Rafiki yangu mpendwa,
Bilionea Warren Buffett huwa ana nukuu yake ambayo naipenda sana na nimekuwa naitumia mara kwa mara. Nukuu hiyo inasema; ‘Kama huwezi kuingiza fedha ukiwa umelala, utafanya kazi maisha yako yote.’
Rafiki, ukiielewa hiyo nukuu na ukaifanyia kazi, utaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako na kuwa huru kwa namna unavyotaka wewe mwenyewe.
Msingi mkuu wa kauli hiyo ni mtu uweze kuingiza fedha hata kama umelala, yaani uweze kuingiza fedha bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.
Je unajua ni kwa namna gani unaweza kufanya hivyo? Kuna njia mbili tu, moja ni kumiliki biashara ambayo inaweza kujiendesha bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja. Na mbili ni kufanya uwekezaji.
Hapa tutaangalia kuhusu uwekezaji, ambacho ndiyo kitu napiga kelele kila mtu akifanye, aanze mara moja na kufanya kwa msimamo kwa maisha yake yote.

Uwekezaji ni pale unapoifanya fedha ikufanyie kazi wewe. Kwenye maisha, kila mmoja wetu huwa anaanza kwa kufanya shughuli fulani ndiyo aweze kuingiza kipato. Lakini kadiri muda unavyokwenda, mtu unapaswa kuifanye fedha unayoingiza ikufanyie kazi na kukuingizia kipato.
Utajiri ambao unakupa uhuru kamili wa maisha yako ni pale ambapo fedha zako zinafanya kazi na kukuingizia kipato cha kutosha kuendesha maisha yako. Kwa maneno mengine ni maisha yako yanakuwa yanaweza kwenda vizuri hata kama wewe hufanyi kazi moja kwa moja.
Fursa za uwekezaji ni nyingi na zote zina manufaa kwa wale wanaowekeza. Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa hawana uelewa ni uwekezaji gani wafanye.
Halafu kuna ambao wanaona kipato walichonacho hakitoshi kuwekeza, wanasubiri mpaka kipato chao kiongezeke ndiyo waanze kuwekeza. Kwa bahati mbaya zaidi, hata pale kipato kinapoongezeka, matumizi nayo yanaongezeka hivyo wanakuwa wamebaki pale pale, kipato hakitoshelezi.
Kwako wewe rafiki yangu mpendwa, ambaye umekuwa unafuatilia kazi ninazofanya, ninachotaka ni wewe uwe unawekeza, kwa kuanzia popote ulipo sasa.
Hiyo ni kwa sababu kuna fursa nzuri za uwekezaji ambazo mtu yeyote anaweza kunufaika nazo bila ya kujali uelewa wake wala kipato chake. Yaani kuna uwekezaji ambao wewe unaweza kuanza kufanya hata kama hujui chochote kuhusu uwekezaji. Na vizuri zaidi ni unaweza kuanza na kiasi kidogo sana cha fedha kufanya uwekezaji wako, kiasi ambacho tayari unacho, hata kama unajiona umefulia kiasi gani.
Rafiki, nataka sana wewe unafanya huu uwekezaji kwa sababu ni fursa ya wazi kabisa ambayo wengi wananufaika nayo. Sitaki fursa hii ikupite wakati upo kwenye nafasi nzuri ya kunufaika nayo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina aina hiyo ya uwekezaji ambayo unapaswa kuanza nayo ili uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Karibu ujifunze kwenye kipindi hiki na uchukue hatua ili usije ukalazimika kufanya kazi mpaka unakufa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.