambayo ndiyo muhimu zaidi ni kuanza kuangalia watu kwa tabia zao, kisha kuwapa mafunzo ya kuwajenga kwenye majukumu yao na maendeleo binafsi.

Kuwapata tu watu haitoshi, unapaswa kuendelea kuwajengea uwezo utakaowafanya kuendelea kuwa bora kwenye majukumu yao.

Watu sahihi ni adimu kupatikana, unapowapata, hakikisha huwapotezi kirahisi.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, rasilimali watu ni eneo ambalo tunalipa uzito mkubwa.
Tunajua malengo makubwa tunayoyapambania hatutayaweza sisi peke yetu.
Tunajitaji timu sahihi ili kupambana na kufikia malengo hayo.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA hatuamini kwenye jeshi la mtu mmoja kujenga mafanikio makubwa.
Tunajenga timu bora na kuendelea kuijengea uwezo ili iweze kukabiliana na kila kitu mpaka kuyafikia malengo makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe