Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja kwenye mafanikio, umekuwa unataka kuyapata. Umeenda mbali zaidi na kupanga jinsi ya kuyapata, nini ufanye ili kufanikiwa. Lakini sasa, inapofika wakati wa kutekeleza mipango uliyoweka, unaona haupo tayari na hivyo kujipa muda wa kusubiri.

Unaweza kujishawishi kwamba haujawa tayari kuanza yale uliyopanga, lakini huo siyo ukweli wenyewe. Ukweli ni kwamba kuna kitu kinakuzuia kufanya, lakini hutaki kukiri hilo. Unatumia kisingizio cha kutokuwa tayari kama sababu ya kutokuanza.

Kinachokuzuia kuanza siyo kutokuwa tayari, bali hofu unayokuwa nayo. Unapatwa na hofu kwenye kuanza kwa sababu unayokuwa umeyapanga ni mageni kwako, ni mambo ambayo hujazoea kuyafanya. Kwa sababu hujazoea kufanya, huna uhakika wa matokeo unayokwenda kupata, na hilo ndiyo linalokupa hofu.

Kwa kutokujua kwamba hofu ndiyo inakuzuia imekuwa kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Umekuwa unajisubirisha sana, ukijiambia unajiandaa, ukipanga utaanza kesho, lakini umekuwa huanzi. Sababu kubwa ni ile hofu ya kufanya vitu vya tofauti.

Sisi binadamu ni viumbe wa mazoea, mambo mengi tunayoyafanya kwenye maisha yetu ni vile tulivyozoea kuyafanya. Hivyo inapohitajika kufanya jambo lolote la tofauti, hofu huwa inatuingia kwa sababu hatuna mazoea nalo.

Kwa nguvu hiyo ya hofu, na kufanya kazi bila ya sisi kujua, imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa watu kufanikiwa. Imekuwa ni breki inayowazuia watu kufanya makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wao.

Ili kujenga mafanikio makubwa, hatua ya kwanza ambayo mtu anatakiwa kuchukua ni kuweza kuivuka hiyo hofu ambayo imekuwa kikwazo kwake. Ili kuweza kuivuka hofu na kuweza kufanya makubwa, kuna mitazamo mikubwa miwili ambayo unapaswa kujijengea.

Mtazamo wa kwanza ni HOFU NI KIASHIRIA cha nini unapaswa kufanya. Wakati hofu inatupata, huwa tunaitumia kama sababu ya kughairisha au kuacha kufanya. Pale tunapopata hofu, tunaacha. Hilo ndiyo la kwanza kubadilisha, unapoingiwa na hofu, usiache kufanya, bali chukulia kama kiashiria cha kufanya. Pale unapokuwa na hofu ya kufanya kitu, jua hicho ndiyo kitu sahihi kufanya. Tafsiri hofu kama dalili unatoka kwenye mazoea uliyonayo, kitu ambacho ni kizuri. Hivyo badala ya kujiambia unaacha au kusubiri, unapaswa kuchagua kufanya, kwa sababu hicho ndiyo kitu sahihi kufanya, na kufanya sasa.

SOMA; Tumia Mbinu Hii Ya Falsafa Ya Ustoa Kushinda Uvivu Na Kufanya Makubwa.

Mtazamo wa pili ni DAWA YA HOFU NI KUFANYA UNACHOHOFIA. Huu ndiyo mtazamo ambao utakuwezesha kuivuka hofu na kufanya makubwa kadiri ya unavyokuwa unataka. Kujua kwamba dawa ya hofu ni kufanya kile unachohofia kufanya. Hivyo unapopatwa na hofu, huyumbishwi kwa namna yoyote, kwa sababu unajua utaishinda kwa kufanya hivyo unachohofia. Kila unapokutana na hofu, kabiliana nayo kwa kufanya na siyo kuacha. Unapaswa kufanya, tena mara moja badala ya kusubiri kwa muda mrefu.

Kwa mfano, kama umekuwa na hofu ya kuongea mbele ya watu, hofu ambayo ni kubwa na imekuwa inawazuia wengi, unapaswa kutumia kila fursa unayopata kuongea mbele ya watu kufanya hilo. Pale unapokuwa kwenye mkutano wowote na ikatokea nafasi ya kusema kitu, jitolee kufanya hivyo. Utapatwa na hofu, lakini jiambie utafanya na hapo utaweza kufanya na kuishinda hofu. Kama kuongea kwenye kundi kubwa unapata hofu zaidi, unaweza kuanza na makundi madogo madogo na kwenda ukiongeza ukubwa wa kundi unaloongea kadiri unavyozidi kuishinda hofu.

Kitu kingine muhimu kuelewa kwenye hofu ni njaa ambayo unapaswa kuipa. Hofu inakuwa na nguvu kwako pale unapoilisha chakula. Na chakula cha hofu huwa ni muda. Kadiri unavyoipa hofu muda, ndivyo inavyozidi kukua na kukomaa na kuweza kukukwamisha zaidi. Lakini ukiinyima hofu muda, unakuwa umeiweka kwenye njaa na inakuwa dhaifu kiasi kwamba haiwezi kukusumbua.

Pale unapopanga kufanya kitu halafu ukapatwa na hofu, unapaswa kuamua kukifanya mara moja. Usijipe muda wa kutafakari zaidi kuhusu kitu hicho, anza mara moja kufanya. Unapoanza mara moja, matokeo yoyote utakayoyapata yatakuonyesha kwamba hofu siyo kubwa au mbaya kama ulivyokuwa unajiambia. Na hapo utapata nguvu ya kuendelea kufanya  zaidi na zaidi.

Rafiki, hayo ni ya msingi ambayo ukiyafanyia kazi, utaweza kuvuka kila aina ya hofu inayokukabili na kufanya makubwa kwenye maisha yako. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa kina zaidi dhana hii ya hofu na jinsi ya kuitumia kufanya makubwa badala ya kuruhusu iwe kikwazo. Fungua kipindi hicho uweze kujifunza na uache kukwamishwa na hofu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.