Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye biashara, mauzo ndiyo moyo wenyewe. Ni mauzo ndiyo yanafanya biashara kuendelea kuwa hai, kwa sababu ndiyo yanayoleta fedha kwenye biashara.

Biashara siyo taasisi ya serikali, dini au misaada. Bali biashara ni taasisi ya kiuchumi ambayo itaweza kujiendesha kama tu inafanya mauzo. Hiyo ndiyo njia kuu ya biashara kuingiza fedha na kuendelea kuwepo.

Ili biashara iweze kuuza, lazima iwe na wateja ambao wanaiamini na kuwa tayari kulipa fedha na kupata kile kinachouzwa. Ni kwenye kupata wateja wanaokuwa waaminifu kwenye biashara ndipo kazi nyingine kubwa ya biashara ilipo.

Ugumu wa kupata wateja unatokana na usumbufu mwingi ambao umewazunguka watu kwenye zama hizi. Usumbufu huo umeteka umakini wa watu wengi kiasi kwamba kuwafikia, kuwapata na kukaa nao kwa muda mrefu inahitaji kazi kubwa.

Ili kuvuka usumbufu huo unaowatinga wateja unaowalenga, unapaswa kupiga kelele sana. Hapa kupiga kelele inamaanisha kuwafikia wateja wengi zaidi kule waliko na kujua kuhusu biashara yako.

Tunaita hilo kupiga kelele kwa sababu inabidi lifanyike kwa ukubwa na kurudia rudia bila kuacha. Ukifanya mara moja na kudhani umemaliza, utashangazwa na jinsi ambavyo wengi hawatakumbuka hata kama upo.

Wateja unaowalenga wanakutana na taarifa nyingi sana kila siku, hivyo chochote ambacho hawakisikii mara kwa mara, wanakisahau haraka. Njia yoyote unayotumia kuwafikia wateja, iwe ni ana kwa ana, mawasiliano au matangazo ni lazima uifanye kwa wingi na ukubwa, huku ukirudia rudia bila kuacha.

Huo ndiyo uhalisia wa kupata wateja kwenye biashara, lakini bado wengi wamekuwa hawaufanyii kazi. Wanadhani mpango mwingine wanaoweza kuwa nao unafanya kazi kuliko kupiga kelele. Lakini matokeo yanadhihirisha kwamba haufanyi kazi. Matokeo ya mauzo madogo ambayo watu wanayapata yanaweka bayana kwamba bila kupiga kelele nyingi, kupata wateja inakuwa vigumu.

Swali ni kwa nini watu wengi hawapendi kupiga kelele za kutangaza biashara zao kwa watu wengi zaidi? Kwa nini wengi hawapo tayari kuhakikisha watu wengi sana wanajua kuhusu biashara wanayofanya? Kuna baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakiwapelekea wengi kutokuwa tayari kupiga kelele.

Moja ni mtazamo usio sahihi kwamba kizuri kinajiuza na kibaya kinajitangaza. Huu ni usemi ambao wengi wamekuwa wanautumia kwa kiburi, kwa kudhani wakiwa na kitu kuzuri basi watu watakuja wao wenyewe. Ni kweli, watu wanapenda vitu vizuri, ila kwanza lazima wajue vilipo. Hivyo hata kama una kitu kizuri kiasi gani, kama watu hawajui kipo, hawataweza kukifuata. Kuwa na kitu kizuri na piga kelele kwa wengi ili kuwafikia wengi na kuwafanya waje kwenye biashara.

Mbili ni kiburi kingine cha watu kuona kazi ya kupiga kelele siyo ya hadhi yao. Umewahi kuwaona wasanii, wachekeshaji na watu wengine wanavyofanya vituko mbalimbali ili taarifa zao ziwafikie wengi zaidi? Zote hizo ni njia za kupiga kelele na zimekuwa zinawasaidia kuwafikia wengi. Sasa kuna watu huwa wanajipa umuhimu kwa kuona kazi ya kutangaza na kuuza siyo ya hadhi yao. Kitu kimoja ambacho wengi hawakijui ni kwamba hata wale ambao tayari wameshafanikiwa sana, bado wanaendelea kupiga kelele bila kuchoka. Hivyo achana na hicho kiburi na upige kelele, hiyo ndiyo njia pekee ya kuwafikia wateja wengi na kufanya mauzo makubwa.

Kuna sababu nyingine ambazo zimekuwa zinawakwamisha watu wasipige kelele zinazohitajika ili kupata wateja wanaowataka. Nimezieleza sababu hizo kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Karibu ujifunze kupitia kipindi hicho na utoke na msukumo wa kwenda kupiga kelele kwa wingi na ukubwa na kuweza kuuza zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.