Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri mkubwa kwa kutumia fedha ndogo ndogo tunazokuwa nazo.
Tunaendelea kujifunza kuhusu uwekezaji wa pamoja kupitia mifuko ya uwekezaji inayosimamiwa na UTT AMIS. Tayari tumejifunza mifuko mitano ambayo ni UMOJA, WEKEZA MAISHA, WATOTO, JIKUMU NA UKWASI.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza mfuko wa sita wa uwekezaji wa pamoja kwenye UTT AMIS ambao ni mfuko wa HATIFUNGANI. Kabla ya kuangalia mfuko huo kwa kina, kwanza tupate uelewa uwekezaji wa hatifungani maana yake ni nini.

MAANA YA UWEKEZAJI WA HATIFUNGANI.
Uwekezaji wa hatifungani ni kuikopesha taasisi fedha ambapo inaitumia kwenye shughuli zake na kukulipa wewe riba kwenye fedha hiyo. Huu ni uwekezaji ambapo unachangia mtaji na unalipwa riba kwa kipindi kilichopangwa. Kwenye kila kipindi utalipwa riba, huku msingi uliowekeza ukibaki vile vile. Mwisho wa uwekezaji unarudishiwa msingi wote uliowekeza.
Uwekezaji wa hatifungani ndiyo salama zaidi ukilinganisha na uwekezaji mwingine kwenye masoko ya mitaji. Hii ni kwa sababu kuyumba kwa uchumi huwa hakuathiri moja kwa moja kupanda na kushuka thamani ya uwekezaji kama ilivyo kwenye hisa. Kwani ukishanunua hatifungani ni umeingia mkataba na taasisi husika, kwamba watakupa riba kiasi fulani. Riba itaendelea kutolewa hiyo hiyo hata kama kuna mabadiliko ya uchumi. Na mtaji uliowekeza utabaki vile vile hata kama kuna kupanda na kushuka kwa soko.
Hatari ya kupoteza kwenye hatifungani ni pale taasisi ambayo umenunua hatifungani zake inapofilisika, hapo ndipo unakuwa umepoteza. Lakini hata kwenye hatua hiyo ya kufilisikia, kama kuna fidia itakayotolea, basi watu wa kwanza kufidiwa ni wale wenye hatifungani kabla hawajafidiwa wenye hisa.
Pamoja na uimara huo wa uwekezaji wa hatifungani, bado ni uwekezaji ambao marejesho yake yapo chini ukilinganisha na uwekezaji mwingine kwenye masoko ya mitaji.
MFUKO UTT AMIS WA HATIFUNGANI
Mfuko wa Hatifungani ni mfuko wa wazi unaowekeza kwenye dhamana za serikali za muda mrefu, hatifungani za kampuni binafsi na kwenye soko la fedha. Mfuko ulianzishwa tarehe 16 Septemba 2019 na hutoa fursa kwa wawekezaji kukuza mtaji pamoja na kupata gawio.
MALENGO YA MFUKO
Mfuko wa hatifungani ni mfuko wa wazi unaolenga kutoa gawio kila mwezi au kila baada ya miezi sita na kumpa mwekezaji fursa ya kukuza mtaji.
UKWASI/KUUZA VIPANDE
Malipo ya mauzo ya vipande yatashughulikiwa ndani ya siku 10 za kazi baada ya kupokelewa. Fedha zitatumwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya mwekezaji.
NANI ANARUHUSIWA KUWEKEZA
Mfuko huu uko wazi kwa mwekezaji Mtanzania na asiye Mtanzania, aliye ndani au nje ya nchi, watu binafsi (ikijumuisha watoto) na wawekezaji wasio watu binafsi, vikundi na taasisi.
SERA YA MFUKO
Mfuko unaruhusiwa kuwekeza kwenye sehemu zenye vipato vya kudumu. Dhamana zenye mapato ya kudumu zinajumuisha zaidi ya 90% ya uwekezaji na 10% zilizobaki huwekezwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
SIFA ZA MFUKO
Mfuko unatoa machaguo matatu ya uwekezaji kama ifuatavyo;
1. Mpango wa kukuza mtaji
2. Mpango wa gawio kila mwezi
3. Mpango wa gawio kila baada ya miezi sita
Kiwango cha chini cha kuanza kuwekeza:
(a) TZS. 50,000 kwa mpango wa kukuza mtaji;
(b) TZS. 10,000,000 kwa mpango wa gawio kila mwezi; na
(c) TZS. 5,000,000 kwa mpango wa gawio kila baada ya miezi sita.
Kiwango cha chini cha nyongeza katika uwekezaji ni TZS. 5,000 kwa mipango yote ya uwekezaji.
