3362; Matatizo yanapoanzia.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Matatizo yote ya maisha yetu huwa yana mwanzo ambao unafanana.
Hiyo ina maana kama ukiweza kufanyia kazi mwanzo huo, utaweza kuyatatua matatizo hayo.
Na zaidi ya hapo, unaweza kuyazuia yasitokee kabisa.

Chanzo kikuu cha matatizo ambayo tunapitia kwenye maisha ni kukosa udhibiti wa yale ambayo tunapaswa kuwa na udhibiti nayo.
Pale tunapojikuta tumeacha mambo yajiendee kwa mazoea, ndiyo tunajikuta tumetengeneza matatizo ambayo yanatuathiri sana.

Umasikini huwa hauanzii kwenye kukosa fedha, bali kwenye kukosa udhibiti wa fedha.
Unaweza kukuta watu wawili, ambao wanaanza na kipato kinacholingana, lakini baada ya muda mmoja anajenga utajiri wakati mwingine anabaki kwenye umasikini.
Tofauti inaanzia kwenye udhibiti wao kwenye fedha.
Yule ambaye hawezi kueleza fedha yake inaenda wapi, anaishia kubaki kwenye unasikini.
Maana yake ni kila anapopata fedha, anafanya kila matumizi yanayokuja mbele yake na hivyo kushindwa kuweka akiba au uwekezaji.

Kadhalika kukosa uzalishaji, huwa hakuanzii kwenye kukosa muda.
Watu wote tuna muda sawa, wa masaa 24 kwa siku.
Tofauti inaanzia kwenye jinsi tunavyotumia muda huo.
Wenye uzalishaji na ufanisi mkubwa huwa wanapangilia na kudhibiti muda wao, kwa kuweka vipaumbele na kuvifuata.
Huku wasio na uzalishaji na ufanisi ni watu wa kwenda na mihemko, kufanya kila linalokuja mbele yao.
Wanaishia kuchoka, lakini wanapoangalia hakuna makubwa wanayokuwa wamefanya.

Kupata mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka, unapaswa kuwa na udhibiti mkubwa wa vitu vyote vinavyoanzia ndani yako.
Kila kitu kilocho ndani ya uwezo wako kudhibiti, unapaswa kuwa na udhibiti mkubwa juu yake.
Usikubali kuendesha maisha yako kwa mazoea au mihemko.
Badala yake yaendeshe kwa nidhamu kali sana ya kupanga na kufanya bila ya kuyumbishwa na chochote.
Nidhamu kali itakuepusha na mengi ambayo yamekuwa yanawakwamisha watu wengine.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, nidhamu na udhibiti ni vitu tunavyovifanyia kazi kwa ukubwa sana.
Tunapangilia kila kitu kabla na kufuata mpango huo bila kuyumba.
Tunapangilia fedha kabla hata hatujaipokea na kufuata mpango huo baada ya kuipokea bila kukubali kuyumbishwa.
Tunapangilia muda kabla hatujaufikia na kufuata mpango huo bila kuhangaika na mengi yanayojitokeza.
Tunajua kila rasilimali yetu muhimu ilipo na inachofanya kwenye kutuletea mafanikio makubwa tunayoyataka.
Huo ndiyo udhibiti tunaousimamia na unaotupa mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Simamia vizuri udhibiti wa rasilimali zote za maisha yako ili uweze kuzitumia kwa manufaa kujenga mafanikio unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe