Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo kwa kuchukua hatua ndogo ndogo (kuanza na elfu moja) na kwa muda mrefu (angalau miaka 10).

Kuna aina nyingi za uwekezaji, kuanzia kwenye mali na masoko ya mitaji. Ndani ya masoko ya mitaji kuna hisa, hatifungani na mifuko ya pamoja. Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumechagua uwekezaji wetu mkuu kuwa wa mifuko ya pamoja.

KWA NINI UWEKEZAJI MIFUKO YA PAMOJA.

Sababu za kuchagua uwekezaji wetu mkuu kuwa kwenye mifuko ya pamoja (mutual funds) ni kama ifuatavyo;

1. Kiwango kidogo cha kuweza kuanza na kuendelea kuwekeza.

2. Urahisi wa kuwekeza ukiwa popote, kupitia simu na benki.

3. Kutohitaji elimu kubwa ya uwekezaji.

4. Kutohitajika kufuatilia sana uwekezaji, hivyo kuweza kuendelea na majukumu yetu mengine.

5. Urahisi wa kuuza uwekezaji na kupata fedha pale unapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo (ukwasi).

KWA NINI MIFUKO YA PAMOJA YA UTT.

Uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja (mutual funds) upo wa aina nyingi pia. Yaani kuna taasisi mbalimbali ambazo zinatoa uwekezaji wa aina hii. Kwenye programu ya NGUVU YA BUKU tumechagua mifuko ya pamoja ya UTT kwa sababu zifuatazo;

1. Ukongwe wa taasisi hii kwenye tasnia hii ya uwekezaji. Kwa zaidi ya miaka 20 UTT imekuwa kwenye huu uwekezaji na kufanya vizuri.

2. Wingi wa mifuko na hivyo kuwepo na uwanja mpana wa kuchagua. UTT wana mifuko sita mpaka sasa.

3. Taasisi iko chini ya usimamizi wa serikali kupitia wizara ya fedha, hilo linafanya kuwa salama zaidi.

MPANGO BINAFSI WA UWEKEZAJI KWA KILA MMOJA.

 Pamoja na sisi wote kuwa kwenye programu moja ya NGUVU YA BUKU na kuwekeza kwenye taasisi moja ya UTT, bado kila mmoja wetu atakuwa na mpango wake binafsi kulingana na malengo aliyonayo.

Tumeshajifunza mifuko yote sita ya UTT, na hiyo ndiyo kila mmoja ataitumia kupangilia uwekezaji wake kwa muda mrefu.

Katika kupangilia uwekezaji binafsi, kuna vitu vya kuzingatia kama ifuatavyo;

1. Kuanza uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kukuza kwa muda mrefu, utatumia MFUKO WA UMOJA. Huu ni mzuri kwa uwekezaji mdogo mdogo ambao huna mpango wa kutoa.

2. Kuwafundisha watoto uwekezaji na kuwafanyia maandalizi ya baadaye, utatumia mfuko wa WATOTO.

3. Kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha ambacho unaweza kukitoa pale unapokuwa na matumizi nacho, utatumia mfuko wa UKWASI. Mfano kama unafanya biashara na sehemu kubwa ya faida unaiweka ili ikifika kiasi fulani ufanye kitu kikubwa kwenye biashara, badala ya kuweka akiba hiyo benki ambapo hakuna ongezeko kubwa, unaweka kwenye mfuko wa UKWASI ambao unakupa ongezeko kubwa kuliko benki. Na unapotaka kutoa fedha hiyo unaipata kwa haraka bila ya gharama za kutoka.

4. Kama unataka kupata bima ya maisha ili jambo lolote linapotokea uweze kunufaika, unatumia mfuko wa WEKEZA MAISHA.

5. Unapotaka kipato cha mara kwa mara pale unapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha na hutaki kukitumia, unawekeza kwenye mfuko wa JIKIMU.

6. Pale unapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha na ungependa kuwa unaingiza kipato cha kila mwezi bila kuathiri kiasi hicho cha fedha, unawekeza kwenye mfuko wa HATIFUNGANI. Kwa mfano mtu aliyepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, iwe ni mafao, fidia, mirathi au kushinda bahati nasibu, wengi hutumia fedha hizo kwa pupa na kupoteza zote. Lakini mtu akiwekeza kiasi hicho chote kwenye mfuko kama wa HATIFUNGANI, anakuwa anapata kipato cha kila mwezi huku uwekezaji wake ukiendelea kuwepo na kukua thamani. Hii ni njia bora sana kwa wastaafu, kuliko kutumia mafao yao kwenye miradi inayohitaji usimamizi ambao hawawezi kufanya, wanaweza kuyawekeza hivi na wakawa wanapata kipato cha kila mwezi, kulingana na kiasi walichonacho.

SABABU ZAIDI ZA UWEKEZAJI.

Pamoja na kuwekeza kwa sababu ya kukuza thamani na kutengeneza kipato cha baadaye, kuna sababu nyingine ambazo mtu unaweza kuwa nazo kwenye kufanya huu uwekezaji kupitia mifuko ya pamoja. Baadhi ya sababu hizo ni kama ifuatavyo;

1. Kujenga dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kwa shughuli zako mbalimbali. Uwekezaji huu unaweza kutumika kama dhamana wakati wa kuomba mkopo. Tena ni dhamana inayopewa kiasi kikubwa cha uwekezaji na kwa urahisi kuliko dhamana nyingine.

2. Kujenga mfuko mbadala wa mafao ya uzeeni. Kuna mifuko ya pensheni ya serikali, lakini huwa ina changamoto mbalimbali, hasa inapofika wakati mtu amestaafu na anataka kupata fedha zake. Kwa waajiriwa, unaweza kutumia mifuko hii kama mfuko mbadala wa pensheni. Kwa waliojiajiriwa na wanaofanya biashara ambao hawana mfumo rasmi wa pensheni, mifuko hii ni sehemu nzuri kujijengea utaratibu ninafsi wa mafao.

3. Kuwa na ukwasi ambao utakusaidia pale unapokuwa na uhitaji. Tumeona jinsi ambavyo mtu anaweza kuwa na thamani kubwa ya utajiri, lakini akihitaji kiasi kikubwa cha fedha, anakosa kwa sababu mali anazokuwa nazo hawezi kuuza haraka. Kwa kuwa na uwekezaji kwenye hii mifuko ya pamoja, inakuwa rahisi kupata fedha.

4. Kufanya uwekezaji wa pamoja kulingana na vikundi ambavyo watu wanaweza kuwekeza kwa malengo mbalimbali ya pamoja waliyonayo.

5. Kuwaandaa watoto kwa ajili ya uwekezaji na mipango yao mingine ya baadaye kama elimu n.k.

NI MUHIMU KUWA NA MPANGO BINAFSI WA UWEKEZAJI.

Pamoja na kuwa pamoja kwenye programu moja, lazima kila mtu awe na mpango wake binafsi wa uwekezaji ambao ataenda nao ili kutimiza malengo aliyonayo.

Kinachowaangusha wengi kwenye uwekezaji ni kukosa mipango binafsi, matokeo yake wanajikuta wakifuata mkumbo na kuishia kupoteza kuliko kunufaika.

Unapokuwa na mpango wako binafsi na unaoufuata, unajiona ukiwa unapiga hatua, kwa sababu kila unachofanya kinachangia kwenye matokeo unayotaka kuyapata.

Weka mpango wako binafsi wa uwekezaji kwa kipindi cha miaka 10 na zaidi ijayo kisha nenda nao kwa kipindi chote tunachokuwa pamoja kwenye hii programu ya NGUVU YA BUKU. Utajiona ukiwa unapiga hatua kubwa kadiri tunavyokwenda.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kwenye somo hili kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Kwa nini kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua uwekezaji wa mifuko ya pamoja ya UTT?
2. Zipi sababu zako binafsi za kufanya uwekezaji kwenye hii programu ya NGUVU YA BUKU?
3. Shirikisha mpango wako binafsi wa uwekezaji ambao ndiyo unafanyia kazi kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU.

4. Kama una swali lolote kuhusu somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU, karibu uulize. (Muhimu; usiulize maswali ambayo yalishajibiwa kwenye masomo na mijadala ya nyuma, rejea masomo hayo na mijadala ambayo imeshafanyika.)

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama ushahidi kwamba umesoma somo, kulielewa vyema na kwenda kuchukua hatua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.