Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu anayejifunza kuhusu mafanikio, anajua umuhimu wa mtu kuweka malengo ili aweze kufanikiwa kwenye maisha yake. Bila ya malengo, mtu hawezi kupata mafanikio makubwa anayoyataka.

Kwenye maisha, kila kitu ambacho kina manufaa, huwa pia kinaweza kuwa na madhara kama hakitafanyiwa kazi vizuri. Na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye malengo. Pamoja na nguvu kubwa ambayo malengo yanayo, kama hayatawekwa vizuri, yataishia kuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa.

Na hiyo ndiyo hali ambayo watu wengi sana wamejikuta, kwa malengo wanayojiwekea kuwa kikwazo kwao kupata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka.

Kuna mambo mengi yanayosababisha malengo kuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa na hapa tutakwenda kuangalia moja kubwa ambalo ndiyo linawakwamisha wengi.

Kitu hicho huwa nakiita malengo ya KUBAKA. Malengo ya kubaka ni yale ambayo unakuwa umeyaiga kwa watu wengine. Kwa sababu umesikia watu wanaweka malengo ya aina fulani, na wewe unakimbilia kuweka malengo hayo hayo.

Hii huwa inatokea sana kwa watu wa karibu, ambapo mmoja akiweka malengo fulani ambayo yanaonekana kumpa mafanikio makubwa, wanaomzunguka nao wanaweka malengo ya aina hiyo hiyo.

Hakuna ubaya wowote kwenye kuweka malengo makubwa na ambayo yatampa mtu mafanikio makubwa. Ila kuna tatizo kubwa pale mtu anapoweka malengo kwa kuiga watu wengine. Kwani malengo hayo huwa yanageuka kuwa magumu sana kwao kuyakamilisha.

Kuweka malengo ni hatua moja na ndogo sana kwenye kupata mafanikio. Kuyapata mafanikio unahitajika kufanyia kazi malengo kwa juhudi kubwa sana. Utakutana na magumu na changamoto nyingi, ambazo utapaswa kuzivuka ndiyo ufanikiwe.

Utaweza kuyakabili hayo yote kama malengo unayofanyia kazi yameanzia ndani yako. Kwa malengo kuanzia ndani yako yanakuwa na maana kubwa kwako ambayo inakupa msukumo wa kuyapambania.

Lakini kama malengo umeyaiga kwa wengine, unapokutana na magumu na changamoto hutaweza kuendelea kuyapambania. Badala yake utakata tamaa na kuachana na malengo hayo.

Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao, mwaka mpya wanabaka malengo ya wengine, wakianza kuyafanyia kazi wanakutana na vikwazo na kuamua kuacha nayo. Wanasubiri tena mpaka mwaka mpya mwingine kurudia zoezi hilo ambalo halijazaa matunda.

Rafiki, hebu shtuka na utoke kwenye huo mzunguko wa malengo ya kubaka na yanayokuzuia kupata mafanikio makubwa. Amua sasa kukaa chini na kujiwekea malengo yako mwenyewe, ambayo yana msukumo kutoka ndani yako.

Hayo ndiyo malengo ambayo utaweza kuyapambania kwa kila namna mpaka kuyafikia. Jikumbushe maisha siyo mashindano na watu wengine, bali maisha ni yako kuyaishi. Kazana kuyaishi maisha yako kwa namna ambayo ni sahihi kwako na utaweza kupata mafanikio sahihi kwako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha kwa kina zaidi kuhusu tatizo hili la malengo kuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa. Karibu ufungue kipindi hapo chini na kujifunza ili kubadili maisha yako kupitia kuweka malengo sahihi kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.