Rafiki yangu mpendwa,

Huwa tunatamani maisha ambayo hayana changamoto wala matatizo yoyote yale. Tunataka maisha ambayo tunapata kila tunachotaka na kuwa na furaha muda wote.

Lakini hayo siyo maisha yanayowezekana kwa sisi binadamu kwa sababu hata yangewezekana, yangekosa kabisa maana.

Changamoto, matatizo na mateso tunayoyapitia kwenye maisha ndiyo yanayafanya maisha yetu kuwa na maana. Ni katika kuyakabili na kuyavuka ndiyo tunakamilisha wajibu wa maisha yetu hapa duniani.

Pamoja na mateso kuwa sehemu ya maisha, bado wengi wamekuwa wanaumizwa nayo na kuyalalamikia. Na hiyo ni kwa sababu ya mtazamo usiokuwa sahihi ambao wanao kuhusu mateso wanayokuwa wanayapitia.

Mwanafalsafa Marcus Aurelius kwenye kitabu chake cha sita cha Meditations ametushirikisha namna bora ya kukabiliana na mateso ya maisha huku tukiwa imara na kuyafurahia maisha. Ndiyo, inawezekana kabisa kuyafurahia maisha licha ya kuwa unapitia mateso mbalimbali.

Baadhi ya mambo makuu aliyoshirikisha ya kukabiliana na mateso ni kama ifuatavyo;

Moja ni kuumia au kuteseka ukiwa unatekeleza majukumu ambayo ndiyo uliletwa kuyatekeleza hapa duniani ni kitu kizuri. Anasema kama mkono utaumia ukiwa unafanya kazi ya mkono, hakuna tatizo. Tatizo linakuja pale mkono unapoumia ukiwa unafanya kazi ambayo siyo ya mkono. Kadhalika hivyo ndivyo inakuwa kwenye maisha yetu, tunaumia zaidi pale tunapotezeka kwa mambo ambayo hayana maana kabisa kwetu.

Ili kuweza kuyakabili mateso ya maisha, unapaswa kuwa unafanya yale ambayo yana maana kwako, yale uliyoletwa hapa duniani kuyafanya. Kwa maneno mengine ni kufanya yale yanayotoka ndani yako, ambayo unakuwa unayajali zaidi na kufurahia kuyafanya. Ukiwa unafanya hayo, mateso unayokutana nayo hayawezi kukuumiza hata kidogo.

SOMA; Falsafa Ya Ustoa Na Matumizi Mazuri Ya Muda Wako Ili Kufanya Makubwa.

Mbili ni muda wetu hapa duniani ni mfupi sana. Marcus anaanza kwa kuorodhesha watu maarufu na waliokuwa na madaraka makubwa ambao waliwahi kuwepo duniani, ila wote wameshakufa. Anatutaka tuone jinsi ambavyo maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana, ukilinganisha na umri ambao dunia inao. Hiyo ina maana kwamba hata kama unapitia mateso gani, yana mwisho wake. Ni labda utayatatua kuyamaliza au utakufa na huo utakuwa mwisho wa mateso hayo.

Kuyakabili mateso unayokuwa unapitia, jikumbushe kwamba ni ya muda tu, yatafika mwisho wake kwa yenyewe kuisha au wewe kufa. Sasa ya nini ujitese na mambo ambayo siyo ya kudumu? Wewe fanya sehemu yako na mengine uachie muda utayatatua wenyewe.

Tatu ni kujenga mahusiano mazuri na wale wanaokuzunguka. Watu wengi hufikia hatua mbaya pale wanapopitia mateso kwa sababu ya upweke. Wengi wanaopata mawazo ya kujidhuru na kujiua ni kwa sababu wanaona maisha yao yanakosa maana. Chanzo cha kuona maisha ya maana ni upweke wanaokuwa nao na kudhani wengine hawawajali. Kumbe kwa sehemu kubwa wao ndiyo wanakuwa wamejitenga na hao wengine.

Kukabiliana na mateso ya maisha, mara zote imarisha mahusiano yako na watu wako wa karibu. Bila ya kujali unapitia nini, hakikisha una watu wa kuongea nao, watu ambao wanaweza kukusikiliza bila ya kukuhukumu. Kuweka mambo mengi ndani yako inakusababishia msongo ambao utaathiri afya yako na kupelekea kuyadhuru maisha yako.

Maisha unayoishi ndiyo maisha yako, usiyaendee kama vile unafanya maandalizi ya kuja kuanza kuishi. Hivyo hakikisha unayaishi maisha yako kwa ukamilifu. Matatizo na changamoto unazopitia ni sehemu ya maisha yako na hazitakuja kuisha kama upo hai. Tumia mafunzo haya uliyopata kutoka falsafa ya Ustoa kuweza kujenga maisha yenye maana.

Kujifunza zaidi kuhusu Ustoa na kukabiliana na mateso, angalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.