Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja ninachokiamini bila ya shaka yoyote ile ni kwamba, mtu yeyote mzima na ambaye ana afya kamili, anaweza kuongeza kipato chake mara moja kwa kuanzia popote pale alipo.
Hapo namaanisha kama mtu hana kabisa njia ya kuingiza kipato, anaweza kuanzia hapo hapo na kuanza kuingiza kipato. Kama mtu ameajiriwa na mshahara ni mdogo, anaweza kuanzia hapo hapo na kuongeza kipato. Na kwa aliye kwenye biashara lakini mauzo ni kidogo, anaweza kuanzia hapo hapo na kukuza mauzo yake.

Njia ninayoiamini sana ya kuongeza kipato, ambayo ni ya uhakika na haihitaji vigezo vyovyote vile ili kuitumia ni MAUZO. Kwa kufanya mauzo, mtu yeyote yule anaweza kuongeza kipato chake mara moja kwa kuanzia pale alipo. Yaani haimtaki mtu awe na elimu fulani au uwezo fulani, ni yeye tu kuwa tayari kuongea na watu na kupata kile anachotaka.
Kwenye maisha, kila kitu ni mauzo, yaani kila unachofanya ni kuuza. Hiyo ni kwa sababu chochote unachotaka kwenye maisha yako, unahitaji kuwashawishi wengine wakupe. Kuanzia fedha ambazo ndiyo unazitaka sana, hutazitengeneza au kuziiba, bali utahitaji kuwashawishi wengine wakupe. Hapo kwenye kushawishi wengine wakupe unachotaka ndipo mauzo yanapohusika.
Kwa hiyo tunachokubaliana hapa ni kwamba, kama unataka kuongeza kipato chako kwa kuanzia hapo ulipo sasa, anza kuuza. Huenda huelewi utauzaje au utauza nini, wacha tupate mifano.
Kama unaanzia chini kabisa, yaani huna njia yoyote ya kuingiza kipato, angalia kitu unachopenda kufuatilia, kuzungumzia au kutumia kisha tafuta wengine ambao pia wanakipenda. Nenda kwa ambao wanauza kitu hicho kisha waambie una wateja unaoweza kuwashawishi wakanunua kwake na unakwenda kuwashawishi wanunue kisha yeye atakupa kamisheni kwenye kila mauzo. Au unaweza kuongea naye akakupa na ukaenda kuwauzia kisha ukamlipa na kubaki na kamisheni. Kabla hujaendelea kujiambia hakuna atakayekubali nikuhakikishie jambo moja, kila biashara inakazana kupata mauzo makubwa zaidi. Hivyo ukimwendea mfanyabiashara yoyote na kumhakikishia kuuza, lazima atakupa hiyo fursa.
Kama umeajiriwa na kipato chako hakitoshelezi, anza kwa kutekeleza majukumu mengi na makubwa zaidi kwa mwajiri wako. Mpe thamani kubwa zaidi ya anavyopewa na wengine. Mfanye akutegemee kwa namna ambayo usipokuwepo mambo yanakwama. Na yeye mwenyewe atajikuta anakuongezea malipo. Najua kama umeajiriwa kwa muda mrefu utasema hilo haliwezekani, kwani umeshafanya kazi sana ila huonekani. Lakini hilo siyo kweli, hujaweka kazi ya kutosha. Nakushauri nenda kaweke kazi ya kutosha na kama mwajiri wako hataiona thamani yako, kuna wengine wataiona na kukupa fursa nzuri zaidi. Na zaidi, kama kweli unaweka kazi kubwa sana na huthaminiwi, kwa nini bado unaendelea kuwa hapo? Kwa nini hutafuti kwenda pengine? Kwa nini usifanye vitu vyako vya pembeni? Naamini unapata ujumbe ninaokupa hapo.
Na mwisho, kama unafanya biashara lakini mauzo siyo ya kuridhisha, una vitu viwili vya kufanya kila wakati. Kitu cha kwanza ni kuwafikia wateja wengi wapya, ambao bado hawajajua kuhusu biashara yako. Hapo unahitaji kupiga kelele kubwa sana. Kitu cha pili ni kuwafuatilia wote ambao wameshasikia kuhusu biashara yako kwa msimamo bila kuacha. Yaani unawafuatilia kiasi kwamba wanaendelea kukukumbuka na pale wanapokuwa na uhitaji hawana pengine pa kwenda isipokuwa kwako.
Yafanye hayo rafiki yangu na utaweza kuongeza kipato chako mara dufu kwa kuanzia hapo ulipo sasa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua vizuri dhana hii ya kuongeza kipato chako kupitia MAUZO, karibu ujifunze ili uongeze kipato chako kwa uhakika.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.