Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.

Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.

Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Kila wakati kwenye biashara ni wa kusaka wateja wapya na hivyo kila muuzaji anapaswa kutumia njia mbalimbali kukamilisha hilo.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafikia wateja wengi kwa kutumia mfumo wa Whatsapp Status.

Kwenye somo lililopita tulijifunza jinsi ya kutumia Whatsapp Broadcast kuwafikia wateja wengi kwa wakati mmoja, kwa kupelekea ujumbe mmoja kwa wengi badala ya kupeleka kwa mtu mmoja mmoja.

Kwenye somo hili tunakwenda kuangalia upande mwingine wa whatsapp ambao ni kutumia Status.

Whatsapp status ni kama ubao ambao unaweka taarifa mbalimbali na wale wanaopita kuweza kuona. Tofauti na broadcast ambapo ujumbe unaenda kwa mtu moja kwa moja, status ni mpaka mtu aingie kuangalia na akutane na kile ulichoweka.

Wakati broadcast inakuhakikishia kuwafikia watu kwa urahisi, status inategemea watu kuchukua hatua ya kuja kuangalia. Pamoja na kutokuwa na ufanisi kama broadcast, bado status ni njia muhimu ya kutumia kuwafikia wateja wengi kwenye biashara.

Tukitumia mfano rahisi kueleweka, ni sawa na unatoa vipeperushi vyenye habari kuhusu biashara yako. Kwa broadcast ni sawa na unapita nyumba kwa nyumba kugawa vipeperushi hivyo, hii inakupa nafasi kubwa zaidi ya kuwafikia watu. Kwa status ni sawa na kubandika kipeperushi mahali, ambapo mtu kukiona ni mpaka aende akakisome.

Ili watu waweze kuona status ambazo unaweka, ni lazima wawe wamehifadhi namba yako ya simu kwenye wasap zao na wewe umehifadhi namba zao kwenye wasap zao. Kama hawana namba zako za simu, hawataweza kuona status ambazo umeweka.

Status huwa zinapangwa kulingana na muda ambao zimetumwa, hivyo kwa mtu ambaye ana namba nyingi za simu, atakuwa na status nyingi zinazoonekana kwake, huku zile za muda wa karibuni zaidi zikiwa juu na zile za muda mrefu zikiwa chini. Hivyo ili kuongeza nafasi ya status zako kuonekana na wengi, ziweke mara kwa mara badala ya kuweka mara moja na kuacha.

Hayo mawili ya kuhakikisha namba yako imehifadhiwa na wengi zaidi na kupangilia kuweka status kila baada ya muda fulani ni ya msingi kwenye matumizi ya status kuwafikia watu wengi. Mambo mengine ya kuzingatia kwenye matumizi ya whatsapp status ni kama ilivyo hapo chini.

SOMA; Piga Hizi Kelele Kama Unataka Kufanya Mauzo Makubwa.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA WHATSAPP STATUS KUFIKIA WATEJA WENGI.

1. Weka jumbe za picha au video fupi ambazo zinawavutia watu kufungua ili kuangalia. Hakikisha ujumbe unaoweka unamfanya mteja ashawishike kufungua ili kuona kuna nini. Hilo litapelekea status zako kufunguliwa kwa wingi.

2. Status ziambatane na maelezo ya kuwashawishi wateja kujibu au kuuliza kupata maelezo zaidi. Hilo litafungua uwanja wa mawasiliano na wateja ili kuwaweka kwenye mchakato wa mauzo.

3. Usiweke status nyingi sana kiasi cha watu kuchoka kuangalia au kupita kwa haraka ili kufika ya mwisho. Angalia idadi sahihi ya status kwako kuweka na pishanisha muda wa kuziweka badala ya kuweka zote mara moja. Kama unaweka status kumi, basi weka status moja kila baada ya saa moja au mbili kila baada ya masaa mawili badala ya kuweka nyingi kwa pamoja. Kila unapoweka unasogea juu zaidi na hivyo kuonekana kwa urahisi zaidi.

4. Jibu status za wateja unaowafuatilia mara kwa mara ili kuanzisha nao mazungumzo mbalimbali. Kama wameweka kitu cha kuwapongeza, wape pongezi, kama wanahitaji pole, fanya hivyo. Kwa kuangalia status za wateja unaowalenga na kuwajibu, utapata mambo mengi ya kuanzisha nao mijadala.

5. Usitumie status kama sehemu ya kutuma tu matangazo ya kile unachouza, bali tumia pia kutoa thamani zaidi kwa wale wanaofuatilia. Shirikisha jumbe nzuri ambazo watu wanaweza kujifunza au vichekesho vizuri ambavyo vinawafurahisha watu. Wafanye watu wawe wanapenda kutafuta status zako kwa sababu wanajua kuna manufaa wanayoyapata.

6. Kama namba unayotumia kwenye whatsapp kibiashara ndiyo namba yako binafsi, epuka kuweka status ambazo zinawafanya watu wakuone huna umakini. Haimaanishi usiweke mambo yako binafsi, weka kwa kiasi maana watu wana tabia ya kutaka kuwajua watu zaidi. Lakini usiweke mambo yasiyo na tija, kwa mfano umegombana na mtu halafu unaanza kumrushia vijembe kwa whatsapp status, haitakuwa na msaada wowote kwako zaidi ya kukufanya uonekane umekosa umakini.

7. Tumia pia mitandao mingine ambayo inatoa fursa ya kuweka status, mfano telegram, facebook, instagrama, tiktok na kwingineko. Kwa sababu hakuna gharama za ziada za kufanya hivyo, sambaza jumbe zako maeneo mengi zaidi.

Huhitaji gharama yoyote wala muda mwingi ili kuweka status kwenye Whatsapp, hivyo kila siku weka utaratibu wa kutuma status na fuata utaratibu huo. Hata kama huoni watu wakikujibu, usiache kuweka, kuna ambao wanakuwa wanafuatilia na siku ukiweka kitu kinachowagusa watakutafuta.

Fanya whatsapp status kuwa bango lako ambalo kila wakati unaweka taarifa mbalimbali za kuwafanya watu wajue kile kinachoendelea na kuvutiwa kuchukua hatua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.