Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.
Unakuwa bora kupitia maendeleo binafsi, kwa kujifunza na kuweka kwenye matendo mafunzo ambayo yanakujengea tabia sahihi za kimafanikio. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza moja ya tabia unazohitaji ili kuwa bora na kufanikiwa kwenye kila eneo la maisha yako, ambayo ni USIKIVU.
SANAA ILIYOSAHAULIKA.
Moja ya sanaa muhimu na iliyosahaulika kwenye mahusiano ya watu ni kusikiliza. Tunaishi kwenye zama ambazo kila mtu anakazana kupiga kelele na hakuna mtu anayemsikiliza mwenzake.
Changamoto nyingi kwenye mahusiano zinaanzia kwenye watu kushindwa kusikilizana. Kila mtu anataka kuongea na hakuna aliye tayari kumsikiliza mwingine.
Watu wengi wamekuwa wanashindwa hata kupata mawazo mapya ya kutatua changamoto wanazokutana nazo kwa sababu hawapati watu wa kuwasikiliza. Watu wanajikuta wakiwa na msongo mkubwa kwenye maisha yao, ambao ungeweza kuisha kama wangepata watu wa kuwasikiliza.
Ili kuboresha mahusiano yako na watu kwenye kila eneo la maisha yako, kuanzia maisha binafsi mpaka kwenye mauzo, kuwa msikivu. Jenga tabia ya kuwa unawasikiliza watu kwa umakini mkubwa.
Kwa kuwa hicho ni kitu ambacho kimekuwa adimu sana kwenye zama hizo, utaonekana ni wa tofauti na watu watakuwa tayari kukuambia mambo mengi kadiri ya unavyotaka.
Ukweli ni kwamba, kama unataka watu wakuambie kila unachotaka, wewe kuwa msikilizaji mzuri. Hakuna kitu ambacho watu wanapenda kama kusikilizwa kwa umakini. Unapowapa umakini wako wote, wanajikuta wakijieleza mpaka mambo ambayo hawakuwa wamepanga kuyasema.
Ili kuwa mtu bora na muuzaji bora pia, kuwa msikilizaji mzuri, watu watakuambia siri zao walizozificha kwa wengine.

KUJUA HUJUI.
Unapoongea, unasema kile ambacho tayari unakijua, lakini unaposikiliza, unajifunza vitu ambavyo ulikuwa huvijui. Ukijifanya mjuaji na kuwa mwongeaji sana, kamwe hutajifunza vitu vipya. Utaendelea kubaki na vile vile ambavyo unavijua na ambavyo kwa bahati mbaya sana siyo vingi.
Unapoongea wewe, unaeleza vile ambavyo unavijua wewe na ambavyo kwa sehemu kubwa ni kuhusu wewe. Unapowasikiliza wengine, wanakuambia vile wanavyojua wao, ambavyo pia ni kuwahusu wao.
Unapokutana na wengine na wewe ukawa mwongeaji sana, ni kujifanya unawajua wao kuliko wanavyojijua wenyewe, kitu ambacho siyo sahihi. Tayari uko na watu wanaojijua kuliko unavyowajua wewe, kwa nini usikae kimya na kuwasikiliza wakikuambia kuhusu wao wenyewe?
Kila unapokutana na watu wengine, jua kwamba hujui chochote kuhusu wao. Hilo litakufanya uwe mnyenyekevu na kutaka kujifunza kuhusu watu hao kupitia kusikiliza kwa umakini mkubwa.
Hata kama kuna namna ulikuwa unawachukulia watu hapo awali, kila unapopata nafasi ya kuzungumza nao, weka mtazamo wako pembeni na kuwa tayari kujifunza upya kuhusu wao. Waache wakufundishe kuhusu wao na hilo litakuonyesha fursa za kuweza kuwashawishi wakubaliane na wewe.
Kila mtu unayezungumza naye, jua kuna vitu anavyojua na wewe huvijui, hata kama ni kuwahusu wao wenyewe, maisha yao au kazi zao. Wajibu wako ni kujifunza kutoka kwao na utaweza kujifunza kama utakuwa msikivu. Kuwa msikilizaji mzuri na utajifunza mengi sana kutoka kwa watu.
SOMA; Kuwa Mchapakazi Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUWA MSIKIVU.
Ili kuwa msikivu na kunufaika kwenye kila mazungumzo unayoshiriki, zingatia mambo haya ya msingi kabisa.
1. Weka umakini wako wote kwa mtu anapokuwa anazungumza. Usiwe unafanya kitu kingine chochote wakati mtu anazungumza, badala yake umakini weka kwake. Hata kama unazungumza kwa simu, mtu atajua kama umeweka umakini wako kwake au kuna mambo mengine unayofanya.
2. Uliza maswali pale unapotaka mtu afafanue zaidi au unapotaka kumpeleka kwenye aina fulani ya mazungumzo. Uliza maswali ambayo ni ya kujieleza na siyo maswali ya kujibu NDIYO au HAPANA. Ni kupitia mtu kujieleza ndiyo unajifunza mengi kuhusu yeye. Uzuri ni ukiuliza maswali yako vizuri, watu watakuambia kila unachotaka kujua kuhusu wao.
3. Ondoa kila aina ya usumbufu unaoweza kuingilia mazungumzo unayofanya na mtu. Kama mazungumzo ni ya ana kwa ana, hakikisha hutumii simu yako wakati mwingine anazungumza. Pia epuka mambo ambayo yanakatisha mazungumzo unayofanya na mtu. Ni bora kufanya mazungumzo yenye umakini wote kwa muda mfupi, kuliko mazungumzo yenye usumbufu kwa muda mrefu.
4. Tumia lugha ya vitendo kuashiria umakini ulioweka kwenye mazungumzo ambayo mtu anafanya. Pale kunapokuwa na jambo la kushangaza, onyesha kushangaa. Pale inapokuwa ni kitu cha kusikitisha, sikitika na wewe pia. Haya yote huhitaji hata kuyaigiza, unachohitaji ni wewe kuweka umakini wako wote kwenye mazungumzo ambayo mtu anafanya na moja kwa moja utajikuta ukiwa na lugha hiyo ya vitendo.
5. Mtu anapomaliza kuzungumza na kuwa zamu yako, usikimbilie kujibu, badala yake hesabu moja mpaka tano (siyo kwa sauti) kabla hujaanza kuzungumza. Hiyo itamfanya mtu aone umetafakari yale aliyokueleza kabla ya kujibu. Pale unaporukia kujibu pale tu mtu anapomaliza kuzungumza, unaonekana hukuwa unasikiliza, bali ulikuwa unasubiri zamu yako ya kuzungumza ifike ili ujibu.
6. Toa mrejesho kwenye kila mazungumzo ambayo unafanya na mtu kuonyesha kwamba umeelewa au kueleweka. Pale mtu anapokueleza kitu, kuhakikisha umemwelewa vyema mwambie; Kwa nilivyokuelewa, unamaanisha …. Hapo mtu atakujibu ndiyo kama ndivyo alivyomaanisha au kuboresha pale unapokuwa umeelewa tofauti.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, kama unataka kuwa bora na kuuza zaidi, basi fuata namba ya viungo vyako. Una mdomo mmoja na masikio mawili. Hicho ni kiashiria kwamba unapaswa kusikiliza mara mbili ya unavyoongea.
Ni kupitia kusikiliza kwa makini ndiyo utaweza kuwaelewa watu vizuri na kuweza kuwashawishi wakubaliane na wewe kwenye kile unachotaka wakubali. Uzuri ni kwamba usikivu ni kitu ambacho kila mtu anaweza kujifunza na kukifanya.
Inaweza kuwa vigumu kwako mwanzoni kwa sababu ya mazoea ambayo tunayo kwenye zama hizi za kelele. Lakini kila unapozungumza na mtu, pata picha kuna taa inammulika yule anayezungumza. Wajibu wako ni kupata taswira taa hiyo ipo kwa mtu gani zaidi. Kama ni kwako unaongea sana na utashindwa kumshawishi mtu. Kama ni kwake unasikiliza zaidi na utaweza kumshawishi.
Kuwa msikilizaji mzuri na makini na kwa hakika utaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.