Fikiria mfano wa wakata miti wawili. Wote wamepewa eneo moja la kukata miti na wameenda na mapanga yao. Mkata miti Y anafanya kazi ya kukata siku nzima bila kupumzika. Mkata miti Z anapumzika kila baada ya muda, kisha kuendelea tena. Mwisho wa siku, mkata miti Y amekata miti 3, huku mkata miti Z amekata miti 7. Mkata miti Y anamuuliza mwenzake; “Umewezaje kukata miti mingi kuliko mimi wakati kuna muda ulikuwa unapumzika?” Mkata miti Z akamjibu; “Sikuwa napumzika, nilikuwa nanoa panga langu kila mara ili kuongeza makali.”

Je, ni kwa namna ipi unaenda kuongeza makali katika biashara au huduma yako? Jibu ni kupitia kujifunza zaidi. Hapa chini nimeainisha njia tano za kutumia kujifunza;

Moja; Njia ya kusafiri
Kupitia kusafiri, unapata nafasi ya kubadilisha mazingira na kujifunza vitu vipya ikiwemo ujuzi mpya kupitia  kuona  wengine wanavyofanya kazi zao au kuendesha maisha yao.

Mfano: mfanyabiashara akienda nje ya Eneo jipya, au kwa watu wapya unajifunza jinsi watu hao wanavyofanya biashara zao, namna ya kuwakaribisha na kuwahudumia wateja wao.

Kupitia kusafiri, unajenga marafiki wapya kutoka sehemu mbalimbali. Hii ni kwa sababu hakuna mafanikio ya mtu mmoja, yanatokana na uwepo wa watu wengine.

Marafiki wanao mchango mkubwa katika mafanikio yako. Unapokuwa unasafiri, unapata nafasi ya kuongeza marafiki. Hawa huwa ni marafiki wa uhakika, maana mnakutana katika mazingira na sehemu sahihi. Hivyo, kila mmoja huwa anaogopa kumpoteza mwenzake. Unajikuta mnafanya mambo makubwa yanayochangia maendeleo kwenye vitu mnavyofanya.

Mbili; Njia ya maswali
Unaweza kujiuliza; kwa nini maswali kama nimeishamaliza shule? Ukweli ni kwamba, huwezi kujua kila kitu. Yaani ujue kuhusu mapishi, kutibu watu, kuendesha chombo cha usafiri, uongozi, ushonaji, uchoraji na vitu vingine. Lazima kuna eneo moja ulilobobea na ndilo unaweza kulielezea vema kwa mtu au kulifanyia kazi vema.

Chukulia mfano, wewe ni mfanyabiashara. Una lengo kubwa la kuwa mbobezi kwenye mauzo. Umekutana na mteja, ukamuelezea mawili matatu kuhusu biashara yako. Mteja akasema; hii biashara au bidhaa zako nazijua sana. Nimewahi kuzitumia, zikaniletea matatizo. Sitaki kuziona au kuzitumia tena. Badala ya wewe kuwa mbogo na kuanza kugombana naye, huku ukisema anakufukizia wateja, hajui anachoongea au bidhaa anayoijua sio. Unachofanya ni kumuuliza swali, tena kwa upole wa hali ya juu. Je, unajua nini kuhusu bidhaa hii?

Huulizi kwa sababu hujui. Unauliza uli upate uone kama mteja anaelewa zaidi biashara yako. Pale unapouliza swali, mhusika anajibu swali hilo kwa njia ya maelezo. Kupitia maelezo hayo, unapata nafasi ya kupata jawabu la swali lako. Hali inayokufanya ujifunze kitu kipya ambacho hukuwa unakijua.

Tatu; Kupitia usomaji wa vitabu na tafiti
Kama ukiniuliza leo ni ujuzi upi mtu anahitaji kuwa nao, nitakuambia ujuzi wa kusoma vitabu. Ukifanikiwa angalau kusoma vitabu 12 kwa mwaka sio mbaya ambapo kila mwezi kitabu kimoja. Ila mwenzio ninao uwezo wa kusoma kitabu kimoja kwa siku moja hadi tatu na kukimaliza bila kujali kina kurasa ngapi.

Unaposoma kitabu, unapata maarifa mengi kwa mkupuo. Unakuta mwandishi ili akamilishe kitabu chake anapaswa afanye maandalizi ya mwaka mmoja na zaidi. Huku akizunguka sehemu tofauti, akifanya utafiti na kuongea na watu juu ya mada alizoweka katika kitabu chake. Akiamka usiku wa manane, anaandika.  Hadi mwisho kitabu kinakamilika, anakuwa amechoka. Lengo kuu ni ili wewe upate kilicho bora.

Unapoanza kusoma kitabu hicho, unaanza kupata yale maarifa ya pamoja  ndani ya muda mfupi.
Ipo hivyo hivyo hata kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na watu tofauti tofauti. Wanachukua muda mrefu kutembea sehemu tofauti wakitafuta data. Ili wewe ukiwa unasoma tafiti hizo, uwe na habari za kutosha. Wanapomaliza wazichapishe na kuziweka tayari kwako kuzisoma. Utafiti unaweza kuchukua miezi sita au miaka kadhaa lakini wewe unausoma ndani ya siku moja na kupata majibu ya utafiti uliofanywa.

Nne; Kupitia semina au warsha
Warsha ni mkusanyiko wa watu wanaokutana ili kujadiliana na kufanya shughuli maalumu. Kupitia warsha, washiriki wanahusika moja kwa moja kwa njia mbalimbali ikiwa kujifunza kwa vitendo na kufanya mazoezi yanayojenga ujuzi wanaoutumia katika kufanya jambo fulani.

Mfumo huu una manufaa sana kwenye kujenga ujuzi mpya ambao watu wanauhitaji katika kutekeleza majukumu yao. Kwani wanapata uelewa na mazoezi ya kuwawezesha kutumia ujuzi huo. Kupitia majadiliano mbalimbali yanayofanyika, mtu hujikuta amepata mafunzo zaidi.

Maana kwenye warsha kunakuwa na mada mbalimbali wanazozungumzia. Mfano; kama ni warsha kuhusu masuala ya fedha. majadiliano yote yatahusu fedha. Kama ni kilimo, majadiliano na wataalamu wengi watagusia masuala ya kilimo. Ikiwa wewe ni mmojawapo mwenye malengo ya kukuza kilimo au katika eneo la kifedha mafunzo utakayopata yatakusaidia zaidi.

Tano; Video na audio
Kwenye safari ya kujifunza, sio kila wakati utakuwa unasoma asubuhi, mchana na jioni. Kuna muda utahitaji kuangalia video mbalimbali na kusikiliza mafundisho kupitia simulizi ambazo ni audio. Kupitia video, unataka kuona kitu kinavyofanyika. Kupitia audio, unasikiliza kitu kinavyopaswa kufanyika.

Inawezekana hujui ukweli huu. Watu wengi wanao uwezo wa kuzungumza yale waliyoona, kusikia au kujua kuliko kuandika. Unapokuwa msikilizaji mzuri wa audio, unapata nafasi ya kujifunza zaidi mambo mengi. Hii inakusaidia kukamilisha safari yako ya kutimiza lengo fulani.

Muhimu; Kile unachojifunza hakikisha unakifanyia kazi. Wengi tunajifunza na kupuuzia yale tunayojifunza. Ukiwa mtu wa kujifunza utafanikiwa katika biashara au huduma yako. Naamini hadi hapo Silaha hii ya kujifunza unaenda kukifanyia kazi kwa ukubwa.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz