Rafiki yangu mpendwa,
Kama umekuta mche shambani na ukadhani ni mti wa chungwa, ukautunza vizuri, lakini wakati wa kuzaa matunda yakatoka matunda limao, itakuumiza, kwa sababu siyo ulichotarajia.
Kwa kuwa ulitegemea kupata machungwa, ila ukaishia kupata malimao, lazima utataka kufanya mabadiliko. Sasa hebu niambie, kama utaamua kuyachuma matunda yote ya limao ili msimu unaofuata upate machungwa, nini kitakachotokea?
Unajua dhahiri kabisa kwamba msimu mwingine utapata tena malimao. Hiyo ni kwa sababu huwezi kubadili matokeo kwa kuhangaika na matokeo ya nje, bali kubadili matokeo ya nje unatakiwa kubadili kwanza kile kilicho ndani.
Matokeo yoyote unayoyaona kwa nje, chanzo chake kipo ndani. Kama utahangaika na matokeo hayo, bado hutaweza kuyabadili. Ni mpaka utakapobadili kile kilicho ndani ndiyo utaweza kuyabadili matokeo ya nje.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye fedha na utajiri. Watu wengi wamekuwa wanakazana kubadilika kutoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri kwa kubadili tabia zao. Wanaweza kukazana kuongeza kipato, kuweka akiba na kuwekeza, lakini pamoja na hayo yote bado watabaki kwenye umasikini.
Hiyo ni kwa sababu matokeo ya nje huwa yanaanzia ndani, ambapo kwa mtu ni ule mtazamo ambao anakuwa nao.

Mwandishi T. Harv Eker kwenye kitabu chake kinachoitwa SECRETS OF MILLIONAIRE MIND amefundisha jinsi tunavyoweza kubadili mitazamo yetu ya ndani ili tuweze kujenga utajiri mkubwa na unaodumu.
Harv anaanza kwa kushirikisha hadithi ya maisha yake ambapo kwa miaka mingi alikuwa anahangaika lakini anabaki kwenye umasikini. Licha ya kufanya kazi na biashara mbalimbali, licha ya kuweka akiba na kuwekeza, bado alijikuta akiwa kwenye umasikini.
Ni mpaka pale rafiki wa baba yake alipomwambia kitu ambacho kilimbadili sana. Alimuuliza anadhani kwa nini hafanikiwi wakati kuna wengine wanaofanikiwa? Alimwambia haoni kwamba wale wanaofanikiwa kuliko yeye kuna namna wanafikiri na kufanya tofauti na anavyofanya yeye?
Hilo lilimfungua sana macho Harv na akadhamiria atajifunza jinsi waliofanikiwa wanavyofikiri na kufanya na kuwaiga ili na yeye afanikiwe. Na hapo ndipo alipogundua kwamba mabadiliko ambayo hayaanzii kwenye mtazamo, huwa hayadumu.
Alijifunza na ameshirikisha kanuni ambayo inaonyesha mahusiano ya mtazamo na matokeo ambayo mtu anayapata.
Ambapo mtazamo ndiyo unaamua fikra gani mtu awe nazo.
Fikra zinachochea hisia ambazo mtu anazipata.
Hisia zinamsukuma mtu kwenye hatua anazochukua.
Na hatua ndiyo zinazoleta matokeo yanayoonekana.
Sasa, wengi wanabadili matokeo kwa kubadili hatua wanazochukua na kuishia kushindwa, kwa sababu chenye nguvu ni mtazamo.
Kwenye kitabu chake, Harv ameshirikisha mitazamo 17 inayowatofautisha masikini na matajiri na kutuonyesha jinsi ya kuijenga mitazamo hiyo ili tuweze kutoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha mitazamo hiyo 17 na jinsi ya kujijengea kwenye maisha yako. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na uweze kuijua na kujijengea mitazamo hiyo ili uweze kujenga utajiri mkubwa na wa kudumu kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.