Rafiki yangu mpendwa,
Kama unafanya biashara au unafanya mauzo na lengo lako ni kufanya mauzo makubwa sana ili uweze kuongeza kipato chako na kupata kila unachotaka, basi leo nina habari kali kwako; ACHA KUWARIDHISHA WATEJA.
Najua unaweza kushtushwa na hiyo taarifa, ambayo hukuitegemea itoke kwa mtu anayefundisha mafanikio, biashara na mauzo. Lakini huo ndiyo ukweli ambao unapaswa kuuelewa kama kweli unayataka mafanikio.
Tuanze kwenye msingi mkuu wa biashara na mauzo ambapo lengo la kwanza ni kutengeneza wateja waaminifu kwenye biashara. Wateja ambao siyo tu watanunua mara moja, bali watarudi tena na tena kununua na pia watawaleta wengine nao wanunue.

Ukija kwenye hitaji la kutaka kuwaridhisha wateja, ni kitu kigumu sana ambacho binadamu yeyote anaweza kukikamilisha. Kumridhisha binadamu ni kitu kigumu mno, kwa sababu asili ya binadamu ni kutokuridhika.
Fikiria wakati unaanzia chini kabisa, ulijiambia ukifika hatua fulani utaridhika, lakini ulipofika hatua hiyo nini kilitokea? Uliona hatua nyingine kubwa zaidi na kuona ile uliyofika haikuridhishi. Hivyo ndivyo binadamu tulivyo na huwezi kuwabadili watu kwenye hilo.
Hivyo basi, kama unaendesha biashara yako au mauzo yako kwa kutaka kila mteja aridhike, kusiwe na malalamiko yoyote, utashindwa. Utashindwa kwa sababu utahangaika sana na wateja wachache, ukitaka waridhike na mwisho wa siku bado hawataridhika.
Kwa hali hiyo ya binadamu kutokuridhika, tunapaswa kuondoa kuwaridhisha wateja kwenye malengo yetu ya kibiashara.
Kama kuwaridhisha wateja siyo lengo sahihi, lipi sasa litakuwa lengo?
Lengo sahihi kwenye biashara na mauzo ni hili; WAAHIDI WATEJA MAKUBWA NA TIMIZA KILA UNACHOWAAHIDI, KWA KWENDA HATUA YA ZIADA. Hilo ndiyo lipo ndani ya udhibiti wako, kuahidi makubwa na kutekeleza kama ulivyoahidi.
Kwa kuwa ahadi umetoa wewe, ni wajibu wako kupambana mpaka kutekeleza kama ulivyoahidi. Kuhusu mteja kuridhika, hilo ataamua yeye mwenyewe, kwa kulinganisha matokeo anayoyapata kupitia wewe na kabla ya hayo.
Uzuri ni kwamba, kama utawaahidi wateja makubwa, ambayo hawajawahi kuahidiwa pengine na kisha ukayatimiza kwa namna ambayo hawajawahi kutimiziwa mahali pengine, wengi watajikuta wanaridhika na kile wanachopata.
Japokuwa siyo wote watakaoridhika, bado kuna ambao watataka zaidi, bado kuna ambao watakuwa na malalamiko ya hapa na pale. Na pia kuna ambao wataacha kununua kwako hata kama umefanya makubwa kiasi gani.
SOMA; Wateja tarajiwa wapo wengi zaidi.
Kuzuia hayo yasiathiri mauzo yako, kuna jukumu jingine kubwa sana unalotakiwa kulifanya. Na jukumu hilo ni kila wakati kuwa unawafikia wateja wengi zaidi wapya na kuwashawishi wanunue kwako.
Kamwe usije ukajisahau kwa sababu una wateja wanaonunua kwako sasa. Umeshaona watu huwa hawaridhiki, anaweza kutokea mtu mwingine akawapa hata ahadi za uongo na wakawa tayari kukuacha, licha ya yale makubwa umewafanyia.
Itakuwa ni matatizo yako binafsi kama utawalaumu wateja ambao hawajaridhika na kile unachowapatia. Wajibu wako ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa wengi zaidi kila wakati ili usitegemee wateja wachache ulionao ambao wanaweza wasiridhike na makubwa unayofanya, wakaondoka na kukuacha mikono mitupu.
Wajibu wa kufanya mauzo kwenye biashara yako ni wako na wala siyo wa wateja. Kuwategemea wateja ulionao kwenye uhakika wa mauzo ni kujiweka kwenye wakati mgumu, kwani watakapoondoka, mauzo yako yataathirika sana.
Kila wakati ni wajibu wako kukazana kutengeneza wateja wapya tarajiwa. Kila wakati toa ahadi ambazo ni kubwa. Na kila wakati kazana kutimiza ahadi hizo. Ni kwa mwenendo huo ndiyo utaweza kufanya mauzo makubwa na ya uhakika mara zote.
Karibu ujifunze zaidi dhana hii ya kutokuhangaika kuwaridhisha wateja kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.