Rafiki yangu mpendwa,
Umewahi kupita kwenye njia ambayo mbele kuna ajali imetokea? Bila shaka uligundua kuna foleni inayofanya magari kwenda taratibu. Kabla hujafika kwenye ajali, unaweza kudhani ajali hiyo imeziba barabara.
Lakini unapofika eneo la ajali, unagundua ajali haijaziba barabara hata kidogo, yaani barabara iko wazi kabisa. Sasa swali ni nini kinafanya kuwe na foleni? Na hapo jibu unalo, kwa sababu kila anayefika pale kwenye ajali, anapunguza mwendo na kuangalia nini kinachoendelea.
Kinachokuwa kinasababisha foleni kwenye eneo la ajali siyo ajali yenyewe, bali tabia ya watu kutaka kuangalia na kuona nini kinaendelea pale kwenye ajali.
Huo ni mfano rahisi na halisia wa jinsi sisi binadamu tulivyo. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, ambapo mambo mengi tunayoyafanya ni kwa sababu watu wengine nao wanayafanya.

Kwa sehemu kubwa sana, mambo tunayoyafanya ni kwa sababu wale wanaotuzunguka nao wanayafanya. Tunaweza kutamani sana kufanya mambo ya tofauti na ya kipekee, lakini nguvu ya kufanya yale yanayofanywa na wengine ni kubwa kuliko tunavyoweza kuipinga.
Kwa mfano kama utafanya kitu chako cha tofauti na ukashindwa, watu watakucheka na utajisikia vibaya, kwa sababu umeshindwa wewe mwenyewe. Lakini kama utafanya kile ambacho kinafanywa na wengine na wote mkashinda, mtafarijiana kwamba imekuwa nje ya uwezo wenu.
Hivyo kwa vyovyote vile, kufanya yale ambayo yanafanywa na wengine inaonekana kuwa salama kwa wengi kuliko kufanya mambo yao wenyewe. Na huo ndiyo msukumo utakaokuwa nao kwenye yote unayofanya, kuangalia wengine wanafanya nini na wewe kufanya.
Sasa basi, tatizo kubwa kwako kufanikiwa siyo kuangalia au kutokuangalia wengine, bali ni nani unaowaangalia. Kwa sababu wale unaowaangalia ndiyo watakaoamua kiasi cha mafanikio utakayoyapata.
Kama unawaangalia wale ambao hawajafanikiwa, utaishia kupata matokeo kama yao, ambayo ni kutokufanikiwa. Na kama utawaangalia wale waliofanikiwa, utapata matokeo kama yao, ambayo ni mafanikio.
SOMA; Tabiri Mafanikio Yako Kwa Hiki Kipimo Cha Uhakika.
Kwa kifupi, kama unataka kupata ushindi, unapaswa kuwaangalia washindi. Usipoteze muda wako kuwaangalia watu ambao hawapo pale unapotaka kufika. Kwa popote ambapo unataka kufika kwenye maisha yako, watafute ambao wameshafika hapo tayari na waangalie hao, jifunze kutoka kwao.
Hakuna siri kubwa sana kwenye mafanikio, ni kuangalia jinsi ambavyo waliofanikiwa wanafikiri na kufanya na kisha kufanya kama wao. Haitakuwa rahisi, lakini kama utaweka juhudi, hutabaki pale ulipo sasa.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ujifunze jinsi ya kuchagua watu sahihi wa kujifunza kutoka kwao ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako. Fungua kipindi hapo chini ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.