Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.
Unakuwa bora kupitia maendeleo binafsi, kwa kujifunza na kuweka kwenye matendo mafunzo ambayo yanakujengea tabia sahihi za kimafanikio. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza moja ya tabia unazohitaji ili kuwa bora na kufanikiwa kwenye kila eneo la maisha yako, ambayo ni UCHAPAKAZI.

RAFIKI WA KWELI.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, unaweza kuwa na marafiki wengi kwenye maisha yako, lakini hakuna atakayeweza kuwa mwema kwako kama kazi. Kazi ndiye rafiki yako wa kweli, rafiki ambaye hawezi kukusaliti wala kukuonea wivu kwa namna yoyote yule.
Kazi ni rafiki ambaye ukimpenda na yeye atakupenda na kukupa heshima kubwa mbele ya watu wengine. Ni rafiki ambaye atakutoa chini kabisa na kukufikisha kwenye vilele vya mafanikio makubwa.
Marafiki wengine huwa wanataka ufanikiwe, ila siyo ufanikiwe kuwazidi. Lakini rafiki kazi, anataka ufanikiwe zaidi na zaidi na hatakunyima mafanikio kama utampenda na kumthamini.
Ifanye kazi kuwa kipaumbele cha kwanza kwako, ipende, ithamini na iweke kwa kiwango cha kutosha na utakuwa bora sana na kufanya mauzo makubwa.
TEKELEZA MAJUKUMU YAKO.
Wewe kama muuzaji, unayajua majukumu yako kwenye mauzo. Majukumu yako yanaweza kuwa mengi, lakini ya msingi ni kuwafikia wateja, kwa kuwatafuta mara ya kwanza na kuendelea kuwafuatilia ili wanunue na waendelee kununua. Hapo ndipo unapopaswa kuweka kazi hasa ili uwe bora na kukuza mauzo.
Itakuwa ni jambo la kushangaza sana, unajua kabisa kwamba unatakiwa uuze na ili uuze inabidi uwafikie wateja, lakini hufanyi hivyo. Utakuwa ni mtu unayeshangaza kama badala ya kuwafikia wateja wewe unahangaika na mambo mengine ambayo hayana mchango kwako kuwa bora na kuuza zaidi.
Iwe wewe ni muuzaji kwenye biashara yako mwenyewe au umeajiriwa kama muuzaji kwenye biashara inayomilikiwa na mtu mwingine, yajue majukumu yako ya mauzo na uyatekeleze.
Usisubiri kukumbushwa kutekeleza majukumu yako, usisubiri mpaka usukumwe ndiyo utekeleze majukumu yako. Kumbuka kazi ndiye rafiki yako wa kweli na kutekeleza majukumu yako ndiyo kushirikiana vyema na rafiki huyo.
Nikupe siri moja ambayo ukiifanyia kazi utafanikiwa sana; usisubiri wengine wakusukume kufanya majukumu yako, bali yafanye kiasi cha wengine kukuambia upunguze kufanya.
Kingine ninachoweza kukuambia hapa ni hiki; kama hakuna watu wanaokuambia punguza kufanya kazi au wanakuuliza unawezaje kufanya yote hayo unayofanya, basi hujaweka kazi ya kutosha, ongeza juhudi zaidi.
SOMA; Jenga Uaminifu Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
MUDA WA KAZI FANYA KAZI.
Ujue muda wako wa kazi kwenye mauzo na kwenye muda huo, fanya kazi ambazo zinachangia mauzo pekee. Kama muda wako wa mauzo ni kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa 12 jioni, basi huo muda unakuwa ni kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya mauzo tu.
Usifanye kitu kingine chochote ambacho hakina mchango kwenye mauzo kwenye huo muda. Usifuatilie habari kwenye huo muda, usiperuzi mitandao ya kijamii kama hauhisiani na kuuza, usibishane michezo na mambo mengine yasiyo na mchango wa moja kwa moja kwenye mauzo.
Muda wote wa kazi hakikisha upo ana kwa ana na wateja au unawasiliana nao kwenye simu. Kwa kutumia muda wa kazi kufanya kazi, utaweza kukamilisha mengi sana mpaka watu watakushangaa.
Ukijitathmini kwa majukumu unayoyafanya kwenye siku nzima ya mauzo, kama unafanya kazi masaa 10, masaa hasa unayofanya kazi hayazidi mawili. Huo muda mwingine wote unafanya mambo ambayo yana mchango mdogo sana kwenye mauzo au hayana mchango kabisa.
Hebu fikiria ni makubwa kiasi gani utaweza kufanya kama utageuza hizo namba, yaani kwenye masaa 10 ya kazi, 8 ukaweka kwenye majukumu yenye tija na masaa 2 ndiyo ukaweka kwenye majukumu mengine? Kwa hakika utafanya makubwa zaidi ya unavyofanya sasa. Hebu anza na hili muuzaji na uone jinsi utakavyopiga hatua kubwa kwenye mauzo.
NENDA HATUA YA ZIADA.
Kwa majukumu ya mauzo uliyonayo, yakamilishe, lakini usiishie tu hapo, nenda hatua ya ziada. Kila wakati jisukume kufanya zaidi ya ulivyopanga au unavyotegemewa kufanya. Kama umepanga kutembelea wateja 10 kwa siku, ongeza 1 au 2. Kama umepanga kupiga simu 60 kwa siku, ongeza zifike 65 au 70.
Jisukume kwenda hatua ya ziada kwa kila unachofanya, kwa sababu unao uwezo wa kufanya hivyo na kadiri unavyotumia uwezo huo ndiyo unavyozidi kuongezeka. Usikubali kwenda kwa mazoea au kuiga wengine, wewe jitofautishe kwa kwenda hatua ya ziada.
Kwa kila unachofanya, jisukume zaidi na nenda hatua ya ziada. Kuwa tofauti na wengine wanavyofanya na kuwa tofauti na ulivyofanya siku iliyopita. Kadiri unavyojisukuma zaidi ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kufanya makubwa zaidi.
ASIKUZIDI YEYOTE.
Muuzaji bora kuwahi kutokea,
Waruhusu watu wakuzidi akili,
Waruhusu watu wakuzidi elimu,
Waruhusu watu wakuzidi urefu,
Waruhusu watu wakuzidi fedha,
Waruhusu watu wakuzidi mengine ambayo yapo nje ya uwezo wako.
Lakini, kamwe, KAMWE, usimruhusu mtu yeyote akuzidi kwenye UCHAPAKAZI.
Julikana kama mtu unayechapa kazi kuliko wengine wote wanaokuzunguka.
Wape watu nafasi ya kukusema vibaya kwenye mambo mengine yote, lakini usiwaruhusu wakuseme wewe ni mvivu. Weka kazi sana kiasi cha kwamba madhaifu yako mengine yanafukiwa na hilo. Hata kama kuna madhaifu mengine unayo, watu waseme; lakini huyu ni mchapakazi.
Uchapakazi utakubeba sana kwenye maeneo mengine, utafunika madhaifu yako mengine na kukupa fursa kubwa ambazo usingeweza kuzipata kama usingekuwa mchapakazi.
TATHMINI NA BORESHA.
Punda anafanya kazi kuliko wanyama wengine wote, lakini kwa nini yeye siyo mfalme wa mwitu? Kwa sababu moja, punda anafanya kazi zisizokuwa na tija.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu, kuna ambao wanafanya kazi mno, lakini bado hawafanikiwi wala kupata fursa kubwa. hapo tatizo siyo kazi, bali tatizo ni watu wenyewe.
Huwa wanasema ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile halafu kutegemea matokeo ya tofauti. Hivyo ndivyo watu wanavyofanya kwenye kazi, wanarudia yale yale kila wakati halafu wanashangaa kwa nini hawapigi hatua.
Unapaswa kujitathmini kwenye kila kazi unayofanya na kuboresha ufanyaji wako. Kama leo unafanya ulichofanya jana, usitegemee matokeo ya tofauti. Kwa juhudi unazoendelea kuweka, hakikisha unazidi kuwa bora.
Kipimo cha ubora kwenye kazi ni kuongezeka kwa uzalishaji na ufanisi kadiri unavyokwenda na kazi. Kama hivyo vitu haviongezeki, huwezi kupiga hatua.
Uzalishaji ni majukumu unayokamilisha ndani ya muda fulani. Kwa mfano kama huwa inakuchukua saa 1 kupiga simu 10, kadiri unavyoendelea kwenda, idadi ya simu kwenye huo muda inapaswa kuwa inaongezeka. Hicho ndiyo kipimo cha kuwa bora kwenye uzalishaji.
Ufanisi ni matokeo unayozalisha ukilinganisha na juhudi unazoweka. Kwa mfano kama ukiongea na wateja 10, mmoja ananunua, kadiri unavyokwenda unatakiwa uongeze idadi ya wanaonunua katika hao 10.
Hayo yote yanawezekana kama utakuwa unajifanyia tathmini kwa kila kazi unayoweka na kuboresha zaidi.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, weka kazi, kuwa mchapakazi. Haijalishi umeanzia wapi au uko wapi sasa, popote unapotaka kufika, kazi itakufikisha hapo. Je upo tayari kuchapa kazi?
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.