Kwenye maisha ni wazi kwamba, mafanikio siyo bahati, hayaanguki tu kwa mtu aliyelala na kutamani mafanikio yatokee. Bali mafanikio yanatokea kwa yule anayetaka kufanikiwa.

Ili uweze kuyapata mafanikio ya kweli lazima ufanye vitu sahihi kwa muda sahihi. Moja ya vitu muhimu kufanya ni maandalizi mazuri katika utendaji wako.

Unapokuwa na maandalizi mazuri unaisafisha njia yako. Chochote kinachojitokeza kinakuwa kama tanuru la kuchochea moto katika safari yako. Ndiyo maana tunasema maandalizi ni msingi mkuu wa mafanikio.

Kiwango chako cha maandalizi katika utendaji wako ndicho kinachoamua aina ya matokeo unayoenda kupata.

Mfano, bahati katika mafanikio ni zao la maandalizi mazuri. Na maandalizi haya yanapokutana na fursa kitu kikubwa hutokea.

Ni ngumu kupata lift ukiwa kitandani, lakini ukiwa barabarani ni rahisi kupata lift kwa sababu umefanya maandalizi ya kutosha kutoka nyumbani.

Kazi zetu zipo chini ya kiwango kutokana na kukosa maandalizi mazuri. Mauzo yapo chini kwa sababu ya kukosa maandalizi mazuri ya kuwahudumia wateja.

Kujua unachotaka hakikusaidii kukipata kama hujaweza kuwa na maandalizi mazuri.

Mambo ya kuzingatia ili kuwa na maandalizi;

Moja; Fungua moyo
Kuwa na utayari wa kufanya kitu.
Hufanikiwa katika baadhi ya vitu kwa sababu hupati ushirikiano mzuri na moyo wako.

Mbili; Kuwa na orodha ya mambo ya kufanya
Orodha hii hukusaidia kuwa na mahali pa kupitia.

Tatu; Kuwa na vipaumbele
Hapa unarejea kwenye orodha yako kwa kufanya, kisha kupangilia kipi kianze na kipi kifuate.

Nne; Fanya
Kuwa na orodha na vipaumbele bila kufanya haiwezi kukusaidia mpaka pale utakapoamua kuanza kufanya. Na hapo ndipo unapata matokeo mazuri.

Mtu mwenye maandalizi mazuri huyajua haya katika utendaji wake;

Moja; Gharama
Tuchukulie mfano wa mtu anayeta kusafiri kutoka Dar Es Salaam kwenda Mwanza. Moja ya kitu anachohakikisha kipo sawa ni gharama. Ikiwemo gharama za safari chakula n.k. Kadhalika kwenye biashara. Kama ni simu utajua gharama za vocha, bando au safari.

Mbili; Kujua Mwisho wa jambo kabla halijafanyika.
Siku zote mtu mtu aliyekosa maandalizi huwa hajui ni wapi anaelekea na atafika lini kule
aendako au afanyacho. Ndiyo maana inakuwa rahisi kukata tamaa, sababu kubwa hawajui kitaisha lini au kufanyika lini.

Tatu; Kujua Kiwango cha msaada unachohitaji
Maandalizi mazuri yanakusaidia kujua aina ya msaada unaohitaji kufanikisha kitu. Inaweza kuwa ni msaada wa kifedha, mawazo au ushauri kulingana na kitu husika. Ndiyo maana kuna wakufunzi wa mauzo, fedha, mahusiano na maeneo mengine mengi.

Askari vitani ni hatari sana kuingia vitani bila kujua kiwango cha silaha alizonazo nazo kama zinamudu adui anayeenda  kupigana naye. Kiwango cha maandalizi uliyo nayo kitaamua uwezo ulio nao katika kuyatimiza maono uliyo beba.

Nne; Ni rahisi Kufanya marekebisho.
Mwanafunzi Shuleni hufanya mitihani tofauti kabla ya mitihani wa mwisho. Mitihani ya mock, pre mock na pre NECTA huwa zinafanyika kuhakikisha mwanafunzi anajirekebisha kabla ya mitihani wa mwisho. Hata kwenye mauzo ipo hivyo. Huuzi, hupati wateja ukiwa na maandalizi unaweza kurekebisha makosa yako.

Tano; Maandalizi hupunguza ughairishaji wa mambo.
Moja ya sababu kwanini wengi wetu tunaghairisha mambo ni kutojua jambo linachukua muda gani kukamilika. Hii inatukosesha hamasa na ari katika kulifanya. Ndiyo maana tukichoka kidogo tunaacha kulifanya.

Sita; Maandalizi hufanya mtu kujiamini.
Ukigusia suala la kujiamini huwezi kuweka kando suala la maandalizi mazuri. Hii ni kwa sababu mtu yeyote aliyejaa hofu hawezi kufanya vizuri kitu chochote. Ataogopa sana.

Angalizo; Kupanga ni rahisi, lakini kutekeleza kunahitaji kazi. Kufanikiwa ni kazi ngumu, inayohitaji kujitoa hasa. Hivyo, kuwa na maandalizi mazuri kwa kila kitu unachohitaji kukifanya ni muhimu sana. Unahitaji muda, unahitaji kazi yenye maana ili kupata mafanikio makubwa. Jiandae sasa.


Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.