Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.

Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.

Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Kila wakati kwenye biashara ni wa kusaka wateja wapya na hivyo kila muuzaji anapaswa kutumia njia mbalimbali kukamilisha hilo.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja kwa kutumia mfumo wa Whatsapp Broadcast.

KWA NINI WHATSAPP NI MUHIMU KWENYE MAUZO.

Whatsapp ni mtandao wa mawasiliano kwa njia ya ujumbe wa maandishi, picha, sauti na video ambao una watumiaji wengi zaidi duniani. Inakadiriwa zaidi ya watu bilioni 3 wanatumia Whatsapp duniani na nchini Tanzania ni zaidi ya watu milioni 10.

Kwa namba hizo, tunaona jinsi ambavyo watu wengi wanatumia mtandao huo kwa mawasiliano mbalimbali. Kwa kuwa lengo la mauzo ni kuwafikia wateja wengi zaidi, njia bora ya kuwafikia ni ile ambayo tayari watu wanaitumia.

Mtandao wa whatsapp umekuwa rahisi kutumiwa na watu wengi na umekuwa sehemu ya mawasiliano ya watu kila siku. Kupitia mawasiliano ya mtu mmoja mmoja na hata makundi ya pamoja ya watu wanaoshirikiana kwa namna fulani.

Kwa wingi huo wa watu wanaotumia mtandao wa whatsapp, unaufanya kuwa sehemu muhimu ya kuwafikia wateja.

Zipo njia mbalimbali za kuwafikia wateja kwa mtandao wa whatsapp kama ifuatavyo;

1. Kutuma ujumbe mfupi kwa mtu mmoja mmoja.

2. Kutuma picha, sauti na video.

3. Kutuma jumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja (broadcast).

4. Kuwa kwenye makundi mbalimbali kwa ajili ya kuwafikia wengi.

5. Kutumia status ili kufikisha ujumbe kwa wengi.

6. Kuwa na channel ambayo inakuwa na wafuasi ambao unaweza kuwafikia.

Kwenye masomo haya ya USAKAJI tunaangalia maeneo makubwa mawili, Whatsapp broadcast na Whatsapp status.

Somo hili ni kwa ajili ya Whatsapp broadcast na litakalofuata litagusia Whatsapp status.

JINSI WHATSAPP BROADCAST ZINAVYOFANYA KAZI.

Whatsapp broadcast ni njia ya kutuma ujumbe mmoja kwa watu wengi (kiwango cha juu kwa sasa 256) kwa mara moja bila ya gharama za ziada.

Wewe unatuma ujumbe kwenye eneo moja, lakini kila aliyepo kwenye orodha anapokea peke yake, hivyo kuona kama umemtumia yeye tu.

Ni njia bora ya kuwafikia wateja bila ya kuwaweka kwenye kundi la pamoja kwa sababu wateja wengi hawapendi kuwekwa kwenye makundi ambayo yana watu wengi wasiowajua.

Kwa kutuma ujumbe kwa watu wengi, inarahisisha zoezi la kuwafikia wengi kwa muda mfupi. Kwa mfano kama unataka kuwafikia wateja elfu 1, kutuma ujumbe kwa mmoja mmoja itachukua muda mrefu. Lakini ukituma kwa broadcast , unatuma mara nne tu na unakuwa umekamilisha zoezi zima. Yaani ni sawa na kutuma ujumbe kwa watu wanne, ila uwafikie watu elfu 1.

Changamoto ya kutuma ujumbe kwa wengi kwa whatsapp broadcast ni unakuwa huwezi kutaja jina la mtu mmoja mmoja kama tulivyoona kwenye mifumo ya kutuma jumbe fupi kwa wengi (BULK SMS).

Pia ukituma jumbe kwa namba nyingi ambazo hazijahifadhi namba yako, wakikuripoti unafungiwa namba yako hivyo kushindwa kuendelea kutuma hizo broadcast.

SOMA; Usakaji Na Ufuatiliaji Wa Wateja Kwa Kutuma Ujumbe Wa Simu Kwa Watu Wengi.

JINSI YA KUJENGA BROADCAST ZAKO.

Ili kujenga broadcast ambazo ndiyo utakuwa unatuma jumbe, unahitaji kuwa na namba za whatsapp za wale unaowalenga. Ni lazima uhifadhi namba hizo kwenye whatsapp yako ndiyo uweze kuwaweka kwenye broadcast.

