3364; Suluhisho unalijua.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Najua unazo changamoto mbalimbali zinazokukabili kwenye maisha yako.
Changamoto ambazo zinakuwa kikwazo kwako kuyaishi maisha yako kwa namna ambavyo unataka.

Umekuwa unazielezea changamoto hizo na jinsi zinavyokukwamisha.
Umekuwa unaonyesha jinsi ambavyo unataka kuzitatua changamoto hizo ili maisha yako yawe bora.
Lakini bado umekuwa unabaki nazo na zinaendelea kukukwamisha.

Sehemu kubwa ya changamoto ulizonazo zinaweza kutatuliwa na fedha.
Hiyo ina maana ukiwa na fedha zaidi, unaweza kutatua changamoto nyingi zinazokukabili kwa sasa.

Hivyo basi, suluhisho la changamoto hizo nyingi unalijua, ambalo ni kuongeza zaidi kipato chako.
Licha ya kujua suluhisho hilo kuu la changamoto zako, bado umekuwa unaendelea kuhangaika na changamoto.

Kikubwa ambacho ungepaswa kuwa unakifanya ni kupambana ili kuongeza kipato chako.
Ukishajua changamoto uliyonayo inatatuliwa na kipato zaidi, basi hupaswi hata kuwa unaielezea elezea kwa wengi.
Badala yake unapaswa kuwa umetingwa na kuongeza kipato chako ili kutatua changamoto hiyo.

Kwenye biashara hili ndiyo liko dhahiri kabisa.
Hakuna changamoto yoyote ya biashara ambayo haiwezi kutatuliwa na kuwepo kwa mzunguko mzuri wa fedha.
Na mzunguko mzuri wa fedha unatokana na kuwepo kwa mauzo ambayo ni makubwa na mazuri.
Hilo linafanya suluhisho la changamoto zote za biashara kuwa mauzo makubwa na mazuri.

Haijalishi unapitia changamoto gani kwenye biashara yako, sulihisho unalijua ambalo ni kuongeza zaidi mauzo.
Hicho ndiyo kitu unachopaswa kuwa unapambana nacho zaidi pale biashara yako inapokuwa na changamoto.

Ni jambo la kushangaza sana pale unapokuwa unalijua suluhisho la changamoto unazopitia, lakini bado hulifanyii kazi.
Unahangaika sana na changamoto zenyewe kuliko unavyohangaika na suluhisho la uhakika.

Kwa jinsi ambavyo suluhisho la changamoto nyingi liko wazi, lakini bado watu wanazilalamikia changamoto hizo, inajidhihirisha wazi kwamba watu wanazipenda zaidi changamoto hizo kuliko kuzitatua.
Kwa kuwa watu wakifanyia kazi suluhisho la changamoto hizo watawajibika moja kwa moja pale wanaposhindwa kutatua, wamekuwa wanachagua kutokutatua.
Hiyo ni sawa na mtu aliyeumia mahali, lakini hataki kupatibu kwa sababu atakosa maumivu ya kujitetea nayo.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, maana ya changamoto au tatizo ni tofauti kabisa kwetu.
Tunapokuwa na tatizo au changamoto zinazotukabili, swali la kwanza tunalojiuliza ni je linaweza kutatuliwa na fedha zaidi?
Kama jibu ni ndiyo basi hatuliiti tena changamoto au tatizo, bali tunaweka mpango wa kuongeza fedha ili kutatua.

Tukishajua suluhisho la changamoto au matatizo yoyote tunayokuwa tunapitia, tunaachana nayo na kupambana na suluhisho ambalo tumelipata.
Kwa njia hiyo tunazitatua changamoto nyingi kwa haraka zaidi.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tumeweka kipaumbele kikubwa kwenye kuongeza kipato na kujenga utajiri kwa sababu tunajua fedha zinatatua sehemu kubwa ya matatizo na changamoto.
Hivyo kwa kuwa nazo nyingi, inakuwa ni kinga nzuri kwa matatizo ambayo yanaweza kujitokeza.

Wajibu wako kila wakati ni kupima ni kinga kiasi gani ambayo tayari umeshajijengea.
Kila wakati endelea kuimarisha kinga yako kwa kuongeza kipato chako na kujenga utajiri mkubwa.

Jua suluhisho la kila tatizo au changamoto uliyonayo na juhudi zako zote zipeleke kwenye suluhisho kuliko matatizo na changamoto hizo unazokuwa nazo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe