3367; Kuvumilia aibu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Ukiwaangalia wale waliobobea kwenye kile wanachofanya, unaweza kudhani walizaliwa wakiwa wanajua vitu hivyo.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wanafanya kwa viwango vya juu sana, ambavyo vinakuwa vinamshangaza anayetazama.

Lakini ukweli tunaoujua ni kwamba kila mtu unayemuona amebobea leo, kuna wakati alikuwa ndiyo anaanzia chini kabisa, akiwa  hakuna anachojua.
Wakati hao waliobobea wanaanza, kuna wengine wengi walianza nao pamoja.
Lakini ni wachache sana wanaoweza kufikia ubobeza wa hali ya juu. Wengi sana wanaishia kukata tamaa na kuachana na safari hiyo.

Kinachowatofautisha wachache wanaofanikiwa sana na wengi wanaoshindwa ni uwezo wa kuvumilia aibu zilizopo kwenye safari ya mafanikio.

Safari ya kujenga mafanikio makuvwa imejaa vipindi vingi vya kuweka kazi kwa juhudi kubwa, bila kuona matokeo yoyote mazuri. Unahitaji imani kali sana kuweza kuendelea kufanya kwa juhudi wakati hakuna matokeo yanayoonekana.

Kama ugumu hautoshi, kushindwa nako ni nje nje. Pamoja na juhudi kubwa sana unazoendelea kuweka, kushindwa ni kitu kingine ambacho unakutana nacho mara kwa mara.
Mwanzo unaweza kudhani unashindwa kwa sababu zako. Lakini ukweli ni unashindwa kama sehemu ya mafanikio unayoyajenga.

Ni wale wanaoweza kuvumilia aibu ya kushindwa ndiyo watakaweza kupata mafanikio makubwa kadiri ya wanavyotaka.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, aibu kwetu ni kitu ambacho hatukipi uzito wowote.
Tupo kwenye hii safari tukiwa tunajua wazi kwamba mambo siyo rahisi, lakini yanawezekana.
Tunapokosea, tunajitathmini haraka wapi pa kuboresha zaidi na kisha tunaenda kupaboresha.

Kwa sababu mafanikio makubwa unayokuwa unayataka yamejengwa juu ya hatua ndogo ndogo nyingi zinazochukuliwa, wajibu wako ni kuchukua kila hatua inayopaswa kuchukuliwa.
Kama unayataka mafanikio makubwa, kipaumbele chako cha kwanza ni kufanya kila kinachopaswa kufanyika.
Unahitaji ngozi ngumu sana ya kuweza kuvuka magumu, kushindwa na aibu, vitu ambavyo ni sehemu ya kila safari ya mafanikio makubwa.

Kujua huo ukweli ambao wengi hawaujui ni kuwa mbali zaidi na wengi ambao wanahangaika sana ila mafanikio hawayapati.
Kuwa sehemu ya familia ya KISIMA CHA MAARIFA ili uweze kuvuka yote na kujenga mafanikio makubwa kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe