Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.
Unakuwa bora kupitia maendeleo binafsi, kwa kujifunza na kuweka kwenye matendo mafunzo ambayo yanakujengea tabia sahihi za kimafanikio. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza moja ya tabia unazohitaji ili kuwa bora na kufanikiwa kwenye kila eneo la maisha yako, ambayo ni UNG’ANG’ANIZI.

Ung’ang’anizi ni hali ya kuendelea na kitu licha ya kukutana na magumu na changamoto ambazo zinawakwamisha wengine. Ni kuendelea kufanya bila ya kukata tamaa hata pale ambapo wengine wanakata tamaa na kuacha. Ni kuvivuka vikwazo vyote unavyokutana navyo na kuendelea na safari kwa imani kubwa.
Kikwazo kikuu kikubwa kwenye mauzo ni kukataliwa. Mauzo ndiyo kazi yenye kukataliwa zaidi kuliko kazi nyingine yoyote. Unakataliwa wakati unasaka wateja, unakataliwa wakati wa kuwafuatilia na unakataliwa wakati wa kuwataka wafanye maamuzi ya kununua.
Kwa sababu mauzo yanakutaka wewe uwaombe wengine wachukue hatua fulani, ambayo kwa wakati huo wanaweza wasiwe na msukumo wa kuichukua, kukataliwa huwa ni kukubwa. Kama utakuwa mtu wa kukata tamaa na kuacha haraka, kamwe hutaweza kufanikiwa kwenye mauzo.
Tabia muhimu unayohitaji kujijengea ili uweze kuvuka hali ya kukataliwa kwenye mauzo ni UNG’ANG’ANIZI. Ukishaamua kwamba unataka kitu, ng’ang’ana nacho mpaka ukipate bila ya kuishia njiani. Kama umeshaona mteja ana sifa za kununua kwako, ng’ang’ana naye mpaka anunue. Kama umemwomba mteja akupe mawasiliano au mteja wa rufaa na akakataa, huo siyo mwisho, endelea kuomba mpaka upate.
Kwenye mauzo, unapaswa kukata shauri kwamba utapata kile unachotaka au utakufa ukiwa unakipambania. Neno kukata tamaa na kuacha halipaswi kuwa kabisa kwenye fikra zako. Hata ukutane na ugumu kiasi gani, isiingie hata kidogo kwenye fikra zako kuhusu kuacha.
Unaweza kuona mauzo ni magumu na kutaka kwenda kufanya vitu vingine, lakini ugumu wa maisha huwa haondoki, unabadilika tu. Ukijiambia mauzo ni magumu wacha ukalime, subiri pale mvua zitakapoacha kunyesha au zikanyesha za mafuriko na ukapoteza kila kitu. Au mvua zinaweza kuwa sahihi, ukavuna kwa wingi na sokoni mazao yakawa mengi kiasi cha kushindwa kuuza kwa bei nzuri.
Kipi kwenye maisha ambacho hakina vikwazo na changamoto? Hakuna. Unafikiria kufuga, kuna magonjwa ambayo yanaweza kuua mifugo, kuna gharama za ufugaji na bado kuna soko lisiloeleweka.
Hakuna namna unaweza kukimbia magumu na changamoto za maisha. Kwa kuwa upo kwenye mauzo, hapo ndipo pa kuyaendesha mapambano yako mpaka ufanikiwe. Hapo ndipo pa kung’ang’ana mpaka upate kile unachotaka.
SOMA; Jenga Uaminifu Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
Aliyewahi kuwa raisi wa Marekani, Calvin Coolidge amewahi kunukuliwa akisema; “Hakuna chochote hapa duniani kinachoweza kuchukua nafasi ya ung’ang’anizi. Kipaji hakiwezi; hakuna kinachopatikana kwa wingi kama watu wenye vipaji ila hawana mafanikio. Kuwa na akili sana hakuwezi; kuna wengi wenye akili ila hawajafanikiwa. Elimu haiwezi; dunia imejaa watu wenye alimu kubwa ila hawana mafanikio. Ni maamuzi ya dhati na ung’ang’anizi ndivyo vyenye nguvu. Kauli mbiu ya ‘Endelea kwenda!’ imetatua matatizo mengi ya wanadamu.”
Ni dhahiri unawajua watu wenye vipaji vikubwa lakini hawana mafanikio, kwa sababu hawakuweza kuwa na ung’ang’anizi kwenye kitu kimoja, kila mara walikuwa wanahangaika na vitu vipya wakitafuta urahisi.
Unawajua wenye akili nyingi lakini maisha yao hayana mafanikio, kwa sababu hawakuweza kung’ang’ana na kitu kimoja mpaka kiwape matokeo. Akili zao nyingi ziliwahangaisha na mambo mengi na kushindwa kufanikiwa.
Wenye elimu kubwa na hawana mafanikio ndiyo wamejaa kila kona, hasa kwa zama hizi ambazo wengi wamesoma na kazi za ajira hazipo. Hawa wenye elimu wakipata kazi ambayo siyo waliyosomea, kazi kama ya mauzo, huwa hawajitoi kwenye na kung’ang’ana, wanajiona wamejishikiza tu kwa muda wakisubiri kazi ya ndoto yao. Kazi hizo zimekuwa hazipatikani na kwenye kile wanachofanya hawafanikiwi kwa sababu hawajajitoa kweli na kung’ang’ana.
Unaweza kuwa mmoja wa wenye hizo sifa hapo juu na bado hujaweza kuyaona mafanikio makubwa. Unaweza kuwa una vipaji, una akili na elimu kubwa, lakini bado hujawa na mafanikio unayoyataka kwenye maisha yako.
Leo umejua hapa nini kinakukwamisha, ambacho ni kukosa ung’ang’anizi. Toka hapa ukiwa na maamuzi ya aina moja tu, unakwenda kung’ang’ana na mauzo. Unakwenda kujifunza kila kitu kuhusu mauzo na kuwa muuzaji bora. Unakwenda kukaa kwenye mauzo mpaka upate mafanikio makubwa unayoyataka na bado utaendelea kuweka juhudi.
Kwa kufanya maamuzi ya aina hiyo na kuyasimamia, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Kwa kumalizia, tupate kauli ya aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Winston Churchill, ambaye alipata kusema; “Kamwe usikate tamaa. Kamwe usikate tamaa. Kamwe, kamwe, kamwe, kamwe – kwa lolote, kubwa au dogo, muhimu au siyo muhimu — usikate tamaa, isipokuwa kwa mambo mazuri na ya heshima.”
Maamuzi ya wewe kufanya hapa ni kwenye safari yako ya mauzo, KAMWE USIKATE TAMAA, ENDELEA KUNG’ANG’ANA mpaka upate mafanikio unayoyataka. Uwezo wa kufanikiwa unao na nyenzo zote unazohitaji ili kufanikiwa kwenye mauzo unazo, ni wewe kuchukua hatua bila kuacha ili kuyapata mafanikio kwa uhakika.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.