3360; Wanachokitaka watu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kanuni ya uhakika ya kupata kila unachotaka ni kuwapa watu kile wanachotaka.
Swali la msingi ni je watu wanataka nini hasa?
Hapa ndipo wengi wanaposhindwa kujua kwa uhakika na hivyo kushindwa kuwashawishi wawape kile wanachotaka wao.
Wengi hapa huishia kubahatisha nini hasa watu wanataka ili wawape na kupata kile wanachotaka wao.
Lakini huwa ni rahisi sana kujua ni nini ambacho watu wanakitaka zaidi.
Utalijua hilo kwa kutumia saikolojia ya binadamu.
Kwa saikolojia ya binadamu, watu huwa wanataka zaidi kile ambacho hawana au hawajakipata kiasi cha kutosha.
Hata kama siyo kitu muhimu zaidi kwenye maisha, ni asili yetu binadamu kutaka zaidi kile ambacho hatuna.
Ndiyo maana hata furaha zimekuwa hazidumu. Kwa sababu huwa tunaanza na lengo la kupata kitu au kufika hatua fulani. Tunapambana kufikia tukiona baada ya kukamilisha hilo tutapata furaha.
Lakini tukishapata au kufika tulikotaka, tunapata furaha, lakini ni ya muda mfupi. Kwani baada ya hapo tunaanza kuangalia makubwa zaidi ambayo hatuna.
Hivyo ndivyo binadamu tulivyo, tunachukulia kawaida vile tulivyonavyo na kuvipa umuhimu mkubwa vile ambavyo bado hatujavipata.
Wajibu wako mkubwa ni kujua nini ambacho watu wanataka sana ila hawajapata.
Na kwa jinsi maisha yalivyo, kila mtu huwa kuna kitu hapati kwa kiwango cha kumtosha.
Afya, utajiri na mahusiano ni maeneo ambayo watu hawajapata kwa viwango vya kutosha.
Hivyo ukiweza kuwaonyesha watu jinsi kile unachowashawishi kinakwenda kuwapatia hayo, utasikilizwa.
Kusifiwa, kuthaminiwa na kusikilizwa ni vitu ambavyo imekuwa adimu kwa watu kuvipata. Watu wanavipenda sana, lakini hawapo watu wa kuvitoa, kwa sababu kila mtu ametingwa na yake.
Wewe unapokuwa mtu wa kuvitoa hivyo kwa wengine, kwa dhati kabisa kutoka ndani ya moyo wako, unakuwa na ushawishi zaidi kwa wengine.
Uzuri ni kwamba, hakuna binadamu aliyeridhishwa na maisha yake kwa asilimia 100. Kila mtu kuna vitu anavitaka kwenye maisha yake.
Wajibu wako ni kujua nini ambacho mtu anataka sana na hajapata kisha mwonyeshe jinsi unavyokwenda kumpatia.
Hilo litakupa ushawishi mkubwa kwa wengine na kuweza kupata kila unachokitaka kwenye maisha yako.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, msingi wetu wa kupata tunachotaka ni kuwapa wengine kile wanachotaka.
Kazi yetu kubwa ni kujua kile ambacho watu wamekosa au wanapata kwa uchache kisha kuwapatia hivyo.
Yaani hata kama hautakuwa vizuri kwenye mambo mengine, ukiweza tu kuwapa watu kile wanachotaka sana, watakupa kile unachotaka pia.
Hapa ndipo pa kupambaniwa na kila anayeyataka mafanikio makubwa.
Kuangalia kile ambacho wengi wamekikosa na waonyeshe jinsi unavyokwenda kuwapatia.
Usibahatishe kwenye maisha, badala yake tumia njia ambazo tayari zimethibitishwa kuweza kuwashawishi watu wakupe kile unachotaka.
Kumbuka; kupata unachotaka, wape wengine kile wanachotaka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe