Rafiki yangu mpendwa,
Kila mmoja wetu ni muuzaji. Hiyo ni kwa sababu kila mmoja kuna kitu anachokitaka kutoka kwa watu wengine. Mauzo ni mchakato wa kuwashawishi wengine wakupe kile unachotaka, kwa wewe kuwapa kile wanachotaka.
Kwa wengi, mauzo yamekuwa magumu kwa sababu ya kukutana na neno HAPANA kutoka kwa wale wanaowashawishi. Kwa kuwashawishi watu na kukataliwa, wengi wamekuwa wanakata tamaa na kuona hawawezi kupata wanachotaka.
Lakini hilo siyo kweli, kila mtu anaweza kupata chochote anachotaka kwenye maisha yake, kama ataamua kweli kwamba anakitaka na kuwa tayari kukipambania kwa kila namna mpaka kukipata.
Inapokuja kwenye mauzo na mafanikio ya maisha kwa ujumla, mtu yeyote anayetaka kuyapata mafanikio, lazima awe tayari kubobea kwenye hapana. Kubobea kwenye hapana ni kuwa tayari kuzipokea kwa wingi bila ya kuumia au kukata tamaa.

Siri kuu ya mafanikio kwenye mauzo na maisha kwa ujumla haipo kwenye nini unafanya au unafanyaje, bali ipo kwenye kuuliza. Kuuliza au kuomba, kitu ambacho ni cha kawaida sana kinakuwa ndiyo siri kuu ya mafanikio, kwa sababu wengi huwa hawana uthubutu wa kufanya hivyo. Wengi kwa kuhofia kukataliwa, huwa hata hawaulizi au kuomba. Hivyo basi, wale wanaokuwa na ujasiri wa kuuliza au kuomba, wanajiweka kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa.
Rafiki yangu, wewe unapaswa kuwa mmoja wa wachache ambao wamebobea kwenye hapana, kwa kuwa na ujasiri wa kuuliza na kuomba bila ya kuhofia neno HAPANA. Na hapa unakwenda kujifunza mambo yatakayokufanya uwe imara na kuweza kukabiliana na kila hapana unayokutana nayo na kubaki ukiwa imara zaidi.
1. Penda HAPANA.
Kinyume cha hofu ni kupenda, hivyo kama unataka kuivuka hofu ya HAPANA, ipende sana. Penda kusikia neno HAPANA, furahia pale unapoambiwa hapana na hilo halitakuwa kikwazo tena kwako. Si unaijua dawa ya hofu, ni kufanya kile unachohofia. Hivyo kama unahofia neno HAPANA, litafute kwa wingi zaidi na utaacha kulihofia.
2. Hujakataliwa wewe.
Kinachowafanya wengi kuhofia na hivyo kukwepa HAPANA ni kuona wakiambiwa neno hilo basi wamekataliwa wao, hawana thamani. Huo siyo ukweli, mtu akikuambia HAPANA, hajakukataa wewe, wala hajamaanisha kwamba wewe hufai. Alichomaanisha ni hataki kile unachompendekezea. Na hilo halina ubaya wowote, kwani hakuna kitu kimoja kinachopendwa na watu wote. Hata uambiwe HAPANA nyingi kiasi gani, haitakufanya wewe ugeuke kutoka binadamu na kuwa mbuzi, sasa ya nini uogope hapana?
3. Hapana ni siyo sasa.
Hapana nyingi unazopokea, siyo hapana za dhati, bali ni siyo sasa. Yaani mtu anayekuambia hapana, hamaanishi kwamba kamwe hataki kitu hicho. Mara nyingi hapana inamaanisha kwa sasa hataki au hana uhitaji au bado hajakuamini. Hivyo unapaswa kuendelea kuuliza na kuomba bila kuacha, kuna wakati atakuwa tayari na kusema NDIYO, kitu ambacho ndiyo unataka.
4. Weka lengo la hapana.
Ili ujisukume na kuendelea kuuliza au kuomba bila kukata tamaa, jiwekee lengo la hapana unazotaka kupata kwa siku, wiki na kuendelea. Unapopanga kile unachokwenda kufanya, jiwekee hapana ngapi unataka kupata. Kwa mfano ukijiambia unataka kupata hapana 100 kwa siku, hapana moja au 10 hazikusumbui, kwa sababu unajua bado hujafikia lengo.
5. Faida na hasara.
Kila kitu unachofanya huwa kina faida na hasara na hizo ndiyo huwa tunazitumia kufanya maamuzi kwenye yote tunayofanya. Kwenye kupata hapana, hasara ni kidogo na faida ni nyingi. Hasara ni kukosa kile ulichouliza au kuomba, ambapo tayari umekosa hata kabla ya kuuliza au kuomba. Lakini faida ni nyingi, unaweza kupata ndiyo au hata ukipata hapana, unapouliza au kuomba zaidi unajisogeza karibu na ndiyo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza mambo haya matano kwa kina na mengine matano ambapo jumla yanakuwa kumi. Hayo ni mambo ambayo ukiyaelewa na kuyazingatia utaweza kubobea kwenye hapana na kufanya mauzo makubwa na mafanikio pia. Karibu ujifunze kwenye kipindi hiki ili uweze kubobea kwenye hapana na kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.