Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu tunazaliwa, tunakua na tunakufa. Hivyo ndivyo maisha yetu yanavyokwenda hapa duniani. Kati ya kuzaliwa na kufa, huwa tunapitia mambo mengi sana hapo katikati.
Jinsi ambavyo mtu atakuwa na mafanikio ambayo atayapata kwenye maisha yake, itategemea sana jinsi anavyokabiliana na mabadiliko ya maisha. Wapo ambao wanaona kama mabadiliko ya maisha ndiyo yamewakwamisha wasifanikiwe. Lakini unakuta wengine kwenye mabadiliko hayo hayo wameweza kufanikiwa.
Hivyo kitu cha kwanza ambacho mtu anapaswa kujua namna ya kukifanya vyema kwenye maisha yake ni kukabiliana na mabadiliko. Kuhakikisha mabadiliko yoyote yanayokuja kwake, anaweza kuyatumia kwa manufaa zaidi.

Aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha nne cha Meditations ametupa mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kukabiliana vyema na mabadiliko ya maisha.
Kitu cha kwanza ni kujua kwamba mabadiliko yatatokea, iwe unataka au hutaki. Marcus ameshirikisha mifano ya mambo mengi ambayo yamewahi kuja na kupita, watu waliofanya makubwa na hawapo tena na jinsi kila kizazi kinakuwa na mambo yake. Sehemu kubwa ya maandalizi ya kukabiliana na mabadiliko ni kujua kwamba yanakuja. Kwa njia hiyo hutashangazwa pale mabadiliko yanapotokea.
Watu wengi huwa wanashangazwa pale mabadiliko yanapotokea, kwa kuona ni kitu ambacho hawakutegemea. Huwa tunaona mambo yakitokea kwenye maisha ya wengine, kwa nini tunadhani kwetu hayawezi kutokea mambo hayo? Kuwa Mstoa kwa kujua kwamba kile unachoona kinatokea kwa wengine, na kwako pia kitatokea. Hivyo kuwa na maandalizi sahihi ya kukabiliana nayo yatakapotokea.
Kitu cha pili ni kutumia kila mabadiliko yanayotokea kwa manufaa zaidi. Hapa ni kuhakikisha unanufaika zaidi na mabadiliko yanayotokea. Marcus anatumia mfano wa moto, anasema moto ukiwa mkali, chochote kinachowekwa kwenye moto huo kinakuwa nishati ya kuuchochea zaidi. Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyafanya maisha yako, yawe ya moto sana kiasi kwamba kila kinachokuja kwako, kinakuwa kichocheo cha kufanya makubwa zaidi.
Kila mabadiliko yanayotokea, jiulize unawezaje kuyatumia kwa manufaa zaidi. Usikae ukiumia na mabadiliko na kutamani mambo yangerudi kama zamani. Mambo hayatarudi kama zamani, hivyo ni bora kuanza kuyatumia mabadiliko hayo kwa manufaa haraka. Ukiwa mtu wa kutafuta fursa kwenye kila mabadiliko, utaziona fursa nzuri ambazo ukizitumia utaweza kufanya makubwa. Kuwa Mstoa na hakikisha kwenye kila mabadiliko unayopitia, kuna manufaa ambayo umetoka nayo.
Kitu cha tatu ni kuyafurahia mabadiliko yoyote unayokutana nayo. Marcus anasema wengi wanapokutana na mabadiliko huwa wanasema; ‘Kwa nini imetokea kwangu?’ Anasema hiyo siyo sahihi, unachopaswa kusema ni; ‘Bora imetokea kwangu maana naweza kukabiliana nayo vizuri.’ Unapaswa kuyafurahia mabadiliko kutoka kwako kwa sababu unaweza kuyatumia vizuri kuliko watu wengine. Kwa wengine mabadiliko hayo wangeyapoteza tu bure, lakini wewe utayatumia kwa manufaa makubwa zaidi.
Kwa kuyafurahia mabadiliko, unakuwa na mtazamo mzuri na kuweza kuyatumia kwa manufaa. Unayakaribisha kuja kwako na kuhakikisha unanufaika nayo. Chochote ambacho utapenda na kufurahia, utanufaika nacho. Kitendo tu cha mtu kuyachukia mafanikio, inampunguzia msukumo wa yeye kunufaika nayo. Kuwa Mstoa kwa kuyafurahia mabadiliko, yawe ni mazuri au mabaya, yote yanakuja na fursa nzuri kwako.
Hayo ni machache kati ya mengi ambayo Marcus ameshirikisha ya kukabiliana vyema na mabadiliko ambao ni sehemu ya maisha. Mengine nimeyashirikisha kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA kuhusu mada hii. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini, ujifunze na ukanufaike na kila mabadiliko unayopitia.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.