3366; Kujiongezea mizigo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio ni magumu, hata kama utafanya kazi kwa akili na juhudi kubwa.
Utakutana na magumu na changamoto za kila aina.
Huo ni uhalisia ambao kila mtu anakutana nao kwenye safari yake ya mafanikio.

Sasa basi, baadhi wamekuwa wanazidisha ugumu wa safari zao za mafanikio kwa kujiongezea mizigo ambayo inawaletea changamoto nyingi zaidi na zinazowakwamisha.

Na mzigo mkubwa sana ambao watu wamekuwa wanaingia nao kwenye safari ya mafanikio ni mtazamo usiokuwa sahihi juu ya mafanikio.

Watu wanayafanya mafanikio kuwa magumu sana kwao pale wanapokuwa hawayapi kipaumbele kikubwa kuliko mengine yote.
Pale watu wanapoyachukulia mafanikio kama kitu cha kawaida, yanakuwa magumu sana kwao.

Mafanikio yanataka mtu kuweka umakini wake wote kwenye kuyapambania.
Mafanikio yanataka kupewa umuhimu mkubwa kuliko vitu vingine vyote.

Kama una jukumu la kufanya kwenye kuyajenga mafanikio, lakini ukaahirisha jukumu hilo kwa sababu yoyote ile, umeonyesha wazi kwamba hayo mafanikio siyo kitu muhimu zaidi kwako.

Mafanikio makubwa yanataka umakini wa kupanga mambo ya kufanya na kuyafanya kama ulivyopanga.
Yanataka mtu usahau mambo mengine yote pale unapokuwa unayafanyia kazi mafanikio yako makubwa.

Kufanikiwa, lazima ujitoe kweli kweli kwenye mafanikio hayo, tofauti na hapo safari yako itashindikana.
Siyo itakuwa ngumu, maana ugumu tayari kila mtu anaupitia, kwako ni itashindikana kabisa.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunayapa mafanikio heshima ambayo yanastahili. Tunayapa umuhimu namba moja kwenye maisha yetu. Tunafanya yale yanayohitajika kufanyika mara zote bila kuacha.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, mafanikio ndiyo lugha kuu. Hakuna mazungumzo mengine muhimu kuliko kujenga mafanikio.
Fikra za kukata tamaa na kuacha kwa sababu ya magumu, hazipewi nafasi kabisa.
Ugumu na changamoto vinajulikana kuwepo, hivyo havishangazi kabisa.

Tunachukua kila hatua kupunguza mizigo ambayo tunakuwa nayo kwenye hiyo safari ili tuweze kukabiliana na kila tunachokutana nacho.
Tunajua kila wakati tunapambana na makubwa zaidi, hivyo tunahakikisha hatujikwamishi sisi wenyewe kwenye kuyavuka ili kupata mafanikio tunayoyataka.

Pamoja na ugumu wa safari ya mafanikio, tuna uhakika wa kuyapata kwa uendelevu kwa sababu hakuna kitu kingine muhimu zaidi kwetu kuliko kupata mafanikio tunayoyataka.
Tuyapambanie kwa ukubwa bila kuchoka wala kuacha.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe