3363; Siyo kwa ajili ya kila mtu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafunzo na hamasa juu ya mafanikio ni mengi.
Na mafunzo hayo yanayoa matumaini makubwa kwa kila mtu, kwa jinsi inavyoonekana kuwezekana kwa kila mtu.
Watu wanapata msukumo mkubwa wa kuingia kwenye safari ya kupata mafanikio makubwa.
Lakini kwa bahati mbaya sana, wamekuwa hawafiki mbali.
Wengi wanaingia wakiwa wanaangalia upande mmoja pekee, ambao ni wa mambo kwenda kama ambavyo wao wamepanga.
Wanachokuwa hawajaambiwa au wenyewe kufikiria ni kwamba mambo huwa hayaendi kama ambavyo mtu umepanga.
Mara zote mambo huwa yanaenda tofauti.
Hata ujipange kiasi gani, bado kuna vitu vitaenda tofauti na ulivyopanga.
Tukianza kwenye muda, mara zote mambo yatachukua muda mrefu kuliko ulivyotegemea. Hata kama kwenye mipango yako utaweka muda wa ziada wa kufidia, bado muda utakaohitajika utakuwa mwingi kuliko ulivyotegemea.
Kwenye gharama pia, zitakuwa kubwa kuliko ulivyotegemea. Itakuchukua gharama kubwa kuliko ulivyotegemea au kupangilia. Hiyo ni hata kama uliongeza gharama za ziada.
Pagumu zaidi ni kwenye ugumu wa safari nzima, huwa inaishia kuwa ngumu kuliko unavyotegemea au kujiandaa.
Utakutana na magumu na changamoto ambazo hukuzitegemea au kujiandaa nazo.
Hapo ni hata kama ulijiandaa kwa magumu.
Kwa kifupi ni kwamba, uwezo wetu wa kutabiri kwa usahihi chochote kinachokuja ni mdogo sana.
Hivyo kama tunaingia kwenye safari ya mafanikio, ni lazima uwe umejikana.
Lazima ukubali kupambana na kukabiliana na kila kitakachokuja mbele yako.
Lazima ujitoe hasa ili kubaki kwenye safari hiyo bila ya kutetereshwa na chochote.
Siyo kila mtu yupo tayari kujitoa na kuteseka kiasi hicho.
Wengi wanataka kwenda na maisha yao kwa ukawaida, wasijisumbue na mengi makubwa.
Na hakuna ubaya wowote kwenye hilo.
Kwa sababu, lolote kubwa ambalo mtu analitaka, linamtaka ajitoe hasa.
Kujitoa siyo tu kwenye kuweka kazi, japo hilo ndiyo kubwa.
Ni kwenye uvumilivu wa hali ya juu pia, kwa sababu magumu sana yatapitiwa.
Ni kwenye upweke wa safari nzima, kwa sababu wengi hawataiweza, hivyo kwa sehemu kubwa mtu anakuwa peke yake.
Kukatishwa tamaa ni kitu kikubwa ambacho kila anayeingia kwenye safari ya mafanikio atakutana nacho. Ni lazima mtu awe imara sana kiroho kuweza kuendelea na safari bila ya kukata tamaa.
Baada ya kupitia yote hayo, mwisho wa hiyo safari ni nini?
Tumezoea hadithi nyingi mwisho wake ni mzuri, mwisho wa raha na starehe.
Lakini mwisho wa safari ya mafanikio ni tofauti, ni kushindwa na maumivu.
Kila mtu kwenye safari ya mafanikio lazima apitie kushindwa na maumivu makali.
Wengi huo ndiyo unakuwa mwisho wa safari zao.
Kwa wachache ambao ndiyo wanayapata mafanikio makubwa, huwa wanaendelea licha ya kukutana na kushindwa na maumivu.
Ni wachache sana wanaoweza kupitia hayo yote na bado wakabaki imara na kuyapata mafanikio makubwa.
Ndiyo maana licha ya wengi kuyataka mafanikio makubwa, bado siyo kwa ajili ya kila mtu.
Wengi ambao hawapo tayari kujitesa vile inavyohitajika, hawatayapata mafanikio makubwa wanayoyataka.
Na hiyo ni sehemu ya maisha.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kila mwanachama amejikana hasa kuyapata mafanikio makubwa.
Ameyakubali mateso na hata kifo kwenye kuyapambania mafanikio makubwa mpaka kuyapata.
Hakuna kingine kilicho muhimu zaidi ya mafanikio hayo makubwa.
Kushindwa au kuishia njiani ni mijadala ambayo haipo kabisa kwenye hii jamii.
Pamoja na magumu na changamoto ambazo kila mmoja anapitia, shauku ya kupata mafanikio makubwa ipo juu sana na haipoozwi na chochote.
Hata hayo mafanikio yenyewe, hayapoozi shauku iliyopo, bali yanazidi kuichochea.
Kwamba kadiri mtu anavyopata matokeo mazuri, ndivyo anavyozidi kupata msukumo wa kuendelea kufanya kwa ukubwa zaidi.
Kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA ni kujikana kwa ajili ya mafanikio makubwa, ambayo utayapata na kwenda mbele zaidi au utakufa ukiwa unayapambania.
Hakuna kingine zaidi kwenye hilo.
Na hayo ndiyo maamuzi bora kabisa ambayo mtu anaweza kuyafanya kwenye maisha yake.
Maamuzi yatakayoacha alama kubwa kwake.
Fanya maamuzi haya na nenda nayo kwa maisha yako yote.
Utajenga maisha bora na ya kipekee kabisa kwako.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe