Rafiki yangu mpendwa,

Najua mara nyingi umekuwa unafikiria jinsi ambavyo maisha yako yangekuwa ya raha na starehe kama usingekuwa na matatizo au changamoto unazokabiliana nazo sasa.

Ni rahisi kuona kinachofanya maisha yako yasiwe bora ni matatizo na changamoto zinazokukabilia. Lakini nataka nikuambie kitu kimoja, sababu pekee ya maisha yako kuwa na maana ni matatizo na changamoto unazopitia.

Japo unaweza kuona matatizo na changamoto vinazidisha ugumu wa maisha yako, lakini ni huo ugumu ndiyo unaokusukuma uwe bora na kufanya makubwa zaidi.

Hiyo ina maana kwamba kama maisha yako yatakosa kabisa matatizo na changamoto, yatakuwa ya hovyo kuliko yalivyo sasa. Kuthibitisha hilo, angalia maisha ya wale ambao wana kila wanachotaka kwenye maisha yao, kama hawafanyii kazi malengo makubwa yanayowasukuma, wanakuwa wanayaharibu maisha yao kwa starehe zinazogeuka mateso kwao.

Angalia wengi ambao wanayaharibu maisha yao kwa ulevi na uraibu wa madawa ya kulevya. Angalia wengi ambao wamepoteza uhai wao kwenye starehe hatari walizokuwa wanajihusisha nazo.

Tunachoweza kusema rafiki ni kwamba, maisha bila matatizo na changamoto hayawezekani. Hata kama tayari una kila unachotaka, kama una utajiri unaokupa uhuru kamili wa maisha yako, bado matatizo na changamoto havitakosekana.

Hivyo basi rafiki yangu, kama matamanio yako ni siku moja kuamka na usiwe na matatizo wala changamoto zozote, unatafuta matatizo makubwa zaidi.  Karibu uangalie kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ili uweze kuelewa kile hasa ninachomaanisha kwenye hili. Ukishaangalia kipindi hicho, utaacha mara moja kutamani maisha ambayo hayana matatizo wala changamoto.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.