Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio makubwa yamekuwa ni kitu kinachowashangaza wengi, kwa sababu hawaelewi kwa kina ni kwa namna gani yanavyotokea.

Kwani watu wawili, wanaweza kuzaliwa kwenye mazingira yanayofanana, wakapata elimu sana na wakaanza kazi au biashara katika hali ambayo ni sawa.

Lakini miaka 10 baadaye, mmoja akawa amefanikiwa sana wakati mwingine ameshindwa kabisa.

Hapo ndipo watu wanaposhindwa kuelewa nini kinawatofautisha watu kwenye mafanikio. Na kwa sababu binadamu huwa hatupendi kukaa na kitu tusichokielewa, hadithi nyingi huanza kutengenezwa.

Na moja ya hadithi hizo huwa ni imani za kishirikina, kwamba wale wanaofanikiwa sana kuna namna wanatumia imani za kishirikina katika kujenga mafanikio yao makubwa.

Na pale ushahidi wa imani za kishirikina unapokosekana, basi watu huona wale waliofanikiwa sana ni kwa sababu ya bahati walizokutana nazo kwenye safari yao ya maisha.

Ukweli ni kwamba, kuna tofauti kati ya wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Na kwa sehemu kubwa tofauti hizo siyo za nje ambazo zinaonekana, bali ni za ndani kabisa.

Kwa nje watu wote wanaweza kuonekana sawa, lakini kwa ndani wanakuwa tofauti kabisa. Na hilo linaanzia kwenye mtazamo ambao watu wanakuwa nao na kwenda kwenye uwezo wao wa kipekee na vipaji walivyonavyo.

Kwa bahati nzuri sana, kwenye uwezo na vipaji, kila mtu amepewa, ila vinavyotofautiana. Hakuna ambaye yupo hapa duniani na akawa hana uwezo mkubwa ndani yake na vipaji vya kipekee.

Kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa wanapuuza uwezo mkubwa walionao na vipaji vyao na kuishia kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kabisa. Mambo hayo yanawapotezea muda na nguvu na kuwarudisha nyuma. Wakati wale wanaofanikiwa wanajitambua mapema na kutumia uwezo na vipaji vyao kupiga hatua.

Lakini tofauti kubwa kabisa, ambayo ndiyo inawatofautisha kabisa wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni mtazamo ambao watu wanakuwa nao. Wale wanaofanikiwa sana huwa wana mtazamo ambao unawafanya waweze kujenga mafanikio makubwa. Wakati wanaoshindwa wanakuwa na mtazamo unaowazuia kujenga mafanikio makubwa.

Mtazamo huwa unaanzia kwenye namna ya kufikiri na kisha namna ya kufikiri inaathiri namna ya kufanya. Watu wengi wanafikiri kwa udogo sana kiasi kwamba hata wakipata wanachotaka, bado kinakuwa ni kidogo.

SOMA; TABIA ZA KITAJIRI

Wale wanaofanikiwa huwa wanafikiri kwa ukubwa sana, kiasi cha wao wenyewe kutishika na fikra hizo kubwa. Hizo ndizo zinazowasukuma kufanya makubwa sana na kupata mafanikio ambayo hayajawahi kuonekana kwa walio wengi.

Grant Cardone kwenye kitabu chake kinachoitwa 10X Rule, ameshirikisha tofauti 32 kati ya watu wanaopata mafanikio makubwa na wale wanaoshindwa. Tofauti hizo ni za msingi kabisa na zinaanzia kwenye kufikiri na kufanya. Ukizielewa na kuzifanyia kazi, hutaweza kubaki hapo ulipo sasa, ni lazima utapiga hatua kubwa.

Ujumbe mkuu kutoka kwa Cardone ni kama utafikiri kwa ukubwa sana na ukafanya kwa ukubwa sana, ukiwa na mapenzi ya hali ya juu sana yanayoambatana na nidhamu kali sana, ni lazima utafanikiwa. Hata kama mengine yote yatakuwa magumu kiasi gani, ukianza na hivyo na ukaenda bila kuacha, lazima utafanikiwa.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimezifafanua tofauti zote 32 za wanaofanikiwa sana na wanaoshindwa. Fungua kipindi ujifunze tofauti hizo kwa kina, uziweke kwenye maisha yako na uweze kujenga mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka wewe mwenyewe. Karibu ujifunze na kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.