Habari Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kwa muda mrefu bila kuacha. Tumejipa angalau miaka 10 (2024 – 2034) ya kwenda na uwekezaji tunaoufanya kwa msimamo bila kuacha au kutoa uwekezaji huo.

Kwenye somo lililopita tulijifunza dhana ya riba mkusanyiko na nguvu yake kwenye uwekezaji. Tuliona jinsi ambavyo faida kubwa ya uwekezaji haitokani na mtaji tunaoweka, bali ukuaji wa mtaji huo.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza muda unaohitajika ili uwekezaji unaofanya uweze kukua mara mbili. Kama tulivyoona kwenye riba mkusanyiko kwamba sehemu kubwa ya ukuaji inatokana na marejesho, inawezekana kujua kwa kiasi cha riba inayopatikana, ni muda kiasi gani uwekezaji huo utakua mara mbili.

KANUNI YA 72.

Kanuni ya 72 ndiyo inayotumika kupima muda ambao itachukua kwa uwekezaji kukua thamani yake mara mbili. Hapa ni pale uwekezaji unapofanyika bila ya kutolewa na riba kuwa mkusanyiko.

Kukokotoa muda huo, unachukua namba 72 na kuigawa kwa kiwango cha riba inayopatikana kwa mwaka kwenye uwekezaji huo.

Kwa mfano kama uwekezaji unazalisha riba ya asilimia 10 kwa mwaka, kujua muda ambao itachukua uwekezaji unaofanya kukua thamani mara mbili, unachukua 72 na kugawanya kwa 10 ambapo unapata 7.2 (72/10 = 7.2).

Hiyo ni miaka 7 na miezi 2 na nusu, ambapo uwekezaji unaokuwa umefanya thamani yake inakuwa ni mara mbili ya kiasi ulichoweka.

Kama umewekeza milioni 1 na kuiacha bila kuigusa, baada ya miaka 7 inakuwa imekuwa milioni 2. Unaweza kuona hapo jinsi uwekezaji unavyokuwa na nguvu ya ukuaji.

UKUAJI KWENYE UWEKEZAJI ENDELEVU.

Kanuni ya 72 inapima ukuaji wa uwekezaji kwa kiasi kilichowekezwa mara moja na kuachwa bila ya kuguswa. Uwekezaji unakuwa na nguvu zaidi pale unapokuwa endelevu bila kutolewa.

Kwa mfano pale uwekezaji unapofanyika kila wiki au kila mwezi kwa mwendelezo, ina maana kila kiasi unachoweka, kinakua kwa kanuni hiyo ya 72. Na ndiyo maana unakuja kukuta unapata ukuaji mkubwa mbeleni, hata kama ulianza na kiasi kidogo cha uwekezaji.

Na hii ndiyo nguvu tunayonufaika nayo kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU, tunaendelea kufanya uwekezaji mdogo mdogo kila wiki na kwa riba mkusanyiko na kanuni ya 72, uwekezaji huo unakua kadiri muda unavyokwenda.

Tunaona pia kwa nini kadiri uwekezaji unavyokuwa wa muda mrefu, ndivyo pia ukuaji unakuwa mkubwa. Hii ndiyo sababu tumechagua kufanya uwekezaji kwa muda mrefu bila kuingilia.

SOMA; Dhana Ya Riba Mkusanyiko Na Nguvu Yake Kwenye Uwekezaji.

MFANO WA KANUNI YA 72 KWENYE UTT AMIS.

Mfuko wa Umoja wa UTT AMIS ulianza mwaka 2005 kwa thamani ya kipande kuwa Tsh 70 kwa mwekezaji na serikali kuongezea kufika Tsh 100. Kwa hiyo tunaweza kusema mwaka 2005 kipande kimoja cha mfuko wa Umoja wa UTT kilikuwa Tsh 100.

Kufika mwaka 2024, kipande kimoja kimefikia thamani ya Tsh 1,000/=, ambapo ni ukuaji wa mara 10 kwa thamani ya awali. Ina maana mtu aliyewekeza milioni 1 mwaka 2005, mwaka 2024 imekuwa milioni 10, bila ya yeye kufanya chochote kile. Ni ukuaji mkubwa sana, ambao ni kwa kipindi kirefu.

Sasa tupime huu ukuaji kwa KANUNI YA 72 tuone ambayo ulikuwa unaenda. Tutaanza na thamani ya kipande ambayo ni Tsh 100 na wastani wa riba ni 12% kwa mwaka.

Kwa kukokotoa 72/12 tunapata 6, ina maana kila baada ya miaka 6, thamani ilikuwa inakua mara mbili.

Hivyo kuanzia 2005 mpaka 2011, thamani ilipaswa kukua kutoka Tsh 100 mpaka Tsh 200.

Kutoka mwaka 2011 mpaka 2017, thamani ilipaswa kukua kutoka Tsh 200 mpaka Tsh 400.

Na kutoka mwaka 2017 mpaka 2023, thamani ilipaswa kukua kutoka Tsh 400 mpaka Tsh 800.

Kutoka mwaka 2023 mpaka 2029, thamani inapaswa kutoka Tsh 800 na kufika Tsh 1,600/=

Na mwisho, kutoka mwaka 2029 mpaka 2035, thamani inapaswa kutoka Tsh 1,600 mpaka Tsh 3,200.

Hivyo ndivyo namba zinavyopaswa kwenda kulingana na kanuni, sasa turudi kwenye historia ya UTT kwa data zinazopatikana kwenye taarifa zake. Katika hivyo vipindi, thamani zilikuwa kama ifuatavyo;

Mwaka 2005, thamani ya kipande Tsh 100, hiki ndiyo kiasi cha kuanzia.

Mwaka 2011, thamani ya kipande Tsh Taarifa haipo kwenye mtandao

Mwaka 2017, thamani ya kipande Tsh 481, kwa kanuni ilitakiwa kuwa 400.

Mwaka 2023, thamani ya kipande Tsh 877, kwa kanuni ilitakiwa kuwa 800.

Tunaona hapo kuna tofauti kidogo ya thamani halisi na thamani ya ukokotoaji, ambapo uhalisia umekuwa mkubwa kuliko makadirio ya ukokotoaji. Hiyo ni kwa sababu riba zimekuwa zinatofautiana kwa miaka.

Lakini matokeo hayo mazuri yanatuonyesha jinsi mambo haya yanavyofanya kazi kwa uhakika na siyo kubahatisha. Tunapoona ukuaji unaotokea kwenye uwekezaji tunaofanya, siyo mazingaombwe wala kubahatisha, bali ni kwa kanuni zinazofanya kazi.

Hili litupe msukumo wa kuendelea kuwekeza kwa sababu tunajua ukuaji upo.

Lakini pia hatupaswi kuacha kuwa na tahadhari kwamba kila uwekezaji una hatari na historia ya nyuma haimaanishi uhakika wa siku zijazo.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe uliyojifunza kwa kujibu maswali hayo hapo chini;

1. Eleza jinsi ulivyoielewa KANUNI YA 72 na kile inachopima kwenye uwekezaji.

2. Elezea ukuaji ambao mfuko wa Umoja wa UTT umepata tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa. Nini kikubwa ulichojifunza kwenye ukuaji huo?

3. Ukiwekeza milioni 1 mwaka huu 2024, kwa riba ya 12% kwa mwaka, itakuchukua miaka mingapi thamani ya uwekezaji wako kufika milioni 8? Onyesha ulivyokokotoa huo muda.

4. Karibu kama una swali lolote kuhusu somo hili au programu nzima ya NGUVU YA BUKU, uliza hapa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.