Rafiki yangu mpendwa,
Idadi ya watu wanaotaka mafanikio makubwa ni kubwa sana na idadi ya wale wanaoyapata mafanikio hayo ni ndogo sana. Tofauti hii ya wanaotaka na wanaopata haisababishwi na uwezo, kwamba kuna ambao wanaweza kufanikiwa na ambao hawawezi.
Kila mtu tayari anao uwezo mkubwa ndani yake wa kuweza kupata mafanikio yoyote makubwa anayoyataka. Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni uelewa walionao juu ya kile hasa kinachohitajika ili kupata mafanikio makubwa wanayoyataka.

Wapo ambao wanadhani kuna siri ya kupata mafanikio makubwa kwa haraka na bila ya kufanya kazi kubwa. Hawa ndiyo muda wote wanakuwa wanatafuta siri za mafanikio, wakidhani hilo ndiyo linawakwamisha. Watu hawa siyo tu wanashindwa kufanikiwa, bali pia wanaingia kwenye hasara kubwa. Kwani tamaa yao ya kutaka kupata mafanikio ya haraka huwa inawapelekea kutapeliwa.
Kitu muhimu zaidi kujua baada ya kujua kwamba unataka mafanikio makubwa ni gharama unayopaswa kulipa ili kufanikiwa. Na gharama hiyo inalipwa kwa njia kuu mbili; KAZI na MUDA. Ni lazima uweke kazi kubwa sana ili kufanikiwa na lazima pia uweke muda wa kutosha.
Kwenye kazi inaeleweka, juhudi zinapaswa kuwekwa ili kupata mafanikio. Kwenye muda ndiyo wengi huwa hawaelewi. Wengi huona kama wanachelewa kupata mafanikio pale muda unapokwenda na hawayapati mafanikio.
Kitu ambacho wengi hawajui ni miaka sahihi ambayo mtu anapaswa kuweka ili kupata mafanikio makubwa. Na kwa kiwango cha chini kabisa, mtu anahitaji angalau miaka 10 ya kuweka juhudi ndiyo aweze kujenga mafanikio makubwa.
Hiyo ni miaka 10 ya kujituma hasa na kukazana kuwa bora kadiri muda unavyokwenda. Ni miaka kumi ya kuendelea kupanda ngazi za ubora kwenye kile unachofanya mpaka kufikia viwango vya juu kabisa.
Huenda umeshafanya unachofanya kwa zaidi ya miaka 10. Iwe ni kazi au biashara, umekuwa hapo kwa miaka mingi lakini bado hujafanikiwa. Unaweza kuona hili la miaka 10 siyo sahihi. Bado ni sahihi, changamoto ni wewe umefanya kitu kwa miaka 10, lakini uzoefu ulionao ni wa mwaka mmoja tu. Pale ambapo huna tofauti kwenye ufanyaji wako kati ya mwaka mmoja na mwaka mwingine, huwezi kuhesabia ni mwaka wa uzoefu.
Hivyo unaposikia miaka 10 ya kufanya, ni miaka 10 ambayo umekuwa unakazana kuwa bora kila mwaka zaidi ya ulivyokuwa kwenye mwaka uliopita.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kuweka miaka 10 ya ubora kwenye kitu unachofanya ili uweze kujenga mafanikio makubwa. Karibu ujifunze kwenye kipindi hiki na uende ukaweke juhudi sahihi na kwa muda sahihi ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.