SIFA ZA MFUKO
1. Mfuko unawafaa wawekezaji binafsi, taasisi, vikundi au mashirika.
2. Umiliki wa mtu mmoja au umiliki wa pamoja unaruhusiwa katika mfuko huu.
3. Hakuna gharama za kujiunga (entry load) wala kutoka kwenye mfuko (exit load).
4. Mfuko unaruhusu uhamishaji wa vipande kutoka mwekezaji mmoja kwenda kwa mwekezaji mwingine.
5. Mwekezaji akifariki, mrithi, mwakilishi au mwombaji wa pili ataruhusiwa kuendeleza uwekezaji huo.
6. Vipande vinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo katika taasisi za fedha.
7. Hakuna ukomo wa kiwango cha juu cha uwekezaji.
KWA NINI UCHAGUE MFUKO WA HATIFUNGANI WA UTT?
Kwa jinsi uwekezaji wa hatifungani ulivyo, taasisi zote zinazotoa hatifungani huwa zinatangaza kuuza hatifungani zake. Hatifungani za serikali huwa zinatangazwa na benki kuu. Hatifungani za taasisi nyingine huwa zinaorodheshwa kwenye soko la hisa.
Wewe kama mwekezaji unaweza kwenda moja kwa moja sokoni na kununua hatigungani na hivyo kutokuhitaji kutumia taasisi nyingine kama UTT AMISA. Lakini je kwa nini bado uwekeze kwenye hatifungani za UTT badala ya wewe kwenda moja kwa moja sokoni?
Hapa kuna sababu za kwa nini sisi wawekezaji wa NGUVU YA BUKU tunapaswa kuwekeza kwenye hatifungani za UTT badala ya kwenda sokoni moja kwa moja;
1. Urahisi wa mchakato wa kuwekeza. Mchakato wa kuwekeza kwenye hatifungani za UTT ni kuchagua na kuwekeza. Mchakato wa kuwekeza kwenye hatifungani nyingine unahusisha kuweka dau lako, na kisha kusubiri kama umeshinda kulingana na madau waliyoweka wawekezaji wengine. Mchakato huo ni mrefu na unaochukua muda.
2. Urahisi wa kuwekeza. Kwa Hatifungani za UTT unawekeza kwa urahisi, kwa kununua vipande kwa njia ya simu au nyinginezo. Hatifungani nyingine ni mpaka ununue kwenye taasisi husika ambapo utahitaji kuingia makubaliano ya kiuwekezaji.
3. Kiasi kidogo cha kuwekeza kisichoathiri faida. Kwa hatifungani za UTT, kiasi cha kuanza kuwekeza ni cha chini ukilinganisha na hatifungani nyingine. Lakini pia faida unayopata ni ile ile bila kuathiriwa na kiasi au muda wa uwekezaji. Kwa hatifungani nyingine, kianzio huwa ni kiasi kikubwa na faida inaathiriwa na kiasi unachowekeza na muda wa kuwekeza. Kwa mfano anayenunua hatifungani ya miaka 5 anaweza kupata asilimia 6 kwa mwaka, wakati atakayenunua hatifungani ya miaka 10 akapata asilimia 9 kwa mwaka.
4. Urahisi wa kuuza uwekezaji. Kwa hatifungani za UTT, unaweza kujitoa muda wowote kwa kuuza uwekezaji wako na kulipwa fedha zako. Kwenye hatifungani nyingine, kujitoa kunachukua mchakato, ni mpaka hatifungani iorodheshwe kwenye soko la hisa na kuwepo na watu wanaotaka kununua hatifungani hiyo. Hivyo unaweza usipate fedha kwa haraka kama unavyoweza kuwa unataka.
5. Muda wa mwisho kuwekeza. Kwa hatifungani za UTT, hakuna muda wa mwisho kuwekeza, unaweza kuendelea na uwekezaji huo kwa muda mrefu utakavyo. Kwa hatifungani za taasisi nyingine, unaponunua zinakuwa zimepewa muda, kwa mfano miaka 10. Pale miaka hiyo 10 inapoisha unarudishiwa uwekezaji wako na kama utataka utawekeza tena kwenye hatifungani nyingine.
Kwa sababu hizo, tunachagua kuwekeza kwenye mfuko wa hatifungani wa UTT ili kujenga utajiri mkubwa kwa kutumia fedha kidogo kidogo tulizonazo.
MJADALA WA SOMO.
Karibu ushiriki mjadala wa somo hili kama sehemu ya kushirikisha ulivyoelewa somo na maswali kama unayo. Kushiriki mjadala huu, jibu maswali yafuatayo.
1. Eleza jinsi uwekezaji wa hatifungani unavyotofautiana na uwekezaji wa hisa.
2. Eleza jinsi mfuko wa hatifungani wa UTT unavyofanya kazi na mipango mitatu kwenye uwekezaji huo.
3. Eleza kwa nini sisi wawekezaji wa NGUVU YA BUKU tumechagua mfuko wa hatifungani wa UTT badala ya kwenda sokoni moja kwa moja.
4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo juu ya somo la leo na programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kwenye kundi la mafunzo kama sehemu ya wewe kushiriki mafunzo haya na kuyafanyia kazi ili kujenga utajiri kupitia uwekezaji.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.