Njia rahisi ya kujenga broadcast ni kufanya usakaji ambapo utapata namba za whatsapp za wateja ambao unataka kuendelea kuwafuatilia. Usakaji unaweza kuwa wa kuomba rufaa, kutembelea, simu, jumbe za kawaida au matangazo.

Kwa namba zote unazopata za wateja, hifadhi kwenye whatsapp yako na kama zipo whatsapp, ziweke kwenye broadcast.

Kwa kuwa broadcast moja ina ukomo wa watu 256 tu wanaoweza kuwekwa kwa mara moja, utahitaji kuwa na broadcast nyingi kulingana na idadi ya wateja ulionao ambao unawafuatilia. Uzuri ni unaweza kuwa na broadcast nyingi uwezavyo, hivyo ukishajaza broadcast, fungua nyingine.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE MATUMIZI YA WHATSAPP BROADCAST.

Ili kuweza kupata matokeo mazuri kwenye kuwafikia wateja wengi kwa kutumia whatsapp broadcast, zingatia yafuatayo;

1. Hakikisha wateja wote unaotaka kuwafikia umewahifadhi vizuri na wameingia kwenye broadcast kama ambavyo umepanga. Kama una mawasiliano mengi umehifadhi kwenye whatsapp yako inaweza kuwa rahisi kuwasahau baadhi.

2. Washawishi wateja nao wahifadhi namba yako kwenye wasap zao, hilo litapunguza malalamiko na kuripotiwa kitu kinachopelekea namba yako kufungiwa na kushindwa kutumia kabisa huduma za whatsapp. Japo namba ikifungiwa unaweza kuomba ikafunguliwa, lakini kama itafungiwa mara kwa mara, itakuwa na athari.

3. Pangilia vizuri utumaji wako wa jumbe kwa njia ya whatsapp broadcast. Kulingana na wateja ulionao wa kuwafuatilia na jumbe unazowapelekea, usipeleke kwa wingi sana kiasi cha kuwachosha na kuamua kukuzuia (kublock) na wala usipeleke kwa uchache sana kiasi cha kukusahau. Angalau mara moja kila wiki ni kiasi kizuri cha kutuma, japo unaweza kubadili kulingana na hali yako.

4. Tuma jumbe ambazo zinawashawishi wateja wakujibu kwa kukuuliza maswali au kutaka kupata taarifa zaidi. Ukiwapelekea maelezo marefu na yaliyokamilika, moja hawatayasoma na wakiyasoma hawatakuwa na cha kukuuliza. Fanya kama unawasiliana na mtu moja kwa moja kwa kupeleka jumbe fupi na zinazowasukuma kukujibu. Ujumbe unatuma kwa wengi kwa pamoja, ila kila mmoja anakujibu kivyake na hapo utaendelea nao kulingana na kile mnachojadiliana.

5. Kwa wateja wanaojibu jumbe unazotuma kwa broadcast, endeleza mawasiliano zaidi kwa kufanya mazungumzo ya simu na kuwashawishi kuchukua hatua inayofuata kwenye mchakato wako wa mauzo. Wengi hawawezi kuchat kwa muda mrefu kulingana na majukumu yao. Hivyo kitendo cha wao kujibu ni kiashiria kwamba ujumbe uliowapelekea umewagusa na hivyo unahitaji kuwashawishi zaidi wachukue hatua.

6. Epuka kutumia broadcast kama sehemu ya kutuma matangazo ya kile unachouza, wateja watapuuza na kutokufungua kama hawana uhitaji. Wazoeshe kwamba ujumbe wowote unaotoka kwako una manufaa kwao na watakuwa na tabia ya kufungua jumbe zako na kujibu. Hilo litaimarisha mahusiano yako na wateja na kuweza kuwashawishi kwa urahisi.

Kama muuzaji, tumia mtandao wa whatsapp vizuri kwa kuwaweka wateja wote unaowafuatilia kwenye broadcast na kuwa na mpango mzuri wa kuwapelekea jumbe zinazowashawishi kujibu. Kwa njia hiyo utaweza kuwapasha moto wateja wa baridi mpaka wanakuwa tayari kununua, bila ya kutumia gharama kubwa au kupoteza muda mwingi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.