3348; Haraka na ndefu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Maneno mawili ambayo yanaathiri sana muda na mipango yetu ni NDIYO na HAPANA.

Watu huwa wanakuja na mapendekezo mbalimbali kwetu. Na pia sisi wenyewe tunakutana na fursa mbalimbali.
Ni matumizi yetu ya maneno NDIYO na HAPANA ndiyo itaamua jinsi gani tutaendana na hayo yanayotokea.

Kwa kawaida na kitu ambacho kinawakwamisha wengi ni kuwa na haraka kwenye kusema NDIYO.
Matokeo yake ni mtu kujikuta ana mambo mengi ya kufanya kuliko muda alionao wa kuyafanya.

Watu wengi huwa wanakuwa na uzito sana kwenye kusema HAPANA, hata pale wanapokuwa wanajua kabisa kwamba hawatafanya kitu hicho.
Kwa kuwa hapana inaumiza na wengi hawapendi kuwaumiza wengine, wanajikuta wakisema ndiyo ambayo hawaimaanishi.

Kwa kusema ndiyo nyingi ambazo hawazimaanishi, watu wanaishia kuwakwamisha na kuwaumiza wengine pale wanaposhindwa kukamilisha yale waliyoahidi.

Kuondokana na hayo, tumia mfumo wa haraka na ndefu.
Kwa mfumo huu, unakuwa haraka kwenye kusema HAPANA.
Kwa chochote ambacho mtu anakuja nacho kwako, jibu lako la haraka ni hapana.
Hapo unakuwa umewaondoa wengi ambao hawakuwa wanamaanisha hasa kwa kile walichotaka kwao.

Licha ya kuwa na hapana ya haraka, kuna ambao wataendelea kung’ang’ana kuhusu kile wanachotaka kwako.
Hapo ndipo unapaswa kujipa muda wa kutafakari kwa kina kabla ya kusema ndiyo. Hivyo ndivyo ndiyo inavyokuwa ndefu na yenye maana kwako kabla hujaitoa.

Wengi wamekuwa wanafanya kinyume na hili, wanasema ndiyo haraka na kuchelewa kusema hapana.
Wewe unaweza kubadili hilo kwa kufanyia kazi haya uliyojifunza hapa. Kuna na hapana za haraka sana ambapo utakataa mengi unayokutana nayo.
Pia kuwa na ndiyo ambayo ni ndefu, inayokuchukua muda kwako kutafakari kwa kina kitu kabla ya kukubali.

Pia tambua ndiyo ni hapana na hapana ni ndiyo.
Unaposema ndiyo ambayo hunadhamiria, maana yake umesema hapana kwenye mambo ya msingi, kwako.
Na unaposema hapana kwenye mambo yasiyokuwa na tija, maana yake umesema ndiyo kwenye yale yenye tija.
Kuwa mfujaji wa hapana kwa kuzitoa kwa kwa wingi na bahili wa ndiyo kwa kuzitoa pale tu zinapokuwa na tija.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya kipekee tunaijenga, hapana ni neno tunalojivunia kulitumia kwa wingi na mara kwa mara.
Ili kutunza muda wetu na kupeleka umakini wetu kwenye mambo muhimu zaidi kwetu, tunatumia hapana kwa wingi zaidi.
Kuwa ndani ya jamii ambayo inafanya kitu ambacho hakijazoeleka, inakusukuma na wewe kufanya.
Huenda ungekuwa peke yako ungakubali kirahisi, lakini kwa kuambatana na watu watakuhoji kwa yote unayofanya, utafanya kwa umakini zaidi.

Zingatia sana matumizi yako ya NDIYO  na HAPANA ili yasiwe kimwazo kwako kufanya makubwa uliyopanga.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe