3359; Mafanikio siyo kile kinachoonekana.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanakimbizana na vitu vingi ambavyo havina tija kabisa kwao kupata kile wanachotaka, ambacho ni mafanikio makubwa.

Kwenye mitandao ya kijamii, wengi wamekuwa wanatumia idadi ya wafuasi kama kipimo cha kupata fedha na mafanikio kwa ujumla.
Lakini kiuhalisia hilo siyo sahihi, wafuasi unaokuwa nao kwenye mitandao wanaweza wasiwe na maana yoyote kulingana na kile unachofanya na wanavyohusika.
Hata kwenye maisha halisi, wingi wa wafuasi au watu wanaokukubali bado siyo kipimo halisi cha mafanikio.

Katika njia za kuingiza kipato, biashara ndiyo njia ambayo ni ya uhakika na isiyokuwa na ukomo wowote.
Hivyo kila anayeingia kwenye biashara, anakuwa anaona amefika kwenye njia ya uhakika ya kupata fedha.
Lakini hilo pia siyo kweli, siyo kila biashara ina uwezo wa kuingiza fedha kadiri ya inavyohitajika.
Kuna kazi kubwa inayopaswa kufanyika mpaka biashara iweze kuingiza fedha kwa uhakika.

Lakini pia wanaoingia kwenye biashara huwa wana msukumo wa kuwa huru.
Kwa kuwa kwenye biashara, wanaona wanakuwa huru kufanya mambo yao kadiri ya wanavyokuwa wakitaka wenyewe.
Lakini hilo nalo linategemea kiasi cha kazi inayokuwa imewekwa ili kuifanya biashara hiyo kuwa chanzo cha uhuru wa kweli.

Ukipima mafanikio kwa yale yanayoonekana kwa nje utakuwa unajipoteza wewe mwenyewe.
Hiyo ni kwa sababu yanayoonekana kwa nje, mizizi yake inakuwa inaanzia ndani.
Hiyo ina maana kwamba kila anayeyataka mafanikio makubwa, anapaswa kujua anachopaswa kufanya ili kuyapata na kisha kuweka kazi ya kutosha kuleta matokeo yanayohitajika.

Jua kiini hasa cha mafanikio makubwa unayokuwa unayataka na kisha pambania kujenga mafanikio hayo kwa uhakika.
Uzuri wa maisha ni huwa yanakupa kile unachokipambania hasa.
Ukiacha kuhangaika na yale yanayoonekana kwa nje na kufanyia kazi kwa uhakika yale ya ndani, utaweza kujenga mafanikio makubwa unayokuwa unayataka.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mafanikio ya uhakika ndiyo kitu kikuu kinachotusukuma kufanyia kazi.
Hatuhangaiki na mambo yanayoonekana kwa nje, badala yake tunazama ndani kwenye chanzo halisi cha mafanikio yanayohitajika.

Kwenye KISIMA tunajua ushindi wa uhakika ni kujua kinachopaswa kufanyika kisha kuweka kazi ya kutosha katika kukifanya.
Kwa sehemu kubwa ushindi ni kutokuacha kufanya yale ambayo ni muhimu.
Hata kama hutakuwa wewe unayeyafanya moja kwa moja, lazima uwe na watu sahihi ambao watahakikisha yale ya msingi yanafanyika.

Wewe chagua kuhangaika na yale muhimu ya msingi na ambayo matokeo yake yanaadhiri maeneo mengine yote.
Ni kwa nji hiyo ndiyo unaweza kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu kwa muda mrefu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe